UMUHIMU WA KISWAHILI KATIKA NYANJA ZA
KITAALUMA
Na Jennifer Walter
Lugha ya Kiswahili ni lugha ambayo imevuka mipaka ya ukabila na
utaifa. Ni lugha ambayo inakua na kuenea kwa kasi. Kukua kwa lugha hupimwa
kutokana na mawanda mapana ya utumizi pamoja na kuongezeka kwa idadi kubwa ya
watumiaji.
Mwenye masikio na asikie, mkataa kwao mchawi. Kuna baadhi ya
wasomi hudharau lugha ya Kiswahili kwa kuiona ni lugha ya hadhi ya chini.
Tunatakiwa kuelewa kuwa hakuna lugha yoyote dunani ambayo ni bora kuliko lugha
nyingine. Lugha yoyote ni bora kwa kuwa inakidhi haja ya mawasiliano miongoni
mwa watumiaji.
Pengine lugha hii ya Kiswahili inadharauliwa kutokana na
kutojulikana asili yake ni wapi. Bado kuna mjadala mkubwa na endelevu kuhusu
asili ya lugha ya Kiswahili. Wataalamu hao huibuka kwa hoja mbalimbali na
kutetea madai yao. Wapo wanaodai kuwa Kiswahili asili yake inatokana na lugha
ya Kiarabu, ya Kibantu, mchanganyiko wa lugha ya Kiarabu na Kibantu, Kibantu
kilichochanganyika na Kiarabu na mchanganyiko wa lugha mbalimbali za
Kibantu kutoka upwa wa Afrika Mashariki.
Jambo la ajabu zaidi ni kuwa hata Mswahili mwenyewe bado
hajulikani ni yupi! Wako baadhi ya watu ambao hawependi kuitwa Waswahili
kwa kuwa maana ya Mswahili inaandamana na sifa mbaya mathalani mtu laghai,
mwenye hadhi ya chini kiuchumi, asiyejali muda, kutumia maneno mengi kujieleza
au kujitetea n kadhalika.
Tunawezaje kuwaachia wageni kupata fursa zitokanazo na lugha ya
Kiswahili ilhali wenyewe tumerudi nyuma? Wageni wajapo kwetu kujifunza
Kiswahili na hupenda kukitumia ili kuwasiliana na wenyeji, lakini sisi kwa
kujidai tunajua tunazungumza nao kwa kutumia lugha zao. Mgeni huyu akibobea katika
Kiswahili tutaweza kushindana naye katika soko la ajira?
Wanaodhani wanaelewa Kiswahili ndio wa kwanza kukosea na
kukiharibu. Wageni wanajua Kiswahili pengine kuwashinda wazawa kwa kuwa wao
hufuata kanuni sahihi za kisarufi wakkati wenyeji kuongea Kiswahili cha mazoea
chenye makosa mengi. Baadhi ya makosa ni kama vile ‘ilikusudi’. Kwa
mfano, “Nimekuja ili kusudi niwasaidie”. Ili na kusudi ni maneno yenye hadhi
sawa yanayoelezea sababu, hivyo hayatakiwi kutumika pamoja. Mfano mwingine ni “Mimi
binafsi”. Mfano huu wa “mimi binafsi nitachangia laki mbili”. Mimi ni
kiwakilishi cha binafsi hivyo unatakiwa kuteua neno moja litumike badala ya
maneno mawili.
Tunatakiwa tuelewe kwamba vyuo vikuu vingi duniani vinafundisha
lugha ya Kiswahili; mathalan Chuo Kikuu cha Egerton, Kenyatta, nk huko Kenya,
Cambridge, Edinburgh huko Uingereza, Columbia, Philadelphia, nk huko
Marekani na vingine vingi.
Profesa Sun Baohua wa Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing
(CRI) anaeleza kuwa “Somo la Kiswahili hufuata utaratibu wa kufundisha kwa
miaka minne. Miaka miwili ya kwanza tunaiita kipindi cha kuwawekea msingi
wanafunzi ambapo tunafungua somo rasmi la Kiswahili, somo la kuzungumza,
kusikiliza na somo la ziada. Miaka miwili ya pili tunaiita kipindi cha kuinua
uwezo wa lugha. Wanafunzi wanatakiwa kufundishwa somo la uandishi wa
habari, ukalimani, tafsiri, fasihi ya Kiswahili na somo la taarifa za
habari kutoka nchi ya Afrika Mashariki”.
Walimu wa kufundisha lugha ya Kiswahili katika vyuo hivyo wapo
wachache. Wataalamu wa ukalimani na tafsiri nao wanahitajika zaidi ili kuzidi
kueneza lugha hii. Wataalamu wa lugha ya Kiswahili hawapatikani katika vitivo
au ndaki nyingine isipokuwa katika kitivo cha Kiswahili.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinapokea wanafunzi wachache
wanaochukua kozi za Kiswahili na wengine kuhama. Kwa mfano mwaka huu (2016)
wamehitimu wanafunzi 18 tu wa shahada ya awali ya Kiswahili. hata hivyo viko
vyuo vingine Tanzania ambavyo hufundisha Kiswahili kwa digrii ya kwanza nay a
uzamili kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu chaTumaini Makumira Arusha,
Ruaha, Iringa na Chuo Kikuu cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SUZA).
Kipi kifanyike ili kuwapata wataalamu wengi wa Kiswahili? Elimu
kwa wanajamii inatakiwa kutolewa ili jamii itambue umihimu na fursa
zipatikanazo katika lugha ya Kiswahili. Wanajamii wakikombolewa kifikra
tutapata wanafunzi wengi kutokana na wanajamii kuhamasika juu ya thamani ya
lugha ya Kiswahili. Kiswahili kwa sasa ni kisima cha mafanikio kwani wapo
wanaokula, wanaolala na kuishi kutokana na lugha ya Kiswahili. Suala la
ukosefu wa ajira kwa vijana litapungua kwa kuwekeza katika lugha adhimu ya
Kiswahili.
Kupenda lugha yetu ni pamoja na kuiongea mfululizo bila ya
kuchanganya na lugha nyingine. “Longa Kiswahili ujisikie huru” ni moja ya kauli
mbiu ya kongamano la Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili Vyuo Vikuu Afrika
Mashariki (Chawakama) kilichoanzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kukuza Kiswahili
kwa wanafunzi wanaosoma lugha ya Kiswahili vyuoni.
Kusisitiza matumizi ya Kiswahili katika sekta zote za serikali,
sekta za watu binafsi na mashirika ya umma ikiwa ni pamoja na kutumia
mawasiliano kwa maandishi kwa barua zote za kikazi ili kukikuza
Kiswahili. Serikali inatakiwa kutunga na kusimamia sera zitakazoboresha na
kukuza zaidi lugha ya Kiswahili.
Katika
kutekeleza jukumu hili, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) chini ya Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam imeandaa vitabu vya masomo yote ya shule ya sekondari
kuanzia na kidato cha kwanza yakiwamo masomo ya sayansi na Huisabati kwa lugha
ya Kiswahili. Katika kukuza lugha na kuboresha mfumo wa elimu nchini, serikali
haina budi kuutazama mradi huu kwa jicho la tatu kwani kwa kufundisha lugha ya
Kiswahili katika shule za sekondari kutainua lugha ya Kiswahili na kukuza
viwango vya ufaulu nchini.
Comments
Post a Comment