MAKALA: DPP ATOA TAARIFA KUHUSU WAHUJUMU UCHUMI 467 WALIOTUBU

                                                           Chanzo: TBC1
Watuhumiwa 467 wa makosa ya uhujumu uchumi nchini Tanzania wamekiri makosa na kuomba msamaha, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Biswalo ameeleza.
DPP Biswalo Mganga asubuhi ya leo Septemba 30, 2019 amewasilisha ripoti ya suala hilo kwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli na kuongeza kuwa kiasi cha Shilingi bilioni 107 za Tanzania sawa na takribani dola milioni 4.6 zitarejeshwa na watuhumiwa hao.
Rais Magufuli alitoa wiki moja kuanzia Septemba 22 kwa watuhumiwa wote makosa ya uhujumu uchumi kukiri makosa yao, kuomba radhi na kurejesha kiasi cha fedha wanachoshitakiwa kuhujumu.
Hii leo ameongeza tena wiki moja baada ya kuombwa na DPP Maganga ambaye ameeleza kuwa baadhi ya maombi yamekwama magerezani na kwenye ofisi zake za mikoa.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mashtaka ya uhujumu uchumi hayana dhamana, na wote wanaoshtakiwa nayo husalia rumande mpaka kutoka kwa hukumu zao.
"Najua wapo ambao wanadanganywa kuwa huu msamaha ni wa uongo, kuwa wakikubali watakuwa wamejishitaki wenyewe. Wengine wanadanganywa na mawakili ambao wanataka kuendelea kuwachomoa pesa zao. Sasa wachague kuwasikiliza mawakili au wewe DPP na ushauri wangu," amesisitiza Magufuli.
"DPP mfanye haraka, msichukue muda mrefu kupitia maombi hayo ili watu hawa warudi kwenye jumuiya zao. Ikichukua mwezi ama mwaka hata dhana nzima ya msamaha itaondoka."
Toka aingie madarakani takribani miaka minne iliyopita Magufuli amejipambanua kwa kupigana dhidi ya rushwa na ufisadi.
Katika vita hiyo, vigogo kadhaa wa serikali walifutwa kazi kwa tuhuma za uzembe na rushwa.
Watu kadhaa pia wamefunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi na kesi nyingi kati ya hizo bado zinaunguruma.
"Najua wanateseka. Unaona wanavyopelekwa mahakamani, wengine wamekonda kweli, inatia huruma na inaumiza. Najua wengine wanataka kuomba msamaha..." alisema Magufuli Septemba 22, wakati akitangaza msamaha.
Hata hivyo alionya kuwa kwa wale watakaoshindwa kuomba msamaha, waendelee kubanwa hata kama kesi zao zitachukua miaka 20.
"Nimetoa siku saba hizi na baada ya hizi sitatoa tena...watakaoendelea kukaa gerezani wasimlaumu mtu," ameseisitiza hii leo.
Magufuli amefafanua kuwa msamaha wake haufuti sheria juu ya makosa ya uhujumu uchumi nchini humo, na kuwa wale wote watakaonaswa kwa tuhuma hizo waendelee kushtakiwa.
"Huu msamaha hauwahusu wale watakaoshikwa leo na kuendelea. DPP hao muwashughulikie kweli kweli kwa mujibu wa sheria."
Hata hivyo DPP hajatoa hadharani majina ya watu ambao wamemuandikia kuomba radhi.

Sethi na Rugemalira
Image captionWanyabiashara James Rugemalira (kushoto) na Harbinder Sing Sethi (kulia) ni miongoni mwa wafanyabiashara wakubwa wanaokabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.

Baadhi ya watu mashuhuri wanaokabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi ni mwanahabari wa uchunguzi Erick Kabendera.
Mwanahabari huyo anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za kitanzania.
Wafanyabiashara maarufu Harbinder Sing Sethi na James Rugemalira wanaohusishwa na kashfa ya ufisadi ya Tegeta Escrow wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi.
Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Harry Kitilya, pamoja na maafisa wa benki ya Stanbic mlimbwende wa taifa wa zamani (Miss) wa Tanzania Shose Sinare na Sioi Sumari pia wanakabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi.
Wengine waliopo mahabusu kwa mashtaka kama hayo ni viongozi wa kitaifa wa mpira wa miguu, bwana Jamal Malinzi na Michael Wambura ambao ni rais na makamu wa raisi wa zamani wa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF).

Comments