Siri za mahaba ya Mugabe na Tanzania

By Noor Shija,
Mwananchi
Kama
kuna Mtanzania ambaye alikuwa hafahamu namna Rais mstaafu wa Zimbabwe, Robert
Mugabe alivyokuwa akiipenda Tanzania, afuatilie simulizi fupi ya Rais mstaafu
wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.
Mbali
na hiyo mwaka 2014, Mugabe alielezea kusikitishwa kwake na namna viongozi wa
Afrika walivyoshindwa kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere kutokana na mchango wake
wa kuzikomboa nchi za Afrika.
“Ninataka
kusema, mashujaa wengi wa Afrika wamepewa heshima, lakini mtu aliyefedheheshwa
ni Mwalimu Julius Nyerere. Tulikuwa pale, tulifanya harakati za ukombozi pale
na tulitegemea rasilimali za Tanzania, lakini hakuna kinachozungumzwa kuhusu
huyu mtu na nchi yake katika Umoja wa Afrika,” alisema Mugabe katika moja ya
mikutano na viongozi wa Afrika.
Mwaka
2015 jijini Harare nchini Zimbabwe, Mugabe alizindua kitabu kilichoitwa ‘Julius
Nyerere, Asante Sana, Thank you Mwalimu.’ Ni kitabu kilichochapishwa na kituo
cha utafiti na vielelezo cha kusini mwa Afrika (SARDC) chenye masimulizi mengi
kuhusu Nyerere na Tanzania.
Katika
kuunga mkono hayo, Rais mstaafu Mwinyi ametoa simulizi kuhusu uungwana wa
Mugabe wa kufikia hatua ya kugawana umaskini wake na Tanzania, baada ya kupokea
taarifa za kifo cha kiongozi huyo
kilichotokea
Ijumaa iliyopita nchini Singapore alipokuwa akipatiwa matibabu.
“Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Rafiki yetu
sisi wa kwanza kabisa ni ndugu Mugabe,” ni kauli ya Mwinyi akielezea namna
Mugabe alivyoisaidia fedha Tanzania.
Mwinyi
anasema alipochukua uongozi wa nchi mwaka 1985 kutoka kwa Mwalimu Nyerere
aliikuta Hazina ya Taifa ikiwa haina kitu.
“Nilikwenda
kwa Mwalimu Nyerere kumpa hali hiyo, na akanishauri kwamba tuna marafiki
duniani, akiwamo komredi Mugabe, Rajiv Gandhi na wengine wengi, ‘hebu jaribu
kuzungumza nao hawa’” anasema Mwinyi kwenye video aliyorekodiwa akizungumzia
umuhimu wa Mugabe Tanzania.
Rajiv
Gandhi alikuwa waziri mkuu wa sita wa India, kuanzia mwaka 1984 hadi alipouawa
mwaka 1989. Alichukua nafasi hiyo baada ya waziri mkuu wa wakati (ambaye ni
mama yake), Indira Gandhi kuuawa kwa kupigwa risasi na mmoja wa walinzi wake
mwaka 1984.
Mwinyi
anasema Hazina ilikauka kutokana na fedha nyingi kutumika kununulia silaha kwa
ajili ya kuikomboa nchi wakati wa vita vya Kagera mwaka 1978-1979.
Anasema,
pia hali hiyo ilitokana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kumsusia Mwalimu
Nyerere kumkopesha fedha kwa kuwa alikataa masharti yao. “Lakini, akaja
akatusaidia ndugu Mugabe tukaanza maisha.”
“Nakumbuka
nilituma watu wawili mmoja wapo (Benjamin) Mkapa na ndugu Salim (Dk Salim Ahmed
Salim), ama nimesahau lakini mmoja wapo kati ya hao alikwenda kwa Rajiv na
mwingine kwa Mugabe kumuomba msaada.
Mapenzi
ya Mugabe kwa Tanzania yalijidhihirisha alipokuwa akizindua kitabu ambacho
kimekusanya hotuba mbalimbali za Mwalimu Nyerere na hasa kuhusu ukombozi wa
nchi za Afrika.
Kitabu
hicho kilizinduliwa ikulu mjini Harare nchini Zimbabwe wakati huo Mugabe
alikuwa bado yuko madarakani, alisema Mwalimu ni nembo adhimu ya uhuru na umoja
na kwamba kitabu hicho kimejumuisha maeneo mengi ikiwamo juhudi za Afrika
katika kupigania uhuru wa kisiasa.
Mugabe
alisema Mwalimu amefanya mengi katika kubeba mzigo wa nchi za Afrika wakati wa
kutafuta uhuru. “Alijitoa na kuhangaika sana. Alikuwa mtu wa kweli ambaye
hakuna wa kulingana naye,” alisema Mugabe.
“Nimefurahi
sana kusikia kuwa jengo linalojengwa katika Umoja wa Afrika litakalotumiwa na
baraza la usalama kupewa jina la Mwalimu Julius Nyerere,” alisema Mugabe ambaye
ndiye alipendekeza jina hilo alipokuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.
Mugabe
aliongeza kuwa Mwalimu pia alikuwa kiunganishi cha nchi za Afrika kwa China.
Taifa hilo lilikuwa msaada mkubwa kwa nchi za Afrika.
“Nchi
za magharibi zitajisingizia, zitadai, zitaadhibu lakini angalia mashariki
(Mashariki ya mbali), una rafiki ambaye wakati wote anajihisi kama wewe, rafiki
anashirikiana na wewe katika juhudi zako. Tunafuata nyayo za Mwalimu kuelekea
mashariki. Leo uhusiano wetu na China umeimarika. Kitabu kinamwelezea
mwanasiasa mkubwa mwenye weledi, mpiganaji na mzalendo wa kweli,” alisema
Mugabe.
Mugabe
alimwelezea Mwalimu Nyerere kwamba ni mtu aliyechangia harakati za ukombozi kwa
nchi za mashariki ya kati ya Afrika, mwasisi wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika.
Imani ya Mwalimu ilikuwa uhuru utapatikana ikiwa watu watashirikiana.
Alisema
kulikuwa na mkutano uliofanyika Geneva nchini Uswisi lakini kabla ya kwenda
huko, Mwalimu Nyerere aliwakutanisha baadhi ya viongozi wa Afrika jijini Dar es
Salaam kwa ajili ya kuweka msimamo wa pamoja na matokeo ya mkutano huo ni
kuanzishwa kundi la nchi za mstari wa mbele 1976.
“Tuliamua
kwamba hakuna haja ya kuwavunja moyo wale waliotusaidia. Pia, Mwalimu alikuwa
na sifa nyingine ya kuunganisha watu wake. Aliunganisha Tanganyika na
Zanzibar,” alisema Mugabe na kuongeza kuwa Mwalimu alikuwa mtu asiyetetereka,
kiongozi mwenye maono aliyesimama na wote katika mapambano ya ukombozi wa
kusini mwa Afrika.
Mugabe
anasema wakati wa kuanzishwa OAU, Mwalimu alifurahishwa na hatua hiyo ya
kuanzishwa jumuiya hiyo na alitoa fursa ya Dar es Salaam kuwa mwenyeji wa
mkutano wa kamati ya ukombozi ya OAU.
“Dar
es Salaam ikiwa ni kituo ambako tulienda kwa ajili ya mafunzo, miongozo na
mambo mengine,” alisema Mugabe.
Alisema
ni Mwalimu ndiye aliwezesha yeye (Mugabe) kuwa na uhusiano na Mwenyekiti Mao
Zedong wa China na kukajengwa reli kati ya Tanzania na Zambia (Tazara). “Leo,
ushirikiano wa China na Afrika umekolezwa na FOCAC (Jukwaa la ushirikiano wa
China na Afrika) na hii imetokana na Mwalimu aliyeasisi uhusiano na China.”
Mugabe
alimwelezea Mwalimu kama ni mtu aliyejitoa katika ukombozi, umoja na maendeleo
ya Afrika akisisitiza kwamba uongozi wake ni kioo cha jamii, mzalendo na
anayestahiki heshima kubwa.
Akisisitiza
umuhimu wa Mwalimu hilo Mugabe alirudia kwenye mkutano wa 35 wa viongozi wa
nchi na serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC),
uliofanyika Gaborone,Botswana.
Alizitaka
nchi za Afrika kuwaenzi wale waliojitoa kupigania ukombozi wa bara la Afrika.
“Tuwakumbuke wale waliotuachia urithi huu. Hii inaweza kuwa ni kitu, je,
tunaweza kuwa na fedha za kulipa fadhila zao,” alihoji Mugabe.
Mugabe
aliwataka viongozi wenzake kuwa na utaratibu mahsusi wa kuenzi urithi wa
waasisi kama vile Rais wa zamani wa Tanzania, Julius Nyerere, Rais wa zamani wa
Zambia, Kenneth Kaunda na Rais wa zamani wa Botswana, Seretse Khama (ambaye kwa
sasa ni marehemu), wametoa mchango mkubwa wa kuongoza ukombozi kwa Afrika
“Ninataka
sisi Wazimbabwe tusimame kwa ajili ya Nyerere. Afrika lazima ikumbushwe wajibu
wa kumuenzi Nyerere, alibeba mzigo wa mafunzo kwa wapigania uhuru.
“Mwisho
wa siku hakuna hata mmoja anayezungumzia Tanzania kwamba inastahiki kutajwa.
Hata kutaja kidogo kwa kukamilisha kazi, kazi ya kutufanya tuwe marafiki, kazi
ya kutoa mafunzo kwa wapigania ukombozi wa Afrika. Wote tulikwenda kwa njia
mbalimbali, maeneo tofauti nchini Tanzania kwa ajili ya kuzikomboa nchi zetu na
hatujarudi Tanzania,” alisema Mugabe.
Comments
Post a Comment