UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI (UJASILIAMALI WA KILIMO)



UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI WENYE TIJA
Image result for KUKU WA KIENYEJI


Safari yangu ilianza baada ya kukutana na mhamasishaji aliyenitia chachu kwamba 10 x10 x 10 you become a millionea! Kwamba ukianza na kuku 10 kila mmoja akazaa 10 na hao watoto na mama zao wakazaa kila mmoja 10 unakuwa millionea! Wakubwa kuongea ni rahisi utekelezaji ukawa mgumu sana! Changamoto kuu aipatayo mfugaji wa kuku wa kienyeji ni kuzalisha vifaranga wengi na kuweza kuwakuza! Bila hivyo kundi haliwezi kukua na kukupa kipato cha uhakika!

 

Safari ya ufugaji niliianza kwa kununua mitetea 30 na jogoo watatu! Ilibidi nisubiri muda hadi kuku waanze kutaga! Muda ukafika kuku wakaanza kutaga kwa fujo sana! Nilikuwa na banda moja tu ambamo kuku wote walikuwa wakilala humo. Nilitengeneza viota vingi kwa ajili ya kuku kutagia. Asubuhi nilikuwa nawafungulia! Changamoto nilizoanza kupambana nazo kwanza kama mjuavyo kuku tofauti walikuwa wanataga kwenye kiota kimoja! Ilipofika wakati wa kuatamia ikawa kila kwenye kiota kimoja kuna kuku kadhaa wamebanana wanaatamia! Hali hii haipaswi kutokea kwani kuku mmoja anaweza kuwa amejilundikia mayai mengi ambayo hawezi kuyapajoto la kutosha na kuku mwingine anakuwa amekaa kando tu hana hata yai moja. Hii ilibadilika ikawa kero kubwa! Nilijua utotoaji unaweza kuathirika sana!

 

Ili utotoreshe vifaranga vingi kwa wakati mmoja badala ya kutumia incubator, tumia hao hao kuku. Wakianza kutaga kila siku okota mayai na kuyahifadhi mahali salama ili kuku wasiyatie joto! Kuku wengi wanapotaga kwa pamoja hufikia wakati mayai huishatumboni unakuta wamelala kwenye viota wakiwa wameatamia mayai yaliyopo au udongo tu! Kuku anaekuwa amefikia kuatamia utamjua kwani ukimshitua haondoki kwenye kiota. Kuku anaetaga ukimshitua hukimbia! Kwa hiyo kama nimepanga kutotolesha vifaranga 100 kwa mara moja nikishagundua kuwa kuna kuku 8 wameanza kuonesha dalili ya kuatamia hapo husubiri usiku ninawawekea mayai amabayo nilikuwa nimeyahifadhi. Ambapo mimi huwekea kila kuku mayai 15. Kwa hiyo kuku 8 hufanya jumla ya mayai 120. 

 

Kwa kuwa banda langu ni hilo moja tu kuku wengine wanaoendelea kutaga walikuwa wanaendelea kutagia kwenye viota ambavyo kuku wengine walikuwa wanaatamia! Hali hii ilikuwa inaleta tabu sana kwani ilikuwa si rahisi kutambua mayai mapya na yenye siku nyingi. Kuondoa shida hii nilinunua MARKER PEN (rangi yoyote) na siku ya kuwawekea mayai kuku ili waatamie niliyachora mduara kuzunguka yai ili iwe rahisi kuyatambua mayai mapya. Huo mchoro hauwatishi kuku na hakuna dosari yoyote. Kwa hiyo kila siku jioni ninapokuja kuokota mayai yaliyotagwa nilikuwa pia nakagua kila kiota cha kuku walioatamia na kuondoa mayai mapya. Kumnyenyua kuku anaeatamia na kuondoa yai haileti shida yoyote!

Kuku akifikia wakati wa kuatamia ukamnyima mayai hawa wanatabia kuendelea kung'ang'ania kuatamia, hapo ilibidi kutengeneza JELA! Watu wengine wanambinu tofauti kumwachisha kuku asiatamie! Mbinu ya kumtia kuku stress inafanya kazi nzuri sana! Jela inaweza kuwa ni Tega, au Box kubwa au chumba kidogo kilichopo. Ukimfungia kuku JELA bila maji wala chakula kwa kutwa mbili siku ukimfungulia akili yake huwa ni kutafuta chakula tu hakumbuki kurudi kwenye kiota! Njia hii ilifanikiwa sana na ilifanya kuendesha shughuri zangu bila bughudha! Kuna wakati JELA ilikuwa na kuku kibao hivyo unapaswa kutengeneza kibanda cha JELA. Hawa kuku wakitoka JELA hutaga mapema sana amabapo bila hivyo wangekuwa wanaatamia. 

 

Pia kuku wakishaatamia kwa muda wa siku 10 nilikuwa nayapima mayai ili kubaini kama kuna mayai yasiyoweza kuanguliwa! Ni rahisi sana kama una Tochi! Ukimulika yai Kwa kulizungushia vidole kiganjani kama ni yai zima linakuwa na giza kama ni yai bovu linapitisha mwanga kama yai lililotagwa siku hiyo! Jinsi ya kuzungushia vidole yai, tengeneza duara kwa vidole vyako na dole gumba kisha pachika yai katikati ya duara ili mwanga wa tochi upenye kwenye yai! Kwahiyo unaweka tochi inayowaka chini ya yai na hii ifanyike gizani au ndani ya chumba chenye mwaga mdogo. Kadri ya yai linavyokaribia kutotolewa ukilimulika huwa na giza zaidi! Ukimulika mayai toa mayai yasiyoweza kutotolewa maana hayo hutumia joto la Mama bure!

 

Bado ntaendelea kuwaletea makala hii kuhusu ufugaji kuku bado sijamaliza nimeona niwarushie hii kwanza kwa kuanzia. Mwenzenu nilikuwa nahangaika kufukia tanuru la mkaa nimekuta limefunguka! Si mnajua maisha jamani! Vijana tuamke na kujiingiza katika miradi hii soon tutaona mabadiliko.



KANUNI SAHIHI ZA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI

KANUNI SAHIHI ZA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI


KANUNI SAHIHI ZA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI
KANUNI SAHIHI ZA UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI:Kaya nyingi hapa nchini hujihusisha na ufugaji wa kuku kwa lengo la kujipatia chakula na kipato. Mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku ni pamoja na mayai, nyama, mbolea na manyoya kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
Mifumo ya ufugaji kuku ambayo hutumika hapa nchini ni huria, nusu huria na shadidi. Ufugaji wa kuku utakuwa endelevu na wenye tija kwa kufuata kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-
·         Kufuga kuku kwenye banda bora
·         Kuchagua kuku bora wa kufuga
·         Kutunza na kulisha kuku kulingana na hatua mbalimbali za ukuaji
·         Kudhibiti na kutibu magonjwa ya kuku
·         Kutunza kumbukumbu
Kuku huhitaji banda bora ili wasiathirike na madhara mbalimbali. Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo:-
·         Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama hatari,
·         Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika kwa urahisi,
·         Lijengwe sehemu yenye mwinuko isiyotuama maji, isiyo na upepo mkali na iwe mbali kidogo na nyumba ya kuishi watu.
·         Liwe na vichanja kwa ajili ya kuku kupumzika na kulala
·         Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji, kutagia, kuatamia na sehemu ya kulelea vifaranga
·         Liwe na nafasi ya kutosha kulingana na idadi ya kuku na kuweka vyombo vya chakula na maji
·         Kwenye mazingira ya joto banda liwe la ukuta mfupi na sehemu kubwa wazi yenye wavu hadi kufikia kwenye paa
·         Kwenye mazingira ya baridi banda liwe na ukuta mrefu unaokaribia paa na sehemu ndogo tu iwe wazi yenye wavu ili kupitisha hewa na mwanga
VIFAA VINAVYOTUMIKA KWA UJENZI WA BANDA
Vifaa vya kujengea banda vizingatie gharama na upatikanaji wake katika eneo husika. Baadhi ya vifaa hivyo ni kama ifuatavyo:-
·         Sakafu Saruji, udongo, mbao, mianzi au fito
·         Kuta Fito, mabanzi, mbao, nguzo mianzi,udongo, matofali, mawe, mabati na wavu
·         Paa Nyasi, makuti, majani ya migomba, mabati na vigae.
·         Wigo Matofali, mbao, fito nguzo, mabanzi, mianzi, matete, wavu na mabati
Ukubwa wa banda utategemea idadi ya kuku na aina ya kundi la kuku. Kuku wanahitaji nafasi tofauti kutegemea umri, aina, na njia ya ufugaji. Eneo la mita moja ya mraba linatosha kwa vifaranga 16 wa umri wa wiki 1 – 4. Hivyo banda lenye mita za mraba 16 linaweza kulea vifaranga 320 hadi wiki 4. Baada ya wiki 4 eneo hili liongezwe kutegemea aina ya kuku na njia inayotumika katika ufugaji kama inavyoonekana kwenye Jedwali Na. 1
 JEDWALI NA 1: ENEO LINALOHITAJIKA KUFUGA KUKU KWENYE SAKAFU YA MATANDAZO KUTEGEMEA NA UMRI NA AINA YA KUKU

UMRI WA KUKU
IDADI YA KUKU KWA MITA 1 YA MRABA
KUKU WA MAYAI
KUKU WA NYAMA
Siku 1 hadi wiki 4
18
18
Wiki ya 5 hadi ya 8
9
9
Wiki ya 9 hadi 20
6
Wiki 21 na kuendelea
3 – 4

ANGALIZO:
Mabanda yanayozungushiwa wigo kama ilivyo katika mfumo wa nusu huria, kuku mmoja huhitaji eneo la wazi lenye ukubwa wa mita za mraba 10. Mfano, kuku 100 huhitaji eneo la mita za mraba 1000
 VIFAA NA VYOMBO MUHIMU
Mfugaji anashauriwa kutumia vifaa na vyombo maalum ili kurahisisha na kuboresha utunzaji wa makundi mbalimbali ya kuku. Vifaa na vyombo vinavyohitajika kwa ajili ya kuwekea chakula na maji, kutagia mayai na kupumzikia vinapatikana kwenye maduka ya pembejeo za mifugo. Aidha, mfugaji anaweza kutengeneza mwenyewe kwa kutumia malighafi zilizopo kwenye mazingira yake.
 KUCHAGUA KUKU BORA WA KUFUGA
KUKU WA ASILI
 Aina za kuku wa asili wanaopatikana hapa nchini ni pamoja na Kuchi (Kuza), Poni (Kishingo), Njachama, Kinyavu, Mbuni na Tongwe (Msumbiji). Mfugaji anaweza kuongeza uzalishaji kwa kuchagua kuku mwenye sifa zifuatazo:-
·         Uwezo wa kutaga mayai mengi (kati ya 15-20) katika mzunguko mmoja wa utagaji (Jedwali Na 2),
·         Uwezo wa kuatamia na kuangua vifaranga wengi,
·         Uwezo wa kustahimili magonjwa,
·         Anayetoka maeneo yasiyo na magonjwa; na
·         Umbo kubwa na kukua haraka.
 KUKU WA KISASA
Kuku bora wa kisasa kwa ajili ya mayai au nyama ni mwenye sifa zifuatazo:-
·         Uwezo wa kuanza kutaga wakiwa na umri mdogo (miezi 5 – 6) kutegemea na koo,
·         Umbo kubwa na anayekua haraka (kilo 1.5-2.0 kwa kipindi cha wiki 8-12) kutegemea na koo kwa kuku wa nyama,
·         Anayetaga mayai mengi (250 au zaidi) kwa kuku wa mayai kwa mwaka; na
·         Awe na uwezo wa kutaga katika umri wa miezi 6 – 8.
 KUCHAGUA JOGOO BORA WA MBEGU
Jogoo wa mbegu anatakiwa awe na sifa zifuatazo:
·         Achaguliwe kutoka kwenye koo zenye sifa ya kutaga mayai mengi,
·         Mrefu, umbo kubwa, miguu imara na yenye nguvu,
·         Awe machachari, ushawishi kwa mitetea na ari ya kupanda; na
·         Uwezo wa kupanda akiwa na umri wa miezi 7 – 10.
 MAYAI KWA AJILI YA KUTOTOA VIFARANGA
UCHAGUZI WA MAYAI
Mayai kwa ajili ya kutotoa vifaranga yawe na sifa zifuatazo:-
·         Yaliyorutubishwa na jogoo,
·         Yasiwe na nyufa,
·         Yasiwe na maganda tepetepe,
·         Yasiwe na kiini kilichovunjika,
·         Yawe na ukubwa wa wastani; na
·         Yasiwe yamekaa zaidi ya wiki 2 baada ya kutagwa.
 UTUNZAJI WA MAYAI
Mayai ya kienyeji kwa ajili ya kutotoa vifaranga yatunzwe kwa kusimamishwa wima sehemu iliyochongoka ikiwa imeangalia chini kwa siku 3 za mwanzo na kisha yageuzwe ili sehemu iliyo butu iangalie chini. Mayai yahifadhiwe kwenye sehemu iliyo na ubaridi kidogo na giza.
UTUNZAJI WA KUKU KWA MAKUNDI
UTUNZAJI WA VIFARANGA
Malezi bora ya vifaranga ni muhimu katika ufugaji wa kuku kwa sababu vifaranga hawana uwezo wa kustahimili mazingira wakiwa wenyewe mara wanapoanguliwa. Ukosefu wa malezi bora husababisha vifaranga kuwa dhaifu, kufa kwa wingi na hivyo kupunguza idadi ya kuku wa baadaye. Malezi ya vifaranga yanaweza kufanyika kwa kutumia kuku walezi au kutumia vifaa maalum.
KULEA VIFARANGA KWA KUTUMIA KUKU MLEZI
Vifaranga wanaweza kulelewa na mama yao au kuku mlezi. Endapo kuku wengi wametotoa vifaranga kwa wakati mmoja, achaguliwe kuku mlezi aliye na uwezo wa kulea vifaranga wengi kati ya waliototoa aendelee kulea na wengine waliototoa waachwe huru ili warudi kwenye mzunguko wa kutaga. Kuku mmoja anaweza kulea vifaranga 20 hadi 25. Mfugaji wa kuku, pamoja na kanuni nyingine, anapaswa kuzingatia yafuatayo:-
·         Kuku anayelea vifaranga atengewe chumba maalum, apewe maji ya kutosha na chakula chenye virutubishi muhimu,
·         Vifaranga wasiachiwe kutoka nje hadi watakapofika umri wa wiki 6,
·         Vifaranga watengwe na mama/mlezi baada ya wiki 4 kuruhusu mama aendelee na mzunguko wa kutaga; na
·         Katika maeneo yenye hali ya hewa ya ubaridi vifaranga wacheleweshwe kutenganishwa na mama/malezi hadi wiki ya 6 au mpaka waonekane wameota manyoya ya kutosha.
KULEA VIFARANGA KWA KUTUMIA BRUDA
Bruda ni chombo/sehemu iliyoandaliwa mahususi kwa ajili ya kuwapatia joto vifaranga badala ya mama/mlezi. Mfugaji anaweza kulea vifaranga wengi kwa kutumia bruda ambayo ni mduara unaoweza kutengenezwa kwa kutumia mbao, karatasi ngumu au kwa kuziba pembe za chumba. Aidha, njia hii hupunguza vifo vya vifaranga vinavyosababishwa na ndege au wanyama hatari, huruhusu kuku kutaga mapema zaidi na kuwa na mizunguko mingi ya utagaji (kwa kuku wanaoatamia). Vilevile, hurahisisha udhibiti wa magonjwa.
Mfugaji anapaswa kufuata taratibu zifuatazo katika kulea vifaranga kwa kutumia bruda:-
·         Kuweka vifaa vya kuongeza joto kwa mfano taa ya umeme, chemli au jiko la mkaa. Zingatia kiwango cha joto katika bruda kinachohitajika. Wiki ya kwanza ni 35 oC, wiki ya pili ni 33 oC, wiki ya tatu ni 31 oC na wiki ya nne ni 29 oC,
·         Kuchunguza mtawanyiko wa vifaranga ndani ya bruda ili kutathimini hali ya joto. Wakijikusanya kwenye chanzo cha joto, inaashiria kuwa baridi imezidi hivyo joto liongezwe. Wakiwa mbali na chanzo cha joto maana yake joto limezidi hivyo joto lipunguzwe,
·         Bruda iwe na sakafu yenye malalo yatokanayo na maranda ya mbao au pumba za mpunga. Malalo yabadilishwe endapo yataonekana yameloana,
·         Bruda iwekwe vifaa vya maji na chakula. Maji na chakula kiwekwe kabla ya kuweka vifaranga,
·         Vifaa vya joto viwekwe ndani ya bruda masaa 6 kabla ya kuingia vifaranga,
·         Vifaranga walishwe chakula cha kuanzia gramu 12 – 15 kwa kipindi cha wiki ya kwanza na gram 15 – 21 kwa kipindi cha wiki ya 2. Katika wiki ya 3 wapewe gramu 21 – 35 kwa kifaranga na chakula hicho kiwepo muda wote,
·         Vifaranga wapatiwe vitamini, madini na dawa za kinga (antibiotics); na
·         Vifaranga wapatiwe chanjo kulingana na maelekezo ya mtaalamu wa mifugo. Chanjo dhidi ya magonjwa muhimu kwa mfano, Marek’s (mara anapototolewa), Mdondo (siku ya 3 – 4 na kurudiwa baada ya siku ya 21 na kila baada ya miezi 3) na Gumboro (siku ya 7 na kurudia tena siku ya 21). Wapatiwe dawa ya minyoo (wiki ya 8) na Coccidiosis (wiki ya 3 – 4)
KUTUNZA KUKU WANAOKUA (WIKI 8 – 18)
Utunzaji wa kundi hili unategemea mfumo unaotumika.
KUKU WANAOFUGWA KATIKA MFUMO HURIA
Kuku wanaofugwa katika mfumo huu wapatiwe matunzo bora yakiwemo yafuatayo;
·         Wapewe chakula cha ziada asubuhi kabla ya kutoka na wanaporudi kwenye banda. Chakula hicho kinaweza kugawanywa mara 2 kwa siku,
·         Wapatiwe maji safi na ya kutosha wakati wote; na
·         Wapatiwe chanjo na dawa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
KUKU WANAOFUGWA KATIKA MFUMO SHADIDI
·         Majogoo watenganishwe na mitetea katika wiki 7 hadi 10 ili kuzuia uzaliano usio na mpangilio,
·         Wapewe chakula cha kukuzia kuanzia wiki ya 8 – 15 gramu 55 – 60 na kuanzia wiki ya 16 gramu 65 – 80 kwa wanaofugwa mfumo huria na gram 120- 125 kwa kuku kwa siku kwa wanaofugwa mfumo wa shadidi,
·         Kuku wa nyama wapatiwe chakula cha kuku wa nyama muda wote,
·         Wapatiwe maji safi ya kunywa kwa muda wote kwenye vyombo visafi,
·         Kuku wachunguzwe dalili zozote za ugonjwa ili waweze kupata tiba sahihi kutoka kwa mtaalamu wa mifugo,
·         Kuku wa wiki 9 – 20 wanahitaji nafasi ya mita za mraba 0.15 kwa kuku na wiki 21 au zaidi mita za mraba 0.2 kwa kuku,
·         Kuwe na vyombo maalum vya kutosha kwa ajili ya chakula na maji
·         Wafanyiwe usafi wa banda mara kwa mara ili kuzuia magonjwa yanayotokana na uchafu; na
·         Wakatwe midomo ili kuzuia kudonoana.
KUKU WANAOTAGA
Mahitaji ya kuku wanaotaga ni tofauti na ya makundi mengine. Mambo ya kuzingatia kwa kuku wanaotaga ni pamoja na:-
·         Banda liwe na viota vya kutagia mayai (kiota 1 kwa kuku 3 – 5). Viota viwekwe bandani mara kuku watakapofikisha umri wa wiki 18 ili waanze kuzoea kuvitumia,
·         Wapatiwe chakula na maji safi wakati wote kwa kutumia vyombo maalum ambavyo ni visafi,
·         Kuku wasiotaga waondolewe kwenye kundi. Kuku hao huonekana wasafi na sehemu ya kutolea yai huwa ndogo na kavu, upanga wake kichwani (comb) huwa mdogo na mwekundu,
·         Wapewe dawa ya minyoo kila baada ya miezi 3,
·         Wawekewe fito au ubao mwembamba kama sehemu ya kupumzikia na mazoezi ili kuzuia kudonoana,
·         Mayai yakusanywe mara 4 au zaidi kwa siku ili yasidonolewe na kuku,
·         Kuwe na malalo makavu na yabadilishwe mara yanapochafuka,
·         Vyombo vifanyiwe usafi kila siku ili kuzuia magonjwa; na
·         Watundikiwe majani mabichi aina ya mchicha, papai, alfaalfa, majani jamii ya mikunde ili kuboresha lishe.
 UDHIBITI NA TIBA DHIDI YA MAGONJWA YA KUKU
Kuku wanaopata lishe bora, kutunzwa vizuri na kupatiwa chanjo dhidi ya magonjwa yanayotokea mara kwa mara huwa na afya nzuri. Ni bora kuzuia magonjwa kuliko kutibu ili kupunguza vifo na gharama. Iwapo ugonjwa utatokea kuku wagonjwa watenganishwe na kuku wasio wagonjwa na wapatiwe tiba. Kanuni muhimu za kufuata ili kuzuia magonjwa ni:-
·         Banda liwe safi muda wote,
·         Kabla ya kuweka kuku, banda linyunyiziwe dawa ya kuua wadudu wa magonjwa mbalimbali,
·         Kuku wakaguliwe kila siku ili kubaini wagonjwa au wenye matatizo, kuwatenga na kutoa taarifa kwa mtaalam wa mifugo,
·         Kuku wapatiwe chanjo dhidi ya magonjwa mbalimbali,
·         Watu wasiohusika wasiingie eneo la kufugia kuku bila utaratibu,
·         Ndege na wanyama wengine wasifike eneo la kufugia kuku,
·         Banda la kufugia kuku litenganishwe na mabanda ya mifugo mingine,
·         Lango la kuingilia katika banda la kuku liwekewe dawa ya kukanyaga kwa wanaoingia ndani ili kuzuia kuingiza vimelea vya wadudu wa magonjwa; na
·         Vifaa vya chakula na maji viwe safi wakati wote.
 DALILI ZA KUKU MGONJWA
Dalili za ujumla zinazoonekana kwa kuku mgonjwa ni kama zifuatazo:-
·         Kuzubaa,
·         Kupoteza hamu ya kula,
·         Kujitenga na wenzake katika kundi; na
·         Kupunguza au kusimama kutaga.
 Mfugaji anapoona mojawapo ya dalili hizo amwone mtaalam wa mifugo
 UFUGAJI WA AINA NYINGINE ZA NDEGE
Aina ya ndege wengine wanaofugwa hapa nchini ni pamoja na Bata maji, Bata bukini, Bata mzinga, Kanga na Njiwa. Ndege hao hufugwa kwa kiasi kidogo ukilinganisha na kuku kwa kuwa soko lao ni dogo. Utunzaji wao hautofautiani sana na kuku;
·         Wajengewe banda la kuishi ambalo ukubwa wake utategemea idadi ya ndege wanaofugwa,
·         Wapatiwe chakula chenye virutubisho na maji ya kunywa ya kutosha,
·         Wapatiwe kinga na tiba dhidi ya magonjwa,
·         Bata maji na Bata bukini wajengewe bwawa lenye nafasi ya kutosha kwa ajili ya kuogelea; na
·         Njiwa wajengewe viota sehemu ya juu kama kwenye mapaa ya nyumba.
 UTUNZAJI WA KUMBUKUMBU
Utunzaji wa kumbukumbu ni muhimu sana katika ufugaji wa kuku na ndege wengine wafugwao ili kusaidia mfugaji kujua maendeleo ya ufugaji wake. Utaratibu wa kuweka kumbukumbu mara tukio linapotokea ni lazima ili kuepuka kusahau. Mfugaji ahakikishe anaweka kumbukumbu ambazo ni sahihi na zinazoeleweka.
 AINA ZA KUMBUKUMBU
Kumbukumbu zinazopaswa kuwekwa ni pamoja na:-
·         Aina na idadi ya kuku waliopo kwenye kila kundi (mfano vifaranga, wanaokua, wanaotaga, majogoo),
·         Uzalishaji wa mayai kwa kundi la kuku waliopo,
·         Utotoaji wa vifaranga,
·         Kinga na matibabu,
·         Mapato na matumizi,
·         Utagaji wa kila kuku na utunzaji (kwa kuku wa asili); na
·         Kumbukumbu za vifo.

Share this:
















Comments