Video na Makala: Mwenge wa Uhuru wa Tanzania



Falsafa, Dhana na umuhimu wa mbio za Mwenge nchini


    Pg 13 Falsafa, Dhana na umuhimu  wa mbio za Mwenge nchini

    HISTORIA ya nchi yetu ni pana na ya kuvutia kwa namna ya pekee ukilinganisha na nchi nyingi za Afrika na Duniani kote.
    Upekee huu unatokana na uwezo wa kujenga hoja na uadilifu wa viongozi wetu, hasa mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipochaguliwa kuwa mjumbe kwenye Baraza la kikoloni la kutunga Sheria (Tanganyika Legislative Council) mwaka 1958.
    Kwa kuwa Mwalimu alikuwa na ndoto ya kuiona Tanganyika na Afrika iliyo huru, mwaka 1958 katika hotuba yake ya kwanza alitamka maneno ya kifalsafa kwa wajumbe na Spika wa Baraza la kikoloni la kutunga Sheria kwa kusema:
     “Sisi tunataka Uhuru wa Tanganyika, Mkitupatia tutauwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje na mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau”.
    Maneno haya aliyarudia tena mwaka 1959 alipohutubia kikao cha 35 cha Baraza la Umoja wa Mataifa kama Mbunge mwakilishi pekee wa Tanganyika.
    Falsafa hiyo ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilikuwa ni kiashiria kikubwa kwa Waingereza kwamba watu wa Tanganyika wamechoka kutawaliwa. Siku Tanganyika ilipopata Uhuru tarehe 09 Desemba, 1961.
    Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliuwasha Mwenge wa Uhuru na akamkabidhi Luteni Alexander Ngwebe Nyirenda na kikosi cha Vijana wenzake wakaupeleka Mwenge wa Uhuru juu ya Mlima Kilimanjaro.
    Mwalimu wakati akitoa hotuba ya siku ya Uhuru; aliwatangazia Watanganyika, Afrika na Dunia kwa ujumla kwa kusema:
     “Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna  matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipo jaa dharau”.
    Luteni Alexander Nyirenda alipandisha Bendera na Mwenge wa uhuru juu ya mlima Kilimanjaro usiku wa kuamkia tarehe 9 Desemba mwaka 1961 ambapo baada  ya  Uhuru wa Tanganyika na kuwashwa kwa Mwenge wa Uhuru,  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wenzake wa awamu ya kwanza walielekeza juhudi zao katika kuwaunganisha Watanzania na kuweka misingi imara ya kulijenga taifa huru la Tanganyika; kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano na kuweka sera za kukabili  maadui ujinga, umaskini na maradhi.
    Awamu hii  ilitafsiri falsafa ya Mwalimu aliyoijenga katika Mwenge wa Uhuru kwa kuweka  misingi madhubuti ya uhusiano wa nje, sera ya kutofungamana na siasa za upande wowote, na kuweka msisitizo mkubwa katika ukombozi wa Bara la Afrika na mapambano dhidi ya ubeberu na vibaraka wao. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimio la Arusha lililosisitiza siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, na kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni matunda ya utelekezaji wa Falsafa ya Mwenge wa Uhuru.
    Mara baada  ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964, Tanganyika iliungana na Zanzibar na kupata Taifa moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haya ni mafanikio makubwa katika kutekeleza falsafa ya Mwenge wa Uhuru kwani Wazanzibar walirejeshewa matumaini yaliyokuwa yametoweka chini ya utawala wa Kisultani.
    Hata baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, falsafa yaMwenge wa Uhuru iliendelezwa kwa kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujenga na kuimairisha misingi ya amani, umoja, uzalendo, upendo, mshikamano na kuhamasisha shughuli za maendeleo katika jamii zetu na kupeleka kwa Watanzania wote ujumbe maalum uliokusudiwa na Serikali kila mwaka.
    Aidha, Mwenge wa Uhuru ni chombo pekee tulichonacho kama taifa cha kuwaunganisha Watanzania na kuwa wamoja kwani haufungamani na itikadi za kisiasa, makabila yetu wala Dini zetu. Mwenge wa Uhuru ni mali ya Watanzania wote.
    Kwa nini Mwenge wa Uhuru husimamiwa na Serikali
    Hadi mwaka 1992, Mbio za Mwenge wa Uhuru zilikuwa zikisimamiwa na kuratibiwa na Chama Tawala.   Baada ya nchi yetu kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992; mwaka 1993 Mbio za Mwenge wa Uhuru zilianza kusimamiwa na Serikali chini ya Wizara yenye dhamana na Maendeleo ya Vijana. 
    Mabadiliko hayo yalikuwa ni kiashiria kikubwa kwa watanzania wote kwamba Mwenge wa Uhuru hauna Chama, hauna kabila na hauna dini isipokuwa ni  kwa ajili ya kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa. Kwa sasa Mbio za Mwenge wa Uhuru zinaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Zanzibar.
    Aidha, rasilimali fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa hutolewa na Serikali na hutengwa na Wizara zenye dhama na kupitishwa na Bunge la bajeti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mwaka wa fedha husika.
    Tangu Mbio za Mwenge wa Uhuru ziasisiwe hadi leo, misingi na madhumuni ya Mwenge wa Uhuru na Mbio zake zimeendelea kuwa zenye manufaa makubwa na zitaendelea kurithishwa vizazi hadi vizazi katika taifa letu.
    Faida na Mafanikio ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa na Kimataifa.
    I.  Mwenge wa Uhuru umekuwa ni chombo muhimu cha kujenga undugu, umoja, mshikamano na kudumisha amani pote unapopita bila kujali itikadi zetu za kisiasa, dini wala makabila yetu. Umuhimu huu unatokana na ukweli kwamba, leo hii tunahitaji kujenga Taifa lenye amani, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa kuliko wakati wowote ule ikiwa ni pamoja na kujenga taifa lisilokuwa na dhuluma, unyonge, rushwa, ubaguzi, ukabila, udini wala vitendo vya kifisadi.
    II.  Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kuhamasisha wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao katika kubuni na kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo katika nyanja za kilimo, ufugaji, Uvuvi  endelevu, uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji, umeme na huduma za jamii katika maeneo yote nchini na hasa katika maeneo yasiyofikika kiurahisi.
    Kwa mfano, kwa mwaka 2015 pekee, miradi 1,342 yenye thamani ya Shilingi 463,519,966,467.77 ilizinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi. Kati ya fedha hizo, Shilingi 73,462,492,473. 62 zilitokana na nguvu za wananchi. 
    Hata hivyo, michango yote inayotolewa na wananchi ni ya hiari na hutolewa baada ya wananchi kuhamasishwa na kufahamu umuhimu na matumizi yake ambayo ni kugharamia kwa miradi yao wenyewe.
    III. Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa zikitumika kuelimisha wananchi katika maeneo yote nchini jinsi ya kupambana na maradhi yanayotishia ustawi wa watu wetu kama vile UKIMWI, Malaria na kupambana na matumizi ya Dawa za kulevya. Pamoja na njia nyingine tunazotumia kuwahamasisha wananchi wetu. Bado Mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa ni njia sahihi ya kufikisha taarifa na elimu sahihi ya changomoto hizi kwa watanzania wote.
    IV. Mbio za Mwenge wa Uhuru pia, zimeendelea kuhamasisha na kuimarisha umuhimu wa Muungano kwa watanzania wa pande zote mbili za nchi yetu.
    V. Kimataifa, Mwenge wa Uhuru umeendelea kusimamia dhana ya na maudhui yake ya kumulika hata nje ya mipaka yetu. Kwani umeendelea kuhamasisha amani ndani ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika na Duniani kwa ujumla. Tanzania imeendelea kuwa msuluhishi wa Amani Afrika na mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine Duniani kote na imeshiriki ukombozi wa Bara la Afrika hasa kusini mwa Afrika na kusisitiza juu ya umoja, mshikamano, upendo na amani kwa mataifa hayo.
     VI.  Mwenge wa uhuru umeendeleza falsafa ya kumulika ndani ya mipaka ya taifa letu kwa kumulika uovu katika jamii ikiwemo uzembe, kutowajibika, vitendo vya rushwa na ufisadi katika miradi mbalimbali ya maendeleo na huduma za kijamii nchini.
    VII.  Mbio za Mwenge wa Uhuru pia hutumika katika kuratibu na kutathimini shughuli mbambali za maendeleo zinazofanywa na wadau wa maendeleo na kukusanya taarifa zinazohusu kero za  wananchi ambazo husaidia Serikali katika upangaji na utelezaji wa mipango ya  maendeleo kwa wananchi wake.
     Dhana Potofu dhidi ya Mwenge wa Uhuru.
    Pamoja na maono ya Baba wa Taifa, falsafa ya Mwenge wa Uhuru , faida na umuhimu wa Mwenge wa Uhuru ambao umeelezwa hapo juu, wapo watu wachache ambao huenda kwa sababu zao za kisiasa au maslahi yao binafsi wameamua kutumia nafasi zao na ushawishi wao kuupotosha umma wa Watanzania kwamba Mwenge wa Uhuru haufai kwa kutoa hoja  nyepesi (Cheap arguments). Hoja hizo hizo ni pamoja na:-
    (i)      Falsafa ya Mwenge wa Uhuru haihitajiki sasa kwa Watanzania
    Serikali kama ilivyoeleza hapo juu, inaendelea kusisitiza kuwa falsafa ya Mwenge wa Uhuru na maono ya Baba wa Taifa juu ya taifa hili bado yanaendelea kuishi japo yeye hatupo naye tena kwani ni dhahiri kuwa chombo hiki kinasaidia sana katika jitihada za kuwaunganisha Watanzania, kujenga umoja wa kitaifa, upendo, mshikamano, amani, uzalendo na kuchochea shughuli za maendeleo kote nchini. Kwa sasa Mbio za Mwenge wa Uhuru zinahitajika zaidi kwa lengo la kuhamasisha watu wetu kufanya kazi na kujiletea Maendeleo kama silaha ya kupambana na adui ujinga na umaskini.
    (ii)     Michango wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru.
    Serikali ingependa ifahamike kwa wananchi kuwa, Mbio za Mwenge wa Uhuru zinaendeshwa kwa rasilimali fedha za serikali zinazopitishwa na Bunge. Aidha, pale inapohitajika, wadau kwa hiari yao, husaidia katika kugharamia machapisho ya ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru uliokusudiwa kama jitihada zao katika kuisaidia Serikali kufikisha ujumbe kwa wananchi wengi zaidi. 
    Mbio hizi pamoja na dhana nyingine zilizofafanuliwa hapo awali, unawahamasisha wadau mbalimbali kushiriki na kuchangia kwa hiari shughuli za Maendeleo katika maeneo yao.
    Michango ya wadau katika Halmashauri zetu hujumuisha nguvu za wananchi, Vifaa na fedha taslimu ambazo hutumika katika miradi wanayoibuni na kuitekeleza wenyewe. 
    Lengo la kuwashirikisha wananchi katika miradi yao ya  maendeleo ni  kujenga  moyo wa kujitolea, uzalendo na utaifa kwa wananchi wetu ili  waweze kumiliki miradi inayoanzishwa na kujenga misingi ya uendelevu wa Miradi hiyo.
    Mara nyingi, asilimia ishirini ya kila mradi unaowekewa jiwe la msingi, kuzinduliwa, au kufunguliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru ni sharti itokane na nguvu za wananchi. Serikali inaendelea kusisitiza kuwa, michango hiyo ni ya hiari na matumizi yake huwekwa wazi kwa wanachi kila mradi wakati wa kuzinduliwa au kuwekewa jiwe la msingi.
    (iii) Mikesha ya Mbio za Mwenge wa Uhuru na maambukizi ya VVU/UKIMWI
    Baadhi ya watu wachache wamekuwa wakidai kuwa, mikesha ya Mbio za Mwenge wa Uhuru inachochea vitendo vya ngono zembe vinavyopelekea maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI katika maeneo mbalimbali nchini. Serikali inapenda kufafanua jambo hili kuwa, Suala la mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI ni jambo linalopewa kipaumbele kikubwa katika Mbio za Mwenge wa Uhuru.
    Tangu mwaka 2000 hadi sasa, ujumbe wa mapambano dhidi ya UKIMWI umefanywa kuwa ujumbe wa kudumu na uandaliwa kwa kushirikiana na Tume ya taifa ya kuthibiti UKIMWI (TACAIDS) na kisha kutolewa kwa ufasaha na vijana wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa kila mwaka katika Halmashauri za Wilaya zote zote nchini.
    Lengo likiwa ni kuhakikisha maambukizi mapya ya VVU yanafikia asilimia sifuri katika jamii yetu. Katika kufanikisha azma hii, Mbio za Mwenge wa Uhuru huwafikishia wananchi wote nchini, taarifa sahihi kukusu VVU/UKIMWI kwa njia ya machapisho, sanaa kama vile maigizo, mashahiri na nyimbo, ushuhuda (testimony) kutoka kwa waathirika na hotuba za wakimbiza Mwenge kitaifa ambao huandaliwa na mamlaka husika kabla ya kunza mbio hizi.
    Mbio za Mwenge wa Uhuru pia huhamasisha wananchi kupima VVU kwa hiari na kila siku, wastani wa watu 200 hadi 600 hujitokeza kupima VVU jambo ambalo ni nadra sana kutokea kwa watu wengi kujitokeza kupima VVU kwa wingi  katika program nyingine zinazolenga kuhamasisha upimaji wa VVU.
    Mbio za Mwenge wa Uhuru pia hukemea tabia za unyanyapaa katika jamii, huhamasisha juu ya matumizi sahihi ya ARVs na kuwaelekeza wananchi jinsi ya kujikinga na maabukizi ya VVU. Hivyo siyo kweli kuwa mikesha ya Mbio za Mwenge wa Uhuru inachangia katika maambukizi ya VVU.
    Ni vyema tukafahamu kuwa UKIMWI upo na tabia zetu hatarishi hasa za kufanya ngono zembe ndizo changamoto kubwa tunayotakiwa kuijadili kama Watanzania katika kupambana na ugonjwa huu wa UKIMWI na sio Mwenge wa Uhuru.
    Mwenge huu unatusaidia kupambana na tabia zetu hatarishi ambazo ndizo zimekuwa kikwazo kikubwa katika jitihada za Serikali za kupambana na VVU/UKIMWI.
     Kutokana na umuhimu, dhana na falsafa ya Mwenge wa Uhuru kama ilivyoelezwa :-
    · Serikali itaendelea kujenga mshikamano, umoja, upendo na kudumisha amani miongoni mwa Watanzania kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru.
    · Serikali itaendelea kuutumia Mwenge wa Uhuru kuwahamasisha wananchi kupambana na maadui ujinga, maradhi na umaskini kwa watu wetu.
    · Serikali itaendelea kuutumia Mwenge wa Uhuru kumulika, kufichua na kuchukua hatua dhidi ya watu au kundi la watu wanaojihusisha na vitendo vyote vinavyolihujumu Taifa ikiwa ni pamaoja na vitendo vya kibaguzi, rushwa, ufisadi, ubadhirifu, uzembe na chuki.
     Serikali inapenda kutumia nafasi hii kuwaomba watanzania wote kutambua kuwa, kila taifa lina chimbuko lake, utamaduni wake, na taratibu zake. Mwenge wa Uhuru utabaki kuwa ni chombo muhimu na alama ya Taifa letu.
    Kama Taifa tutaendelea kushirikiana na kuenzi kazi na fikra za waasisi wa Taifa hili. Tushiriki katika shughuli za maendeleo kupitia Mbio za Mwenge wa Uhuru, tuusikilize ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru unapopita katika maeneo yetu, tuutafakari na kuufanyia kazi kwa vitendo kwa maendeleo ya Taifa letu.
    Tujiepushe na biashara na matumizi ya Dawa za kulevya, vitendo vinavyosababisha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na tufanye kazi kwa bidii huku tukiendeleza mshikamo, umoja, upendo, amani na undugu wetu.
    Serikali inatoa wito kwa Vijana ambao ndiyo nguzo ya Taifa, kudumisha chombo hiki kwa faida yetu sote na vizazi vijavyo. 

    ZIJUE MAANA NA FAIDA ZA MWENGE WA UHURU WA TANZANIA

    MWENGE, kwa mujibu wa maana, ni kitu mfano wa kikombe chenye mpini mrefu na utambi ambacho aghalabu huwasha na kukimbizwa katika kusheherekea au kutukuza tukio fulani (Kamusi ya Kiswahili Sanifu, TUKI, OUP, ukurasa wa 295 na Kamusi ya Karne ya 21, LONGHORN, ukurasa wa 375).

    Mwenge unafanana sana na kibatari (koroboi) inayotumia mafuta ya taa. Hata hivyo, mwenge kwa wananchi wengi wa Tanzania ni ishara ya uhuru wa Tanganyika! Imefanywa ishara, kama ilivyoashiriwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyetanganza azimio la kuwasha “mwenge wa uhuru.”

    Historia inatukumbusha kwamba, Mwalimu Nyerere akihutubia Baraza la Kutunga Sheria [LEGICO] wakati huo, mnamo mwezi wa Oktoba 22, 1959 kama Mwenyekiti (Rais) wa TANU na mjumbe wa LEGICO, Mwalimu Nyerere alisema: “Sisi (Watanganyika), tunataka kuuwasha mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau.” Haya yalikuwa maneno yenye “mvuto wa kisiasa,” “hamasa ya kijamii,” na “changamoto ya kiuchumi” kwa kizazi cha vijana wa Tanganyika (wakati ule na enzi zile). TANU ilipokea maneno haya na kuyatumia kama “chachu” ya kuleta mabadiliko.

    Dhana ya mwenge, ukiachilia mbali historia na falsafa ya matumizi yake, kwenye maeneo aliyokulia Mwalimu Nyerere (yaani, Butiama ambako ibada ya mwenge ilikuwa sehemu ya matambiko ya wenyeji wa huko) ilikuwa kichocheo katika dhana ya uhuru.

    Maneno yaliyotumiwa na Mwalimu Nyerere katika kuweka jiwe la msingi la kuwasha mwenge yalikuwa ndio falsafa iliyowaleta Watanganyika chini ya chama ukombozi (TANU) katika kupigania uhuru kwa moyo wa kizalendo na kujitolea kwa hali na mali.

    Vijana, kama sehemu muhimu ya harakati za ukombozi kwa kutumia TANU walichukua alama ya “mwenge” na kuifanya alama yao. Vijana wa TANU (TANU Youth League, TYL) waliufanya mwenge kuwa dira ya maisha ya vijana.

    Hata sasa, na kwa mujibu wa ushahidi wa kadi za Umoja wa Vijana wa CCM, mwenge umeendelea kuwa “Alama ya UVCCM.” Hata hivyo, mada hii ya wiki haiandikwi katika kutafuta nani anamiliki nini na kwa nini kwenye mwenge wa uhuru; isipokuwa ni katika kuwakumbusha wapanga sera kwamba, “falsafa ya mwenge imepoteza maana.” Mwenge haikuwashwa ili ukimbizwe kama upepo unaofuata mwelekeo na kamwe haurudi nyuma! Dhana ya kukimbiza mwenge si falsafa ya kukimbia kutoka ulipowashwa kuelekea utakakozimwa; hasha! Utakuwa ni ujinga kudhani kwamba, “mwenge ni kuuwasha na kuukimbiza huku ukifungua miradi ya pwagu na pwaguzi.” Dhana ya mwenge haiwezi kupimwa kwa mikesha, sherehe na kupita kila pembe ya nchi.”

    Tuanze na nukta ya kwanza; matumaini. Mwenge uliwashwa ili ulete tumaini pale pasipokuwa na matumaini. Suala muafaka la kuuliza hapa ni: matumaini gani mwenge uliwashwa kwayo? Jibu rahisi (na la haraka) ni: uhuru! Falsafa ya uhuru haiwezi kupimwa kwa kutokuwapo kwa wakoloni. Uhuru wa maamuzi ndio lililokuwa lengo la harakati za ukombozi na kujikomboa kutoka kwa utawala wa Uingereza ambao uliweka wasaidizi wake (Gavana) na watendaji wengine waliyewakilisha masilahi ya ukoloni. Uhuru uliyodhamiriwa ni ukombozi wa fikra za kujitawala.

    Mwongozo wa TANU wa 1971 ukurasa wa 3 fungu la nne lilitamka hivi, “...hivi sasa katika Afrika ni kwamba hakujawa na wananchi wa nchi yoyote ya Afrika ambayo wamekwisha fikia kiwango cha ukombozi halisi.

    Afrika bado ni bara la watu waliyomo katika unyonge wa kunyonywa na kunyanyaswa. Ndio kusema kwamba vyama vya siasa vya kimapinduzi katika nchi za Afrika zinazojitawala, kama vile TANU, bado vingali ni vyama vya ukombozi.”

    Ni miaka takriban 41 (sasa) tangu andiko hili litolewe; Tanzania tungali watumwa na tumeshindwa kufanya mapinduzi ya fikra. Inawezekana msomaji ukashangaa kwa nini naandika hapa kwamba, “Tanzania ni watumwa wa fikra.”

    Utumwa wa fikra ni hali inayompata mtu anayejiona yupo huru huku mawazo yake yamefungwa kwenye kutawaliwa. Kwa mtaji huu, anaendelea kuwa mtumwa wa kuwatumikia wakoloni kiuchumi, kisiasa, na kijami kama wakala anayetumika kwa masilahi ya kibinafsi. Wengi wa watumwa wa fikra ni wale wanaopewa nafasi za uongozi (kama dhamana) huku wakitumia nafasi hizo kwa utashi wa mabeberu (na wastakabari) wanyonyaji. Viongozi wengi wa nchi za Afrika, pamoja na Tanzania, ni watumwa wa fikra na wanatawala kama mawakala wa mabeberu. Uhuru umeuzwa kwa utashi wa viongozi wachache waliyejipa mamlaka ya kutawala wananchi wasiyekuwa na satwa kwa misingi ya utawala wa demokrasia za kijeshi.

    Kama lilivyoainisha Azimio la Arusha (05/02/1967) kwamba, “Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyeonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndio uliyotufanya tuonewe, tunyonywe, na kupuuzwa. Sasa tunataka kufanya mapinduzi.” Hakuna mapinduzi ya fikra yaliyoambatana na kuwashwa mwenge uliyodhamiria kuleta matumaini mapya kwenye fikra za wananchi baada ya uhuru!

    Uhuru wa bendera (kwa kuiteremsha Union Jack na kupandisha bendera ya uhuru wa Tanganyika) hakukuleta saada (manufaa) ya moja kwa moja katika kuwaondoa wananchi katika mawazo ya kutawaliwa.

    Viongozi waliyechukua nafasi za wakoloni wamegeuka mbwa-mwitu (waliyevalia ngozi za kondoo) na kuendesha ujambazi wa kiserikali.

    Uongozi wa kisiasa na unaotawala uendeshaji wa shughuli za serikali (kuu na za mitaa) umekuwa ukijivika sura ya ubinadamu kwa kutangaza thamani ya uhuru, haki na usawa ilhali kwa wakati huohuo menejimenti ya uchumi, siasa na jamii ikiwekwa rehani kwa mabeberu na wanyonyaji wa kigeni kwa njia ya ubinafsishaji, unyang’anyi na ujambazi wa kiserikali (kleptocracy).

    Uhuru umepoteza maana; na matumaini yaliyodhaniwa kupatikana baada ya uhuru yamegeuka machungu ya kutawaliwa kiuchumi, kijamii na kisiasa na mawakala (na makuwadi) wa utandawazi wanaolipwa na wanyonyaji kwenye siasa za kimataifa. Hivi ndivyo thamani ya uhuru ilivyopotea na kwa jinsi hiyo; nadhani, kama dhana chanya, mwenge umepoteza thamani pia! Hata kama utabaki kuwa alama ya vijana wa CCM, alama ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alama kwenye baadhi ya vyo vikuu na taasisi za umma (kama Chuo Kikuu Mlimani, Chuo Kikuu Mzumbe, na kadhalika) bado nadhani kuwepo kwake kwenye “alama” hizo kutabaki kama historia iliyokosa mashiko kwa vile falsafa ya mwenge ilikuwa kuleta matumaini kwa wananchi. Kama matumaini ya uhuru hayakufikiwa leo (takriban miaka 50 ya uhuru) yatafikiwa lini?

    Hata wale waliyebudni dhana ya “tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele” sijui walifikiria nini na kwa nini? Sijapa majibu ya dhana hii! Inawezekana, kwa utashi wa waliyebuni falsafa ya Miaka ya 50 ya Uhuru, wana hoja makini na yenye ithibati; muda utatueleza juu yake.

    Nukta ya pili kwenye tamko la kuwasha mwenge ni upendo; kama dhana pana na yenye hitajio la uchambuzi angavu. Mwenge ulisadikiwa uwashwe ili pale penye chuki pawe na upendo! Upendo uliolengwa hapa sidhani kama ni ule wa “mapenzi” ya ngono uzembe ambapo kwenye mikesha ya “mbio za mwenge” vijana wa kike na kiume wanajimwaga kama wapo kwenye “fiesta” huku wanakula na kuponda raha kana kwamba wapo Manhattan (New York)! Upendo uliyodhamiriwa na uwashwaji wa mwenge ni hali angavu ya thamani ya utu na ubinadamu wa kujali, kuhurumiana, kusaidiana katika hali zote, kushirikiana katika uzalishaji mali na kugawana pato la taifa kwa njia za uhuru, haki na usawa. Upendo uliyotakiwa ni kujitolea kwa masilahi ya watu wengine.

    Dhana ya upendo ililenga kauli mbiu ya “kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.” Leo uongozi wa kisiasa umesahau dhana hii; na wananchi waliyo wengi wanaishi kwa chuki; na kuchukiana imekuwa ndio itikadi ya vyama na wanasiasa. Wanasiasa wanachukiana; wanahasimiana, na hata kutaka kuuana kwa sumu na mitego mingine ya kisiasa! Chuki imefanywa sehemu ya siasa kwa wanasiasa na wananchi wa kawaida. Hakuna upendo wa kweli baina ya watu wa jinsi moja na au jinsi tofauti; watu wamekuwa kama wanyama wanaokula nyama na wale wanaokula nyasi: tunawindana kwa kuviziana katika kutafuta ulipizaji wa visasi, kutesana, na kuuana.

    Mateso yanayotokana na chuki za kiwendawazimu yamemfanya binadamu kuwa kama ‘shetani’ mwenye jicho moja au “milihoi” au “popo-bawa” au popo-mnyonya damu (vampire) kwa kutamani damu za wahanga. Binadamu amekuwa mtu wa chuki na roho (ya shetani) anayetamani kuua na au kutesa binadamu wengine! Huyu ndiye binadamu aliyebadilika roho na kuchukua maisha ya kihayawani kwa kutamani kuzima kiu yake ya ufisadi wa kishenzi kwa kukandamiza uhuru, haki na usawa wa watu wengine pasipo haki na makusudi ya uumbwaji wake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kimaumbile. Chuki inayowachukua wanasiasa na watu wengine ndio inayozaa mauwaji na utesaji wa watu wasiyekuwa na hatia (rejea: mauwaji ya albino na vikongwe; mauwaji ya watu wasiyo na hatia; na mateso yanayofanywa kwa watu kiakili, kimwili na kisaikolojia).

    Binadamu amejaa tamaa na uchu wa kihayawani zaidi kuliko wakati wa kabla na baada ya miaka ya mwanzo ya uhuru. Binadamu waliyekabidhiwa uongozi wa chama na serikali na hata kwenye baadhi ya vyama vya siasa, kijamii na kiuchumi wamekuwa walafi, wenye choyo na roho zenye inda na ila ya kutamani kupata zaidi kwa njia zisizokuwa halali!

    Haya na mengine wanayoyaficha kwenye nafsi zao huwapa kiburi na kujenga mazingira ya chuki baina ya watu wenye nacho na wale masikini waliyo wengi. Chuki baina ya wenye nacho na wasiyo nacho (masikini wa kutupwa) hujenga matabaka ya kijamii ambayo kwa sehemu kubwa ndio yanayoongeza upogo (tofauti) baina ya watu wenye hali ya juu kimaisha na watu wa hali ya chini kimaisha. Kuwepo kwa mfumo huu wa maisha unaotokana na roho ya chuki; ndivyo kunavyochochoea uhalifu na vurugu za kijamii.

    Nukta ya tatu na ya mwisho; ni heshima! Kama nilivyogusia hapo kabla, binadamu anahitaji heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake. Heshima ya binadamu inatokana na kazi. Hata hivyo, sote (mimi na wewe) ni mshahidi kwamba, “heshima na utu wa sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania imetoweka kwa kukosa uhuru, haki na usawa katika kazi.” Kazi (ajira) kwa wananchi wengi wa Tanzania ni kilimo, siyo? Jibu la moja kwa moja ni: ndiyo!
    Kama ndiyo; hebu tukitazame kilimo chetu, bado ni cha jembe la mkono (kiserema) na kutegemea mvua kwenye mashamba yasiyokuwa na uwezo wa kuzalisha ziada. Tumekuwa hata wakati mwingine tukitegemea chakula cha msaada kutoka kwa mikoa yenye ziada ya chakula (kwa usaidizi wa serikali) au hata kuomba misaada (kama ilivyowahi kutokea miaka ya 1970).

    Heshima ya wananchi wa vijijini imepungua kwa vile baada ya kutelekezwa sera ya ujamaa vijijini (miaka ya 1970) wamekuwa kama wakimbizi kwenye nchi yao. Maisha magumu na msoto huku wengi wakipoteza uwezo wa kuzalisha na kujikuta wakitumikishwa kwenye mashamba na miradi ya wawekezaji waliyewekeza kwenye ardhi ya wananchi na au hata kuwapora ardhi yao kwa kisingizio cha uwekezaji na au ubinafsishaji. Wananchi wamebaki watumwa kwa kufanyishwa kazi za kijungu-jiko (kishumbutu) ilhali faida ya kazi ikivunwa kwa wingi (wa faida) na wawekezaji.

    Wananchi wamefanywa raia daraja la pili na la tatu. Wawekezaji wamepewa haki zaidi (exclusive rights) na hata wakati mwingine wanafanya wapendavyo; kama vile kuchafua vyanzo vya maji vya wananchi kwa kemikali za sumu na hata kuwaua pale wanapodhaniwa kuvuka mipaka ya miradi ya wawekezaji.

    Kwa hali hizi tatu zilizojadiliwa na kuwekwa hapa (japokuwa kwa muhtasari sana); nadhani ni sahihi kabisa kudhani kwamba, “mwenge wa uhuru umepoteza maana yake ya kifalsafa.” Kama alama, basi imebaki alama isiyokuwa na athari zilizokusudiwa kwenye tangazo la tarehe 22, Oktoba 1959 lilitolewa na Mwalimu Nyerere. Mwenge wa uhuru umebaki kuwa sehemu ya “programu ya kampeni” kwa chama tawala kwa vile mara zote vijana wake ndio wanaopewa nafasi ya kushiriki kwenye harakati zake (na ndio wanaotumia alama hiyo).

    Jitihada za makusudi zinazofanywa na makada mbalimbali wa vyama mbaimbali vya siasa juu ya kuhuisha moyo wa kizalendo kwa kuutumia mwenge wa uhuru zimekuwa zikizimwa na wanasiasa waliyomo ndani ya mfumo wa utawala msonge kwa kile kinachodaiwa kwamba, “mwenge ni alama yao na kamwe hawawezi kukubaliana na mawazo mbadala juu yake.” Hivi ndivyo ilivyo; na ndivyo baadhi ya wanasiasa vijana, wakongwe na vigogo wanavyodhani na kutaka hali hiyo iendelee milele kwa kuwa kwa hali hiyo na mazingira yalivyo chama chao kinanufaika na mfumo wa nchi kukosa (1) matuamaini ya uhuru (2) upendo na (3) heshima ya binadamu. Nchi inaendesha kama shmaba la wanyama ilhali kuna kla sababu ya maisha yenye staha na yenye hadhi ya utu na heshima ya binadamu.

    Mwisho, wakati umefika sasa; tukubali kwamba, “mbio za mwenge zimebaki kuwa udhalilishaji wa falsafa na dhana ya uhuru.” Kwa iuwa hakuna uhuru mahali ambapo hapana matumaini; hakuna uhuru mahali pasipokuwa na upendo; na hakuna uhuru mahali pasipokuwa na heshima ya binadamu.

    Pale mwanzo palipokuwa na Azimio la Arusha wananchi wa Tanzania walikuwa na hakika ya kufanya mapinduzi ya fikra kwa kukataa kuonewa, kunyonywa, kupuuzwa na kudharauliwa; baada ya kupuuzwa Azimio la Arusha na kuchochewa kwa moto wa ujasiriamali wa kisiasa na kuwafanya wanasiasa wa chama tawala kujiingiza moja kwa moja kwenye uwakala wa kuharibu mujtamaa wa ujenzi wa jamii ya watu waliyo sawa na huru.

    Wanasiasa walafi wameharibu nchi na kuifanya kama “shamba la bibi.” Vijana wamegeuzwa mtaji wa kisiasa kwa wanasiasa vigogo kuwatumia kwa kigezo cha mwenge wa uhuru kueneza propaganda na mwisho wake sehemu ya vijana wanaoshiriki kwenye kukimbiza mwenge hupewa nafasi za utendaji kama fadhila ya utumishi wao kwenye kueneza chuki ya maangamizo ya uharibifu wa shakhsiya ya vijana wengi kwa vile hakuna matumaini ya vijana wasiokuwa na kazi mahsusi kwenye maisha yao ya leo na kesho.

    Hakuna njia nyepesi kwa vijana na kizazi cha Tanzania isipokuwa kukubali mapinduzi ya fikra. Kwa elimu yenye manufaa ndipo vijana na kizazi cha Tanzania kinaweza kujikomboa na uzezeta wa kutumiwa kama daraja na wanasiasa walafi na wenye uchu wa kutawala kifisadi.


    HEKO TANZANIA!

    Makala na Maligwa; Simu ya kiganjani: +255 713 593347 Barua pepe: maligwa1968@yahoo.com



    Comments