___________________________________________________________
UMUHIMU
WA KISWAHILI KATIKA TAIFA
Mwalimu
J. K. Nyerere ametuasa tusiwe wabinafsi katika masuala yahusuyo taifa. Suala la
ubinafsi amelipiga vita tangu alipoasisi taifa hili na kutuagiza tuondokane na
unafsi kama alivyoandika katika kitabu chake cha ‘Tujisahihishe.’ Kitabu hiki
kilichapishwa mwezi Juni 1962. Kwa maana hiyo, alitupa fursa ya kuielimisha
jamii bila uchoyo na husuda.
Katika
eneo la lugha, tunayo mambo mengi tunayoweza kujifunza kwa faida yetu binafsi,
kwa taifa letu na kwa ulimwengu mzima kwa jumla. Hapa yafaa nitoe ufafanuzi
kidogo. Katika miezi ya hivi karibuni liko jambo lililotokea huko
Uingereza ambalo ni mfano wa kuigwa.
Wabunge
wa Bunge la Uingereza ambao ni wapenzi wa lugha yao ya taifa hawakuridhishwa na
hadhi ya lugha yao inavyotumika kitaifa na kimataifa. Wameishauri
Serikali yao iimarishe ufundishaji wa lugha ya Kiingereza katika shule
zote na hasa vyuo vya lugha. Pia waliishauri serikali kufundisha
Kiingereza kwa umakini mkubwa katika shule na vyuo. Pia walishauri kuwa shule
na vyuo vya lugha viongezewe fedha katika bajeti kila mwaka ili kupatiwa
fedha mwaka hadi mwaka kuanzia mwaka 2011/2012. Pamoja na kutilia mkazo mafunzo
ya lugha yao, wamesisitiza pia lugha za kigeni zisomeshwe kwa watu wa kada
mbalimbali hasa wanadiplomasia.
Kamati
ya Mambo ya Nje ya Bunge imeshauri kuwa kupandishwa vyeo kwa maofisa kutokane
na ujuzi na weledi wa Kiingereza pamoja na lugha moja ya kimataifa.
Wamekubali bajeti kwa mafunzo ya lugha iongezeke kutoka
$ 3 milioni kwa mwaka 2011/12 hadi $ 3.9 milioni kwa mwaka 2013/14. Vilevile
idadi ya wanafunzi kwa mwaka iongezwe na kuwa 1000.
Lugha
kubwa za nchi za nje kama lugha ya Mandarin, Kiarabu, Kihispania na Kireno
zisomeshwe shuleni. Lugha ya Mandarin ni lugha rasmi na lugha ya taifa la
Wachina. Lugha ya Kihispania hutumika katika nchi za Argentina, Chile, Uruguay,
n.k. Kireno hutumika katika nchi za Brazil, Cuba, Venezuela, n.k
Kireno. Nchi za Argentina, Chile, Uruguay, n.k. hutumia
Kihispania. Lugha hizi mbili hutumika katika nchi za Amerika
ya Kusini. Lugha ya Kiarabu nayo inatiliwa mkazo kama lugha muhimu na sababu
kubwa ni za kiuchumi na kisiasa.
Je,
Waingereza wamegundua nini walipoamua kufungua tena chuo chao cha lugha
walichofunga mwaka 2007? Bila shaka wamegundua kuwa nafasi ya lugha ni kubwa
duniani hasa katika mazingira ya utandawazi kama masuala ya diplomasia,
biashara, siasa na uchumi. Uamuzi wa kujifunza lugha ya Kiarabu, Kimandarin,
Kihispania na Kireno ni kuwawezesha Waingereza kujua kwa undani masuala mengi
yanayowahusu Wachina, nchi za Amerika ya Kusini na Waarabu katika
biashara. Kwa upande wa Kiarabu ni dhahiri kuwa ni suala la mafuta.
Katika
bara la Afrika, ziko lugha tofauti ambazo zinatufanya tusielewane kutokana na
sababu za kihistoria. Nchi za Afrika zinatumia lugha zenye asili ya kikoloni
kama Kiarabu, Kifaransa, Kireno na Kiingereza. Hizi ndizo lugha zinazotumika
katika vikao vya Umoja wa nchi za Afrika (AU)
Lugha
ya Kiafrika iliyokubaliwa kutumika katika shughuli za kikazi za AU ni
Kiswahili. Tanzania ilipewa jukumu la kukikuza na kukiendeleza Kiswahili ili
kifikie hadhi ya Kimataifa. Agizo hili lilitolewa mwaka 1988 huko Addis Ababa,
Ethiopia.Tumefikia wapi tangu mwaka 1988 Tanzania ilipoteuliwa katika
kikao kilichofanyika huko Mauritus cha Mawaziri wa Umoja wa Nchi huru za Afrika
(OAU) na kuridhiwa na Wakuu nchi na serikali mwaka huo huo? Ilitakiwa uandaliwe
utaratibu wa mafunzo ya ukalimani na tafsiri kwa ajili ya kuwaandaa
wataalamu kwa kazi katika Umoja wa Nchi Huru za Afrika.
Mafunzo
yaliandaliwa kwa kuwapeleka wataalamu wazalendo waliozifahamu lugha za
Kifaransa, Kiingereza na Kiswahili. Wataalamu hawa walipelekwa Chuo Kikuu
cha Paris kwa kipindi cha mwaka mmoja. Baada ya kufaulu walirejea nyumbani
llakini hawakuelekezwa kujiandaa kwenda Addis Ababa. Mpaka leo mpango wa kwapeleka
Watanzania Addis Ababa haukutekelezwa kikamilifu.
Kwa
suala la ukuzaji wa Kiswahili ndani ya nchi, mipango imekwama ya
kukuza Kiswahili kutokana na kutokuwepo kwa sera ya lugha iliyo wazi. Kila
waziri mwenye dhamana ya kusimamia lugha anapoteuliwa huwa hana mawazo ya
kutupeleka mbele katika kukifanya Kiswahili kiwe ni lugha imara ya kitaifa.
Hapa
nchini kiko kituo cha kufundisha lugha za kigeni huko Zanzibar
linachojulikana kama Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI). Kina
kila sababu ya kuitwa kituo cha lugha kwani kinafundisha lugha za kigeni
kama Kiarabu, Kiingereza , Kijerumani na Kifaransa katika ngazi ya
Diploma kikiwaandaa wataalamu wa ngazi ya kati. Pia kinafundisha Kiswahili kwa
wageni wanaokuja hapa nchini ama kufanya kazi au kujifunza Kiswahili ili
baadaye wakafundishe katika nchi zao.
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itambue kuwapo kwa kituo hiki na kipatiwe
fedha za kutosha. Yanatakiwa maboresho ya hali ya juu ili kukiwezesha
kituo hiki kikidhi vigezo vya kimataifa. Kwa mfano wanatakiwa wahadhiri wenye
digrii za uzamili na uzamivu katika lugha nilizotaja hapo juu pamoja na vifaa
vya kufundishia kama vitabu, video na kanda zake na vilevile maabara kisasa za
lugha kwa ajili ya kufundishia fonetiki, fonolojia na sintaksia.
Kituo
hii kitawavutia wanafunzi wengi kutoka nje na taifa litapata fursa nzuri
ya kujiongezea kipato pamoja na kuwaandaa Watanzania ujipatia ajira nchi za
nje.
Na
Stephen Maina
____________________________________________________________
Faida ya lugha ya Kiswahili kwa Watanzania nchi za SADC
Baadhi ya viongozi wa SADC
Uamuzi wa kuidhinisha matumizi ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya
nne katika Jumuiya ya SADC ni hatua kubwa kwa historia ya maendeleo ya lugha ya
Kiswahili na utamaduni wa kitanzania.
Mpaka sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha rasmi katika Jumuiya za
Kikanda ambazo ni Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa upande wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kiswahili kitasambaa na kuhamasisha wakazi wa nchi
ya Sudan ya Kusini ambao wamejiunga hivi karibuni kujifunza lugha hiyo.
Ni wazi kwamba, Watanzania na baadhi ya nchi za SADC zinazotumia
lugha ya Kiswahili kama Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Malawi na Zambia
watanufaika kama watangulizi na wataalamu wa lugha ya Kiswahili ikilinganishwa
na wanachama wengine wa SADC.
Mkataba wa SADC unaainisha malengo makuu ya kuanzishwa kwa jumuiya
hiyo ikiwemo kukuza umoja, amani na usalama katika mtengamano wetu.
LUGHA KAMA HAKI
Matumizi ya lugha ya Kiswahili yatahakikisha na kuchochea
ufikiwaji wa haki ya ushiriki wa wananchi katika masuala ya maendeleo.
Mathalani ibara ya 21(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa
haki na uhuru kwa kila raia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maamuzi
katika mambo yanayomhusu au kumuathiri. Hivyo basi, Watanzania ambao wengi wao ni wazungumzaji wa lugha ya
Kiswahili, wataweza kuelewa na kushiriki kwa namna tofauti mambo
yatakayofanyiwa maamuzi na Jumuiya ya SADC.
UMUHIMU WA LUGHA YA KISWAHILI
Katika mawanda ya kimataifa lugha ya Kiswahili inazungumzwa na
watu zaidi ya milioni 150 duniani na kwa Afrika Kiswahili kikiwa ni lugha ya
kwanza ya asili inayozungumzwa na watu wengi. Kwa Afrika, Kiswahili kinatumiwa
kwa kiwango kikubwa katika nchi ya Kenya, Uganda, Jamhuri ya Demokrasia ya
Kongo, Tanzania, Burundi, Rwanda na Msumbiji, Malawi na Zambia
Matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mtangamano wa SADC
yanaambatana na faida mbalimbali kama kutambulisha utamaduni wa lugha Kiswahili
ulimwenguni.
Kiswahili kitatambuliwa rasmi katika nchi wanachama 11 ambazo ni
Zimbabwe, Angola, Botswana, Lesotho, Swatini, Afrika ya Kusini, Madagaska,
Mauritius, Seychelles, Namibia na Comoro. Kwa kuwa lugha inabeba vionjo vya
kiutamaduni wa sehemu fulani, faida hii itaambatana na utambulisho wa utamaduni
wa wenyeji wa Tanzania kwa katika nchi hizo. Hivyo, kwa kupitia nchi hizo ni
wazi kwamba Kiswahili kitaendelea kusambaa ulimwenguni.
Vilvile matumizi ya lugha ya Kiswahili yatarahisisha mawasiliano
kwa Watanzania ya katika kutumia fursa zinazopatikana
ndani ya SADC. Faida hii iongeza mwingiliano wa taarifa za kimaendeleo katika
nyanja za kiuchumi, kiutalii, kiutamaduni, kiteknolojia na kisiasa.
Pia, matumizi ya Kiswahili katika Jumuiya ya SADC yanaiweka
Tanzania katika nafasi nzuri ya fursa zinazoambatana na uhitaji wa elimu ya
Kiswahili. Hii inahusisha fursa kwa Tanzania kutoa wataalamu wa kufundisha
Kiswahili katika nchi wanachama, fursa ya kuuza vitabu vya kufundishia
Kiswahili pamoja na nyenzo nyingine za kufundishia Kiswahili kwa nchi hizo.
MAPENDEKEZO
Serikali ya Tanzania iweke mkakati wa kutumia fursa Kiswahili
kutumika katika Jumuiya ya SADC, ikiwemo kuongeza uwekezaji katika elimu ya
kiswahili kwa kuhamasisha wanafunzi wa Kiswahili nchini ili kwenda kuwa walimu
katika nchi wanachama wa SADC, pia kuandaa na kuzalisha nyenzo za kufundishia
na kuweka mkakati wa jinsi ya kuzipeleka katika nchi wanachama
.
Comments
Post a Comment