Kwa
ufupi
Oktoba
14 mwaka huu, Tanzania itatimiza miaka 20 bila Mwalimu Julius Nyerere. Alikuwa
waziri mkuu wa kwanza wa Tanganyika na baadaye Rais wa kwanza wa Tanganyika na
Tanzania. Habari kuhusu maisha yake zimeandikwa katika magazeti na vitabu. Makala
haya yanaangazia maisha yake ya awali na shule ya msingi. Endelea…
Mtemi Nyerere Burito
(1860-1942) wa kabila la Wazanaki na mkewe, bibi Christina Mugaya wa
Nyang’ombe, miaka 97 iliyopita walipomzaa mtoto waliyemwita Kambarage, hawakujua
kama mtoto wao huyo angekuja kuwa Rais wa Tanganyika miaka 39 baadaye.
Kambarage Nyerere, kama
ambavyo alivyojulikana kabla ya kubatizwa kwake mwaka 1943, alizaliwa Aprili
13, 1922 katika Kijiji cha Butiama karibu na Pwani ya Ziwa Victoria.
Kwa mujibu wa historia ya
maisha yake, wakati wa utoto wake Kambarage alikuwa akiwasaidia wazazi wake
kazi za shambani ikiwa ni pamoja na kuchunga mifugo.
Baadaye Kambarage
alikumbuka maisha yake ya ujanani. Alimwambia mwandishi Marie-Aude Fouere wa
kitabu cha ‘Remembering Julius Nyerere in Tanzania: History, Memory, Legacy’
“nililelewa sawasawa na watoto wengine pale kijijini. Sikupata upendeleo wowote
eti kwa sababu tu baba yangu alikuwa chifu.”
Mama yake Kambarage,
Christina Mugaya alikuwa mke wa tano wa Mzee Burito kati ya wake zake 22. Kwa
mujibu wa Marie-Aude Fouere, wakati Mzee Burito akiwa na miaka 47 ndipo
alipomuoa Mugaya akiwa na miaka 15. Mama Mugaya alimzalia Mzee Burito watoto
wanane, wanne wa kiume (Kambarage akiwa wa pili) na wanne wa kike.
Kwa kadri alivyokiri
mwenyewe, Kambarage alisema maisha yake yaliathiriwa sana na baba yake.
Alipohojiwa na mwandishi William Smith wa kitabu cha ‘Nyerere of Tanzania’
miaka ya 60 alisema “kiwango cha ubinadamu nilichonacho nilirithi kwa baba
yangu,” alisema Kambarage.
Burito hakuwa mwepesi wa
kuamua mambo. Alikuwa mwangalifu sana kabla ya kuchukua hatua na alisisitiza
kila wakati kuwapa watu wake haki zao. Simulizi fulani zinadai kuwa utamaduni
wa Wazanaki ndio uliokuwa na ushawishi mkubwa zaidi tangu utotoni katika uwezo
wa uongozi wa Nyerere kuliko hata elimu aliyoipata baadaye ukubwani.
Katikati ya Aprili 1934,
Kambarage ambaye baadaye aliitwa Julius alilazimika kutembea zaidi ya maili 25
kutoka Butiama kwenda Musoma, akisindikizwa na mmoja wa walinzi wa Mzee Burito
aliyeitwa Kitira Buhoro.
Katika ukurasa wa 46 wa
kitabu chake, ‘Nyerere: The Early Years’, mwandishi Tom Molony anaandika kuwa
baada ya kutembea muda mrefu na kwa kuwa magari yalikuwa yakipita kwa nadra
njia hiyo, hatimaye lilitokea lori ambalo Kitira alilisimamisha, likasimama,
“hapo Kambarage akapanda gari kwa mara ya kwanza” katika maisha yake.
Ingawa ada ya shule
alilipiwa na baba yake, fedha ya kujikimu alipewa na kaka yake aliyeitwa Edward
Wanzagi Nyerere. Wanzagi ndiye aliyekuja kuwa chifu wa mwisho wa Butiama
(1952-61).
Ijumaa ya Aprili 20,
1934, Kambarage alianza rasmi, Shule ya Msingi Mwisenge iliyoko Musoma na
kupewa usajili namba 308. Kati ya walimu waliomfundisha ni James Zangara
Irenge. Mvulana wa kwanza kabisa kukutana na Kambarage shuleni hapo aliitwa
Selemani Kitundu.
Kitundu ndiye baadaye
alikuwa mhamasishaji mkuu wa Chama cha Tanu (Tanganyika African National Union)
tawi la Musoma, ambalo hadi Novemba 1955, kwa mujibu wa kitabu cha ‘Historia ya
Tanu,’ kulikuwa na wanachama 110 tu katika wilaya yote ya Musoma.
Baadaye Kitundu
alikumbuka alivyokutana na Kambarage. Kwa mujibu wa Molony, Kitundu alikumbuka
alipokutana na Kambarage alikuwa amevaa ‘rubega’ na kaptula iliyochanika.
“Alikuwa mwembamba, mwenye macho ‘makali’ na alikuwa mcheshi,” alisema Kitundu.
Aliyekuwa rafiki wa
karibu na Kambarage shuleni Mwisenge ni kijana mwingine wa Kizanaki, Oswald
Mang’ombe Marwa. Kambarage na Mwang’ombe walifahamiana kabla ya kukutana
shuleni kwa sababu baba yake alikuwa ni Chifu Marwa wa Butuguri na rafiki wa
Mzee Burito.
Mang’ombe Marwa, kinasema
kitabu cha ‘Peter DM Bwimbo: Mlinzi Mkuu wa Mwalimu Nyerere,’ baada ya hapo
alikuja kuwa “…mmoja wa walimu wa useremala hapo Bwiru na kwao palikuwa
Butugiri, karibu na Butiama.” Mwang’ombe alifariki dunia Jumapili ya Januari
25, 1970 wakati Kambarage akiwa Rais wa nchi.
Aliyekuwa mshirika
mwingine wa karibu na Kambarage shuleni Mwisenge ni John Nyambeho na Marwa
Ihunyo kutoka Busegwe.
Ihuyo alimwambia Molony
jinsi alivyokumbuka namna kila mwisho wa juma walivyokwenda na Kambarage
kuwinda, na siku moja wote wawili wakamlenga ndege mmoja na wakapata shabaha
yao kwa kumuua, na kwa sababu hiyo “tulianza kuitana binamu ... na kama
tulikuwa na fedha tulikuwa tunakwenda mjini kunywa chai na maandazi.”
Mei 1934, mwezi mmoja
baada ya Kambarage kujiunga na shule hiyo, wavulana walipewa sare yao ya kwanza
ya shule. Kitundu alimwambia Molony kuwa anakumbuka Kambarage alikuwa mwepesi
sana kujibu maswali kwa kasi kubwa.
Baada ya miezi sita
shuleni hapo wanafunzi walifanya mtihani wao wa kwanza. Walioongoza kwa ufaulu
ni Kambarage na Kitundu kiasi kwamba walivushwa darasa, wakitolewa darasa la
kwanza na kuingizwa moja kwa moja darasa la tatu.
Wakiwa darasa la tatu
walifundishwa na walimu Joshua Gunza, James Irenge na Daniel Kirigini. Walimu
wawili miongoni mwa hao watatu, Daniel Kirigini na James Irenge walikuwa hai
wakati wa kifo cha Nyerere Alhamisi ya Oktoba 14, 1999. Kirigini alifariki
dunia mwaka 2002, miaka mitatu baada ya kifo cha Mwalimu akiwa na miaka 104.
Baada ya kifo cha
Kirigini, mwalimu pekee wa Kambarage aliyebaki hai ni Irenge, ambaye mwaka 2002
alikuwa na miaka 91 wakati wa maadhimisho ya miaka mitatu ya kifo cha Mwalimu
Nyerere. Hata hivyo naye alifariki dunia Julai 2012 na kuzikwa Butiama Julai
26, 2012.
Ingawa simulizi fulani
zinadokeza kuwa Kambarage hakuwa mtukutu, alipambana na aliyekuwa mkuu wa
shule, Herman Abdallah kutoka Lindi, ambaye alichukua fedha za wanafunzi bila
ridhaa yao, zikiwamo shilingi mbili za Kambarage. Ingawa aliadhibiwa kwa
kilichodaiwa kuwa ni kumkosea mwalimu wake nidhamu, fedha zake zilirejeshwa.
Historia ya utotoni
inaonyesha kuwa Kambarage hakupenda michezo. Kwake ilikuwa afadhali ashinde
bwenini akijisomea vitabu kuliko kwenda kucheza. Hata hivyo akiwa anajisomea
bwenini, mara kwa mara alikuwa akibughudhiwa na kaka mkuu wa shule, Nyamuhanga
Mageta, huku akimdhihaki kwa wembamba wake. Kwa sababu hiyo aliamua kujitafutia
mahali pengine ambako angeweza kusoma kwa utulivu wakati wengine wakiwa
michezoni.
Kambarage na Mang’ombe
Marwa walijiunga na kituo cha Nyigena Mission ambako walikuwa wakitembea maili
nne kila siku kwa ajili ya mafunzo ya kidini. Ingawa Mang’ombe hakuendelea na
masomo hayo, alibatizwa na kuitwa Oswald Mang’ombe Marwa.
Kambarage alimaliza elimu
ya msingi mwaka 1936 katika Shule ya Msingi Mwisenge. Kwa mujibu wa mwandishi
Godfrey Mwakikagile, katika mitihani yake ya kumaliza shule ya msingi, alikuwa
wa kwanza miongoni mwa wanafunzi wote wa Kanda ya Ziwa na Magharibi.
Comments
Post a Comment