ALHAMISI OKTOBA,3 2019

Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dk Medard Kalemani
Kwa ufupi:
Waziri wa Nishati nchini Tanzania, Dk Medard Kalemani
amemsimamisha kazi muongoza mifumo ya umeme wa kituo cha kupoza nishati hiyo
cha Ubungo jijini Dar es Salaam, Samson Mwangalume.
____________________________________________________________
Dar es Salaam. Waziri wa Nishati nchini
Tanzania, Dk Medard Kalemani amemsimamisha kazi muongoza mifumo ya umeme wa
kituo cha kupoza nishati hiyo cha Ubungo jijini Dar es Salaam, Samson
Mwangalume.
Amechukua uamuzi huo leo
Alhamisi Oktoba 3, 2019 baada ya usiku wa kuamkia leo umeme kukatika huku
chanzo kikielezwa kuwa ni uchafu wa vikombe katika njia za kusafirisha nishati
hiyo.
Dk Kalemani pia ametoa onyo
la mwisho kwa kaimu meneja mwandamizi wa usafirishaji wa umeme, Amos Kahiyula
kuhakikisha haukatiki kutokana na uzembe.
Ametoa maagizo mara baada
ya kutembelea kituo hicho na kutoridhishwa na maelezo ya Kahiyula aliyetoa
sababu hizo baada ya kutakiwa na waziri huyo kueleza chanzo.
"Haiwezekani watu mkae
muda mrefu bila kutazama hali ya vikombe hadi viwe vichafu kiasi cha kusababisha
umeme kukatika, huu ni uzembe usiokubalika kwani serikali imeshawekeza vya
kutosha kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika.”
" Nataka huyo Samson
aliyekuwa mkuu wa zamu asimamishwe kazi kuanzia leo na maelezo yake niyapate
leo ofisini kwangu kwani kama ni vikombe vipo kwa nini hamkuviweka,”
amesema Dk Kalemani.
Ameongeza,
“Pia tulishatoa nyumba kwa wafanyakazi katika kituo hiki ili iwe rahisi
kufika kwenye mitambo kunapotokea tatizo lakini hakuna hata mmoja anayekaa na
badala yake mnakaa majumbani kwenu na kusababisha wengine kutembea hadi
kilometa nne kufika hapa. Hii
haikubaliki.
Kutokana na hilo, amesema mpaka saa nane
mchana leo wafanyakazi sita waliopewa nyumba katika kituo hicho wahamie
kwa kutumia magari ya Tanesco.
Na Nasra Abdallah, Mwananchi nabdallah@mwananchi.co.tz
Na Nasra Abdallah, Mwananchi nabdallah@mwananchi.co.tz
Comments
Post a Comment