ELEMENTS OF INCULTURATION IN THE BIBLE
Understanding
the true meaning of the message of Christ is indispensable for the study and
assimilation of inculturation. This article attempts to identify the elements
of inculturation in the Bible. This is because Jesus, whose message is at the
centre of inculturation, though he was God became man and identified with a
specific culture in order to identify with all cultures. The incarnation of
Jesus offered us the opportunities to study his life, and his message of love
of God and of our neighbour. He has equally challenged us to continue his
mission by inserting this message of love in every culture so that his word
will reach the ends of the world.
Going through the Bible and analyzing how
Jesus himself dealt with the issues involved with Jewish tradition gives us an
insight into the process of inculturation. Jesus not only identified with
Jewish tradition but also, as a Jew, celebrated and affirmed most of their
cultural practices while he purified many of these practices by using himself
and the message of his Father as an example for all to follow. The process of
inculturation is very important so that issues like, dualism, syncretism, and
idolatry will be avoided in the practice of the Christian faith. Inculturation,
therefore, presents us not with an option but an obligation. As followers of
Christ, we need to identify ourselves with the culture, the people and the
history of Jesus himself. This will enhance our faith in him for a better
living of the Christian values and Christian life.
Key Words: Inculturation, The Bible, The Law, the Jewish tradition, the Incarnation, Love of God and of neighbor, Christ of Culture, the message of Christ and the Holy Spirit
Key Words: Inculturation, The Bible, The Law, the Jewish tradition, the Incarnation, Love of God and of neighbor, Christ of Culture, the message of Christ and the Holy Spirit
____________________________________________________________
Ufasiri wa matini za Biblia unaendelea kuwa
jambo linalovutia sana hadi siku za leo, ukisababisha majadiliano ya motomoto
ambayo katika miaka hii ya mwisho yamechukua pia sura mpya. Kwa sababu ya
umuhimu wa kimsingi wa Biblia kwa ajili ya imani ya kikristo, kwa maisha ya
Kanisa na kwa mahusiano baina ya wakristo na waamini wa dini nyingine, basi
Tume ya Kipapa ya Biblia imehimizwa kutoa maoni yake mintarafu mada hiyo.
Suala la ufasiri wa Biblia si uvumbuzi wa
nyakati zetu, kama pengine inavyodaiwa. Biblia yenyewe yathibitisha kuwa
ufasiri wake unaleta magumu mbalimbali. Maana, pamoja na sehemu zake
zinazoeleweka kwa dhahiri zimo nyingine zisizoeleweka vizuri. Mathalani,
Danieli anaposoma sehemu kadhaa za kitabu cha Yeremia alikuwa akijihoji kwa
kirefu kuhusu maana yake (Dan 9:2). Tena, kadiri ya Matendo ya Mitume, mtu wa
Kushi wa karne ya kwanza alikuwa katika hali ileile mintarafu sehemu fulani ya
kitabu cha Isaya (Isa 53:7-8), akitambua kwamba anahitaji msaada wa mwenye
kumfasiria (Mdo 8:30-35). Na hatimaye Waraka wa pili wa Petro unashuhudia
kwamba “hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu
fulani tu” (2Pet 1:20); na tena, kwa upande mwingine, unasisitiza kuwa katika
nyaraka za Mtume Paulo “yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo
watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko
mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe” (2Pet 3:16).
Hivyo, suala hilo ni la zamani, lakini katika
mfululizo wa nyakati suala hilo limekithiri: maana, karne ishirini ama
thelathini zamtenganisha tayari msomaji na matukio na misemo vinavyosimuliwa
katika Biblia; na hilo halina budi kuleta magumu mbalimbali. Kwa upande
mwingine, kwa sababu ya maendeleo ya sayansi za kibinadamu, masuala yahusuyo
ufasiri yamekuwa tata zaidi katika nyakati za leo. Mbinu kadhaa za kisayansi
zimekamilishwa kwa ajili ya utafiti juu ya matini za kale. Sasa je, kwa kiasi
gani mbinu hizo zaweza kutazamwa kuwa zinaufaa ufasiri wa Maandiko Matakatifu?
Kwa muda mrefu busara ya kichungaji ya Kanisa imelijibu swali hilo kwa
utaratibu sana, kwa sababu mara nyingi mbinu hizo (ingawa zina mazuri
yanayokubaliwa ndani yake) zilikuwa zinafungamana na rai zilizo kinyume cha
imani ya kikristo. Ila maendeleo mazuri yamefanyika, yenye hatua maalum katika
mfululizo wa hati za Mababa Watakatifu, kuanzia na ensiklika Providentissimus Deus ya
Leo XIII (18 Novemba 1893) hadi ensiklika Divino afflante Spiritu ya
Pius XII (30 Septemba 1943). Tena maendeleo hayo yamethibitishwa na tamko Sancta
Mater Ecclesia (21 Aprili 1964) la Tume ya Kipapa ya Biblia, na
hususan na hati ya kidogma Dei Verbum ya Mtaguso
Mkuu wa Vatikano II (18 Novemba 1965).
Hivyo, mwelekeo huo wenye kujenga unaleta na kuonyesha wazi matunda yake. Mitaala ya kibiblia imehimizwa sana katika Kanisa Katoliki na thamani yake ya kisayansi imegunduliwa zaidi na zaidi kati ya wasomi na waamini. Dialogia ya kiekumeni imerahisishwa sana. Biblia imezidi kuathiri theolojia, na kutoa mchango wake kwa upyaisho wa theolojia. Shauku ya Biblia imeongezeka kati ya wakatoliki, ikiyasaidia maendeleo ya maisha ya kikristo. Nao wote waliopata mafunzo madhubuti katika uwanja huo hudhani kuwa sasa haiwezekani kuirudia tena awamu ya ufasiri wa maandishi iliyotangulia ile ya kiuhakiki. Maana hao hutazama awamu iliyotangulia kama isiyotosheleza tena.
Lakini, pindi mbinu ya kisayansi iliyosambaa zaidi – yaani mbinu ya “kihistoria-kiuhakiki” – inapotumika kwa kawaida katika ufafanuzi, hata ule wa kikatoliki, papo hapo mbinu hii inajadiliwa tena, na kutiliwa mashaka: kwa upande mmoja katika mazingira ya kisayansi, kwani mbinu na njia nyingine zimejitokeza; kwa upande mwingine, kwa sababu ya malalamiko ya wakristo wengi wanaodhani kuwa mbinu hii haitoshelezi kwa upande wa imani. Mbinu ya kihistoria-kiuhakiki, linavyoeleza jina lake lenyewe, inazingatia hasa mabadiliko ya kihistoria ya matini mbalimbali au ya mapokeo yake katika mfululizo wa nyakati – utaratibu huu huitwa “diakronia”. Lakini katika mahali na mazingira fulani mbinu hii inashindana siku hizi na mbinu nyingine zinazosisitiza umuhimu wa kuzielewa matini mbalimbali kwa kuzitazama kwa jumla katika fani yake – utaratibu huu huitwa “sinkronia”, uwe kuhusu lugha yake, ama utungaji, ama muundo wa masimulizi, ama, tena, juhudi yake ya kushawishi. Na tena, mbinu za kidiakronia hujishughulisha kuielewa historia ya utungaji wa matini katika nyakati zilizopita. Lakini badala yake siku hizi walio wengi wanapendelea kuzihoji matini zenyewe wakiziweka katika mtazamo wa nyakati za sasa: yaani mtazamo wa kifalsafa, kiudodosinafsi, kisosholojia, kisiasa, n.k. Wingi huo wa mbinu na njia huthaminiwa na wengine kama dalili ya utajiri, Lakini wengine bado wanauelewa kama sababu ya fujo kubwa.
Nayo fujo – iwe ya kweli au ya kusingizia – inawaletea hoja mpya wapinzani wa ufafanuzi wa kisayansi. Kwao, mgongano huo wa fasiri mbalimbali huonyesha kwamba hakuna faida yoyote itokanayo katika kuzipitisha matini za Biblia chini ya madai ya mbinu za kisayansi, kinyume chake kuna hasara kubwa. Tena hawa husisitiza kuwa ufafanuzi wa kisayansi matokeo yake ni kuzusha mashaka na wasiwasi kuhusu vipengele vingi ambavyo kwanza vilikuwa vimekubalika kwa amani. Na wakati huohuo wafafanuzi wengi hushawishiwa kuyakubali maoni yanayopingana na imani ya Kanisa mintarafu masuala makuu sana, kama vile kuchukuliwa mimba kwa Yesu na Mama Bikira, miujiza yake Yesu na pia ufufuko wake na umungu wake.
Na ufafanuzi wa kisayansi, hata pale ambapo hauleti mashaka haya, kwa vyovyote, kadiri ya wengine, ni mtindo usiozaa chochote kuhusu mafanikio ya maisha ya kikristo. Badala ya kufungua mlango wa kuingia kwa urahisi na uhakika zaidi katika chemchemi zilizo hai za Neno la Mungu, unaifanya Biblia kuwa kitabu kilichofungwa, ambacho ufasiri wake daima ni mgumu na wenye kudai utaalamu wa hali ya juu. Hivyo ufasiri wa Biblia unakuwa mada kwa ajili ya wataalamu wachache waliobobea. Wengine wanawabandikia hao msemo ule wa Injili, “Mmeuondoa ufunguo wa maarifa. Wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia” (Lk 11:52; taz. Mt 23:13).
Kutokana na hayo, yadhaniwa kuwa ni lazima nafasi ya ufafanuzi wa kisayansi – ulio kazi nzito na ya saburi – ichukuliwe na mbinu nyingine zilizo sahili zaidi, kama vile mojawapo ya mbinu za kisinkronia zinazotazamwa kuwa zatosha. Au pengine yashauriwa kuwa bora ule ufasiri wa Biblia uitwao “wa kiroho”, yaani usomaji unaoongozwa tu na kariha (inspiration) ya kila mmoja binafsi na wenye lengo la kuilisha kariha hiyo tu. Wengine wanatafuta katika Biblia hasa picha fulani ya Kristo kadiri ya maoni yao binafsi, na kuridhisha kwa hisia zao binafsi za kidini. Na wengine tena wanadai kuyapata moja kwa moja katika Biblia majawabu kwa kila swali la kibinafsi ama la kijumuiya. Aidha ni vingi vidhehebu vinavyodai kuwa ni wa kweli ufasiri wa aina moja tu, nao ndio unaopatikana kwa njia ya ufunuo wao binafsi.
Kwa sababu hizo, yafaa kuvichunguza kwa makini vipengele mbalimbali vya ufasiri wa kibiblia vilivyopo hadi leo; tena kuzingatia upinzani, malalamiko na matarajio yanayotolewa kuhusu suala hilo; kutathmini fursa zinazofunguliwa na mbinu na njia mpya; na hatimaye kujaribu kuueleza wazi uelekeo unaowiana zaidi na utume wa ufafanuzi katika Kanisa Katoliki.
Hayo ndiyo madhumuni ya hati hii. Tume ya Kipapa ya Biblia inataka kuzionyesha njia za kupitia ili kuufikia ufasiri wa Biblia ulio aminifu zaidi kwa maumbile yake ya kibinadamu na ya kimungu kwa pamoja. Hati hii haijidai kuamua mintarafu masuala yote yahusuyo Biblia, kama vile, k.m., theolojia ya uvuvio. Bali Tume hiyo inadhamiria kueleza zile mbinu zinazoweza kusaidia kwa manufaa ili kuuthamini utajiri wote uliopo katika matini za Biblia, kusudi Neno la Mungu lipate kuwa zaidi na zaidi chakula cha kiroho kwa wanashirika wa taifa lake; tena liwe kwao chemchemi ya maisha ya imani, tumaini na upendo, na hivyo kuwa pia nuru kwa wanadamu wote (Taz. Dei Verbum,21).
Ili kuifikia shabaha hiyo, hati hii: 1. itaeleza kwa kifupi mbinu na njia[1] mbalimbali zinazotumika, pamoja na kuonyesha msaada zinaotoa na mipaka yake; 2. itachunguza masuala kadhaa ya hemenetiki; 3. itatafakari juu ya vipengele vilivyo maalum vya ufasiri wa kikatoliki wa Biblia na uhusiano wake na fani nyingine za kitheolojia; 4. hatimaye itazingatia nafasi ambayo ufasiri wa Biblia unashika katika maisha ya Kanisa.
Mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ni mbinu ya lazima
kwa ajili ya uchambuzi wa kisayansi wa maana ya matini za kale. Maadam Maandiko
Matakatifu – yaliyo “Neno la Mungu katika lugha ya kibinadamu” – yametungwa na
watunzi wa kibinadamu katika sehemu zake zote na machimbuko yake yote, ufahamu
wake sahihi unakubali utumiaji wa mbinu hii kama halali, unauhitaji, na tena
zaidi, unaudai.
Ili kuitathmini sawasawa mbinu hii katika hali
yake ya sasa, yafaa kutupa jicho katika historia yake. Baadhi ya vipengele vya
mbinu hii ya kiufasiri ni vya kale sana. Tangu zamani vilitumika na wafafanuzi
wa kigiriki kwa kufasiri maandishi ya fasihi bora ya Kigiriki na Kilatini (classical
literature); na baadaye, wakati wa Mababa wa Kanisa, vikatumika na
waandishi kama Orijene, Yeronimo na Augustino. Lakini wakati huo mbinu yenyewe
ilikuwa haijakamilishwa. Miundo yake ya siku za leo ni matokeo ya ukamilishaji
uliofanyika hasa kuanzia zama za wahumanisti wa “Mwamsho wa elimu mpya” (Renaissance
humanists) kwa njia ya utaratibu walioanzisha wa kuyarudia
machimbuko ya maandishi asilia (recursus ad fontes). Hivyo, ingawa uhakiki
wa matini za Agano Jipya ulijiendeleza kama fani ya kisayansi kuanzia
tu karne ya 19, yaani wakati ulipojitenga na textus receptus (yaani, matini
zilizokubalika kimapokeo), kumbe uhakiki wa kifasihi(au wa
maandishi) chanzo chake kinapatikana kuanzia karne ya 17, kwa uvumbuzi wa
Richard Simon. Msomi huyo alionyesha kwamba katika vitabu vya Pentateuko kuna
masimulizi yanayorudiwa mara mbili, tena kuna hitalafu katika maudhui yake,
pamoja na tofauti za mtindo wa ufasaha. Basi hayo yote yalionekana kuwa
hayapatani kirahisi na wazo la kuwa mtunzi wa vitabu hivyo ni mtu mmoja tu,
yaani Musa. Katika karne ya 18 Jean Astruc alijaribu kutoa sababu kwamba Musa
alitumia machimbuko mengi (hasa mawili muhimu zaidi) ili kutunga kitabu cha
Mwanzo; lakini baadaye uhakiki ukapinga zaidi na zaidi wazo la kuwa Musa
mwenyewe ndiye mtunzi wa Pentateuko. Nao uhakiki wa kifasihi kwa muda mrefu
ukafanya bidii kwa lengo la kupambanua machimbuko mbalimbali ya matini. Hivyo,
katika karne 19 ikakamilishwa nadharia iliyoitwa “ya kihati” (documentary
hypothesis) kwa minajili ya kueleza uhariri wa Pentateuko.
Kadiri ya nadharia hiyo, ndani ya Pentateuko zimechangamana hati nne, ambazo
kwa sehemu zinafanana; nazo zaitwa ile ya kiYahvisti (J); ile ya kiElohisti
(E), ile ya kiDeuteronomisti (D), na ile ya kikuhani (P: kutoka Kijerumani
“Priester”). Mintarafu hati hii ya kikuhani huenda aliitumia mhariri wa mwisho
ili kuzifunganisha hati zote kwa pamoja. Kwa njia inayofanana, ulielezwa pia
utungaji wa Injili ndugu tatu (Sinoptiki), ambazo ndani yake zina mambo mengine
yanayolingana, na mengine yanayohitilafiana. Hivyo imebuniwa nadharia iitwayo
ya “machimbuko asilia mawili” (“two source” hypothesis), ambayo kadiri yake
Injili za Mathayo na Luka huenda zilitungwa kutokana na machimbuko mawili ya
msingi: yaani, kwa upande mmoja, Injili ya Marko, na, kwa upande mwingine,
mkusanyo fulani wa maneno ya Yesu (uitwao Q, kutoka katika Kijerumani Quelle,
m.y. “chimbuko”). Katika kiini chake, nadharia hizi mbili zinatumika bado hadi
leo katika ufafanuzi wa kisayansi, ijapokuwa zinaleta ubishi.
Kwa kutarajia kuweka sawa mfuatano wa matini za Biblia kadiri ya wakati wa utungaji wake, uhakiki wa kifasihi ulifanya kazi tu ya kuzitenga sehemu mbalimbali za matini na kuzichambua, ili kupambanua machimbuko yake. Katika harakati hiyo uhakiki ulikuwa hauzingatii kwa kutosha muundo wa mwisho wa matini yenyewe ya Biblia, na pia ujumbe inaoueleza katika hali yake ya mwisho (yaani kazi ya wahariri ilithaminiwa kidogo tu). Kwa sababu hiyo ufafanuzi wa kihistoria-kiuhakiki uliweza kuonekana kama mbinu yenye kupindua na kudhuru matini, hasa kwa sababu baadhi ya wafafanuzi wa wakati huo walikuwa wanatoa maoni yenye kukanusha Biblia. Maana waliathiriwa na mbinu za historia linganishi ya dini mbalimbali – kama zilivyotekelezwa wakati huo – na pia na dhana za kifalsafa.
Hermann Gunkel aliondoa mbinu hii katika mipaka finyu ya uhakiki wa kifasihi wenye mtazamo wa namna hii. Naye, ijapo aliendelea kuvitazama vitabu vya Pentateuko kama mikusanyo ya hati, alifanya utafiti kuhusu mfumo wa pekee wa vifungu vyake mbalimbali akijaribu kuainisha utanzu wa kila kimoja (k.m. “hadithi” au “utenzi”), pia mazingira asilia au Sitz im Leben (k.m. mazingira ya kisheria, ya kiliturujia, n.k.). Na utafiti huo kuhusu tanzu za fasihi ukaunganika na “uchambuzi wa kiuhakiki wa fani” (Formgeschichte) uliozinduliwa na Martin Dibelius na Rudolf Bultmann katika ufafanuzi wa Injili ndugu (Sinoptiki). Naye Bultmann alichanganya mitaala hiyo ya “Formgeschichte” na hemenetiki ya Biblia iliyoathiriwa na falsafa ya “ki-eksistensialisti” ya Martin Heidegger. Matokeo yake yakawa kwamba mbinu ya Formgeschichte ikazusha mara nyingi mashaka mazito. Lakini mbinu hiyo, kwa yenyewe, ilileta matokeo ya kuonyesha kinaganaga zaidi kwamba mapokeo yaliyorekodiwa katika Agano Jipya yamepata asili yake na muundo wake wa msingi katika jumuiya ya kikristo, yaani Kanisa la mwanzoni; na hapo ndipo mahubiri ya Yesu mwenyewe yalipoingia katika mahubiri (ya mitume) yanayotangaza kuwa Yesu ndiye Kristo.
Aidha, baada ya Formgeschichte ilijitokeza mbinu ya Redaktionsgeschichte, yaani “uchambuzi wa kiuhakiki wa uhariri”. Hiyo mbinu inajaribu kuuvumbua mchango wa binafsi ulioletwa na kila mwinjili, na mawaidha ya kitheolojia yaliyoongoza kazi yake ya uhariri. Hivyo, kwa kutumia mbinu hii ya mwisho, mfululizo wa hatua mbalimbali za mbinu ya kihistoria-kiuhakiki umekamilika zaidi: toka uhakiki wa matini tunaingia uhakiki wa kifasihi unaoyagawa maandishi yenyewe ili kutafuta machimbuko yake; kishapo tunaingia uchambuzi wa kiuhakiki wa tanzu, na hatimaye uchanganuzi wa uhariri ambao unaizingatia matini katika utungaji wake. Hivyo basi, imewezekana kuelewa wazi zaidi azma ya watunzi na wahariri wa Biblia, kama vile ujumbe wao kwa walengwa wa kwanza. Ndiyo sababu mbinu ya kihistoria-kiuhakiki imejipatia nafasi muhimu sana hadi leo.
Kanuni za msingi za mbinu ya
kihistoria-kiuhakiki katika muundo wake halisi ndizo zifuatazo:
Ni mbinu ya kihistoria, si tu
kwa sababu inaelekea matini za kale – na hapa inazungumziwa Biblia – na
kutafiti maana yake ya kihistoria; bali hasa kwa sababu inajaribu kugundua kwa
dhahiri michakato ya kihistoria ya utungaji wa matini za Biblia; nayo ni
michakato ya kidiakronia ambayo pengine imetatizwa kwa sababu ya kuchukua muda
mrefu. Na matini hizo za Biblia, katika hatua mbalimbali za utungaji wake,
ziliwaelekea wasikilizaji au wasomaji wa jamii mbalimbali, walioishi katika
mazingira tofauti ya mahali na nyakati.
Ni mbinu ya kiuhakiki, kwa maana katika kila hatua yake inatenda kazi kwa msaada wa vigezo vya kisayansi vilivyo halisi iwezekanavyo (kuanzia hatua ya uhakiki wa matini hadi uchambuzi wa kiuhakiki wa uhariri); nayo mbinu inadhamiria kumwezesha msomaji wa nyakati zetu kuelewa maana ya matini za Biblia, ambayo mara nyingi ni vigumu kuipata.
Maadamu ni mbinu ya uchanganuzi wa kisayansi, inachunguza matini ya Biblia kama ifanyavyo kwa matini nyingine zozote za kale na kuieleza kama ufasaha wa kibinadamu. Lakini, hata hivyo inamsaidia mfafanuzi kuelewa vizuri zaidi maudhui ya ufunuo wa kimungu, hususan kwa njia ya uchambuzi wa kiuhakiki wa uhariri wa matini.
Katika awamu ya sasa ya maendeleo yake, mbinu ya kihistoria-kiuhakiki inapitia hatua hizo zifuatazo:
Uhakiki wa matini – unavyofanyika tangu muda mrefu zaidi – unafungua mfululizo wa kazi za kisayansi. Unazingatia ushuhuda wa miswada (manuscripts) iliyo ya kale zaidi na bora zaidi, na pia wa papiri, pia wa tafsiri za kale na wa Mababa wa Kanisa. Tena, ikifuata kanuni maalum, inafanya bidii kutambua matini ya Biblia inayokaribia zaidi ile ya asili.
Aidha matini inafanyika utafiti kiisimu (wa kimofolojia na wa kisintaksi) na kisemantiki, unaotumia maarifa yatokanayo na mitaala ya filolojia ya kihistoria. Ndipo uhakiki wa maandishi unapojibidisha kugundua katika matini mwanzo na \mwisho wa kila sehemu yenye umoja ndani yake, iwe ndefu ama fupi; tena unanuia kuhakikisha mshikamano (internal coherence) uliomo ndani ya matini.
Na pengine kuna masimulizi yanayorudia mara mbili, ama tofauti zisizopatana kati yake, na dalili nyingine za namna hii; hayo yote huonyesha kuwa baadhi ya matini zimechanganya pamoja hati mbalimbali. Hivyo hizo matini zinagawanywa katika sehemu ndogo zenye umoja kati yake, na hizo sehemu zinapelelezwa mintarafu machimbuko yanayoweza kuwa asili yake. Halafu juhudi za uhakiki wa tanzu zinaelekea kutambua tanzu za fasihi na mazingira zilimochipuka, tena tabia maalum ya kila utanzu, na historia ya mabadiliko yake. Kisha, uhakiki wa mapokeo inazitia matini katika mikondo ya mapokeo ambayo inachunguzwa nao ili maendeleo yake katika mtiririko wa historia yaeleweke. Na hatimaye uhakiki wa uhariri unatafiti mabadiliko yaliyoletwa kabla ya hizo matini kupata sura yake ya mwisho, na kisha unachambua sura hiyo ya mwisho ukijitahidi kupambanua maelekeo yake maalum. Kwa hiyo, kati ya hatua hizo zote, zile za kwanza zinafanya bidii ili kuifafanua matini pamoja na asili yake, kwa mtazamo wa kidiakronia; lakini hatua hiyo ya mwisho inamalizia kwa uchunguzi wa kisinkronia: yaani inafafanua matini kwa yenyewe, kwa kuzingatia mahusiano yaliyopo kati ya sehemu zake mbalimbali; na mwishowe huizingatia kama ujumbe kwa watu wa nyakati zake. Na hapo ndipo yaweza kuchunguzwa dhima ya matini ya kuathiri kiutendaji (function pragmatique).
Ikiwa matini zinazochambuliwa zinaingia katika utanzu wa kifasihi ulio wa kihistoria, ama zinahusiana na matukio ya historia, uhakiki wa kihistoria yatimiliza kazi ya uhakiki wa kifasihi kwa kueleza vizuri uzito wake wa kihistoria, kadiri ya maana ya kisasa ya usemi huo. Basi, kwa njia hii zaangazwa hatua mbalimbali za maendeleo halisi ya ufunuo wa kibiblia.
Je, mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ina thamani ipi, hasa katika awamu ya sasa ya maendeleo yake?
Ni mbinu ambayo, ikitumika kwa namna iliyo nyofu, haina kisamkasa (a priori) kwa yenyewe. Ila kama matumizi yake yanaandamana na kisamkasa, hilo basi halitokani na mbinu yenyewe, bali na maamuzi na kihemenetiki yanayouongoza ufasiri, nayo yaweza kuwa ya mapendeleo.
Katika asili yake mbinu hii ilielekezwa kwenye uhakiki wa machimbuko na kwenye historia ya dini mbalimbali; hivyo ikaleta matokeo ya kuufungua mlango mpya wa kuiendea Biblia, ikionyesha kuwa Biblia ni mkusanyo wa maandishi ambayo, ilivyo mara nyingi, hasa katika Agano la Kale, si kazi ya mwandishi mmoja; na pengine miswada yake ilipitia historia ndefu kabla haijafikia kuchukua sura yake ya mwisho. Na historia hiyo hufungamana kabisa na historia ya taifa la Israeli au ya Kanisa la mwanzoni. Kabla ya mbinu hii kutokea, ufasiri wa Biblia wa kiyahudi au wa kikristo ulikuwa haukuelewa kwa dhahiri mazingira halisi mbalimbali ya kihistoria ambamo Neno la Mungu lilitia mizizi yake. Ulikuwa ukiyaelewa kwa ujumla na kwa mbali. Na mapambano yakatokea baina ya ufafanuzi wa kimapokeo na mbinu ya kisayansi, nayo yakaleta maumivu; maana mwanzoni hiyo mbinu ya kisayansi ilikuwa imeachana kwa makusudi na mtazamo wa imani na pengine iliipinga imani. Lakini baadaye mbinu hiyo ikajionyesha kuwa ya kufaa: yaani ilipojiokoa na athari hizo za nje (external prejudices) ikaleta ufahamu sahihi zaidi wa ukweli wa Maandiko Matakatifu (taz. Dei Verbum, 12). Kadiri ya Divino afflante Spiritu, utafiti wa maana sisisi ya Maandiko ndio wajibu mahsusi wa ufafanuzi; lakini ili kuutekeleza huo wajibu inahitajika kuzipambanua tanzu za kifasihi za matini (Taz. Enchiridion Biblicum [=EB], 560); nalo, basi, lafanyika kwa njia ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki.
Bila shaka, matumizi halisi ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki huonyesha mipaka yake, maana hubana utafiti wa maana ya matini ya Biblia ndani ya mazingira ya kihistoria kwa wakati ilipotungwa, wala haijali uwezekano wa maana nyingine zilizojidhihirisha katika mihula iliyofuata ya ufunuo wa kibiblia na ya historia ya Kanisa. Japo hivyo, mbinu hii imechangia katika utungaji wa vitabu vya thamani kubwa vya ufafanuzi na vya theolojia ya kibiblia.
Tangu muda mrefu limeachwa wazo la kufungamanisha mbinu hiyo na mfumo wa kifalsafa. Na hivi karibuni mwelekeo wa kiufafanuzi umejitokeza wenye kuielekeza mbinu hii ili izingatie hasa fani (form) ya matini kuliko maudhui (content) yake; lakini mwelekeo huo ulisahihishwa kwa msaada wa semantiki ya ngazi mbalimbali (semantiki ya maneno, ya sentensi na ya matini) na pia wa uchunguzi wa jinsi matini zinavyoathiri kiutendaji (aspect pragmatique).
Aidha, mintarafu matumizi ya uchanganuzi wa kisinkronia wa matini ndani ya utaratibu wa mbinu hii, yatupasa tukubali kuwa ni kazi halali kwani kinachozingatiwa hapo ni matini katika hali yake ya mwisho, ambayo ndiyo yenye Neno la Mungu, wala si uhariri wa katikati. Lakini inabaki kuwa chunguzi za kidiakronia ni za lazima ili kufahamisha mkikimkiki wa kihistoria uliomo ndani ya Maandiko Matakatifu na kudhihirisha utajiri wa mchangamano wake: kwa mfano, kanuni ya Agano (Kut 21-23) huonyesha mazingira ya kisiasa, kijamii na kidini ya jamii ya kiisraeli yaliyo tofauti na yale yanayoonyeshwa na kanuni za sheria nyinginezo zihifadhiwazo katika Kumbukumbu la Torati (Kum 12-26) na katika Mambo ya Walawi (sheria za utakatifu, Law 17-26). Kumbe miaka ya nyuma mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ilikemewa kwa maana ilizingatia mno mandhari ya kihistoria katika ufafanuzi; lakini sasa yabidi kukwepa isiingie katika tabia iliyo kinyume ya kuusahau umuhimu wa historia na kuuzingatia ufafanuzi wa kisinkronia tu.
Basi, kwa ujumla madhumuni ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki ni kuipambanua maana iliyonuiwa na waandishi na wahariri hasa kwa utaratibu wa kidiakronia. Kwa msaada wa mbinu na njia nyinginezo, mbinu hiyo humfungulia msomaji wa nyakati zetu mlango wa kupata maana ya matini ya Biblia, tulivyoipokea sisi.
Hakuna mbinu yoyote ya kisayansi kwa mtaala wa
Biblia iwezayo kuudhihirisha utajiri wote wa matini za Biblia. Yoyote ile iwe
thamani yake, mbinu ya kihistoria-kiuhakiki haiwezi kudai kuyatosheleza masuala
yote. Nayo kwa vyovyote huacha gizani masuala mengi yahusuyo maandishi
yanayofanyiwa utafiti. Hivyo hatutashangaa tukiona kuwa siku hizi mbinu na njia
nyinginezo hutolewa ili kuchimba zaidi masuala fulani fulani yastahiliyo
kuchunguzwa kwa makini.
Katika ibara hii B tutaeleza baadhi ya mbinu za uchanganuzi wa kifasihi zilizojitokeza hivi karibuni. Halafu katika ibara zifuatazo (C, D, E) tutazichunguza kwa kifupi njia mbalimbali, ambazo baadhi yake zahusiana na mtaala wa mapokeo, nyingine na “sayansi za kibinadamu”, na nyingine tena na mazingira maalumu ya kisasa. Na hatimaye (F) tutauzingatia usomaji wa kifundamentalisti wa Biblia unaokataa kila jitihada ya kimpangilio ya ufasiri.
Hivi basi, ufafanuzi wa Biblia ukifaidi maendeleo ya mitaala ya kiisimu na kifasihi andishi ya nyakati zetu, hutumia zaidi na zaidi mbinu mpya za uchanganuzi wa kifasihi, na hasa uchanganuzi wa kibalagha, uchanganuzi wa kisimulizi, na uchanganuzi wa kisemiotiki.
Kwa kusema ukweli, uchanganuzi wa kibalagha kwa
wenyewe si mbinu mpya. Ila kilicho kipya ni, kwa upande mmoja, matumizi yake
yenye utaratibu kwa ajili ya kuifasiri Biblia, na, kwa upande mwingine,
kuchanua na kusitawi kwa “balagha mpya”.
Balagha ni sanaa ya kutunga hotuba zenye kushawishi. Na kwa sababu maandishi yote ya Biblia ni kwa namna fulani matini zenye kushawishi, ujuzi fulani wa balagha ni sehemu mojawapo ya elimu ya kawaida ya wafafanuzi. Uchanganuzi wa kibalagha lazima uendeshwe kwa utaratibu wa kiuhakiki, kwa maana ufafanuzi wa kisayansi ni kazi ambayo haina budi kuyatii madai ya roho ya kiuhakiki.
Chunguzi nyingi za siku za karibuni zimezingatia kwa makini kuwepo kwa balagha katika Maandiko. Inawezekana kuainisha njia tatu tofauti. Ya kwanza ina msingi katika balagha bora (classical rethoric) ya Kigiriki na ya Kilatini; ya pili hutazama taratibu za utungaji za kisemiti; na ya tatu hufuatilia tafiti za kisasa ziitwazo “balagha mpya”.
Mazingira yoyote yale ya hotuba huleta kuwepo kwa mambo matatu: msemaji (au mwandishi), hotuba (au matini) na wasikilizaji (au walengwa). Hivyo yatokana kwamba balagha bora hutofautisha mambo matatu yenye kuchangia katika ufasaha wa hotuba: mamlaka ya mlumbaji, hoja zinazotolewa katika hotuba kwa kushawishi, na hisia zinazoamshwa katika wasikilizaji na hotuba yenyewe. Tofauti za mazingira na za walengwa huathiri sana mtindo wa kuongea. Kuanzia Aristotle, balagha bora yaainisha tanzu tatu za ufasaha: utanzu wa kihukumu (mbele ya mahakama), utanzu wa kimajadiliano (katika mikutano ya kisiasa), na utanzu wa kidhihirisho (katika ibada).
Madhali balagha iliathiri sana utamaduni wa kiyunani, idadi inayozidi kuongezeka ya wafafanuzi hutumia vitabu vya balagha bora ili kuchambua vizuri zaidi mandhari kadhaa za maandishi ya kibiblia, hasa yale ya Agano Jipya.
Aidha, wafafanuzi wengine huvitazama kwa makini vipengele mahsusi vya mapokeo ya kifasihi ya kibiblia. Nayo yakiwa yameasisiwa katika utamaduni wa kisemiti, huonyesha kupendelea sana mitungo ya kiurari, ambayo huweka mahusiano maalum kati ya sehemu mbalimbali za matini.
Utafiti wa mitindo ya aina nyingi ya usambamba na wa taratibu nyingine za utungaji za kisemiti wawezesha kupambanua kinaganaga zaidi muundo wa kifasihi wa matini na hivyo kuufikia ufahamu mzuri zaidi wa ujumbe wake.
Ikichukua mtazamo mpana zaidi, “balagha mpya” haitaki kuwa tu orodha ya tamathali za lugha, ya maarifa ya walumbaji, au ya mitindo ya hotuba. Mbinu hiyo inatafiti ni kwa sababu gani matumizi fulani ya lugha yalifikia lengo lililokusudiwa na kufaulu kusadikisha dhana fulani; tena inajaribu kuyaeleza mambo yalivyo, ikikataa kujifungia ndani ya mipaka ya uchanganuzi wa mitindo ya ufasaha tu; huyatilia maanani ipasavyo mazingira ya majadiliano; na hatimaye inachambua mitindo na tungo kama vyombo vya kuchochea utendaji kwa wasikilizaji. Kwa lengo hilo yanufaika na kutumia michango ya hivi karibuni ya fani mbalimbali kama vile isimu, semiotiki, anthropolojia na sosholojia.
Kuhusu Biblia, “balagha mpya” yajaribu kupenya katika mtima wa lugha ya ufunuo ikitazamwa kabisa kama lugha ya kidini yenye kushawishi, pia yajaribu kutathmini jinsi inavyoathiri mazingira ya kijamii ya mawasiliano.
Hivyo, uchanganuzi wa kibalagha huutajirisha mtaala wa uhakiki wa matini, na kwa sababu hiyo unastahili heshima kubwa, hususan katika machakura yake ya hivi karibuni. Nao unauponya uzembe ulioendelea kwa kitambo kirefu na kuvumbua ama kuiangaza zaidi mitazamo mipya.
“Balagha mpya” ina haki kuutilia mkazo uwezo wa lugha wa kuathiri na kushawishi. Maana Biblia si tangazo tu la kweli mbalimbali, lakini ni pia ujumbe wenye dhima ya mawasiliano katika mazingira fulani; tena ni ujumbe wenye nguvu ya kupeleka hoja zake na wenye mkakati wa kibalagha.
Lakini hata hivyo uchanganuzi wa kibalagha, wa kila aina, una mipaka yake. Mathalani unapoeleza tu mitindo ya ufasaha, mara nyingi matokeo yake yanahusu mitindo tu. Nao uchanganuzi huo ni hasa wa kisinkronia; hivyo hauwezi kudai kuwa mbinu yenye kujitegemea na kujitosheleza. Tena unapoelekezwa kwa matini za kibiblia maswali mengi yanazuka: Je, watunzi wa hizo matini walikuwa washiriki wa matabaka yenye elimu ya juu? Je, kwa kiasi gani hawa walishikilia sheria za balagha ili kuyatunga maandishi yao? Je, ni balagha ipi inayofaa zaidi kusudi kulichambua andiko fulani: ile ya kigiriki-kilatini au ile ya kisemiti? Je, hatuingizwi katika hatari ya kuzihusisha baadhi ya matini za Biblia na miundo ya kibalagha yenye hali ya juu mno? Lakini, maswali haya – na mengine tena – yasije yakatukatisha tamaa tusitumie aina hiyo ya uchanganuzi; ila tu yatuhimiza tuitumie kwa upambanuzi mnyofu.
Ufafanuzi wa kisimulizi unatoa mbinu ya kufahamu
na kuwasilisha ujumbe wa Biblia ambayo inahusiana na mtindo wa usimulizi na wa
ushuhuda. Na mtindo huo ni namna ya msingi ya mawasiliano kati ya watu, hata
katika Maandiko Matakatifu. Maana Agano la Kale lazieleza habari za historia ya
wokovu ambayo masimulizi yake yenye nguvu yanakuwa kiini cha ungamo la imani,
cha liturujia na cha katekesi (taz. Zab 78:3-4; Kut 12:24-27; Kum 6:20-25;
26:5-10). Kwa upande wake, tangazo la kerigma ya kikristo lina
ndani yake masimulizi ya mfululizo ya maisha, ya kifo na ya ufufuko wa Yesu
Kristo; ndiyo matukio ambayo Injili hutusimulia kinaganaga. Katekesi nayo
yaelezwa kwa mtindo wa masimulizi (taz. 1Kor 11:23-25).
Mintarafu njia ya kisimulizi inafaa kutofautisha
kati ya mbinu za uchanganuzi na tafakuri ya kitheolojia.
Siku hizi zinatolewa mbinu nyingi za
uchanganuzi. Baadhi yake huanzia toka utafiti wa mitindo ya masimulizi
ya kale. Nyingine zaasisika katika aina hii au ile ya “naratolojia” (elimu
simulizi) ya nyakati zetu, ambayo yaweza kuhusiana kwa namna fulani na
semiotiki. Uchanganuzi wa kisimulizi huyazingatia kwa makini katika matini
mambo yahusuyo msuko wa historia, watendaji na mtazamo wa msimulizi. Aidha
huichunguza namna historia inavyosimuliwa ili kumnasa msomaji akaingie katika
“ulimwengu wa masimulizi” na katika mfumo wake wa tunu.
Mbinu nyingi zinatofautisha baina ya “mwandishi
halisi” na “mwandishi mdokezwa”, “msomaji halisi” na “msomaji mdokezwa”.
“Mwandishi halisi” ndiye mtu aliyeyatunga masimulizi. Na kwa jina “mwandishi
mdokezwa” inamaanishwa taswira ya mwandishi ambayo inadokezwa hatua kwa hatua
wakati wa kusoma (yaani, mwenye utamaduni wake, hulka yake, maelekeo yake,
imani yake, n.k.). Tena huitwa “msomaji halisi” kila mtu aikaribiaye matini,
kuanzia walengwa wa asili walioisoma au kuisikia, hadi wasomaji au wasikilizaji
wa siku za leo. Na kwa jina “msomaji mdokezwa” humaanishwa yule anayekusudiwa
na matini yenyewe au ambaye anaathiriwa nayo; yaani yule mwenye uwezo wa
kutumia akili na hisia zake ili kuingia katika ulimwengu wa masimulizi, na hapo
kuitikia kwa ile namna iliyonuiwa na mwandishi halisi kwa njia ya mwandishi
mdokezwa.
Hivyo basi, matini fulani inaendelea kuwaathiri
wasomaji kwa kiasi wasomaji halisi (k.m. sisi wenyewe tuishio mwishoni mwa
karne ya ishirini) wanachoweza kujifananisha na msomaji mdokezwa. Wajibu
mojawapo wa msingi wa ufafanuzi ni kuirahisisha kazi hiyo ya kujifananisha.
Uchanganuzi wa kisimulizi unaandamana na namna
mpya ya kuutathmini uzito wa matini. Yaani, wakati mbinu ya
kihistoria-kiuhakiki inazingatia matini kama “dirisha” liwezeshalo kutazama na
kuhoji kuhusu muhula fulani (si tu mintarafu matukio yanayosimuliwa, bali pia
kuhusu hali ya jumuiya ambayo kwayo yenyewe yalisimuliwa); kumbe, kwa njia ya
uchanganuzi wa kisimulizi husisitizwa kuwa matini ni pia kama “kioo”, yaani
inaonyesha picha fulani ya ulimwengu – “ulimwengu wa masimulizi” – yenye
kuiathiri mitazamo ya msomaji na kumfanya azishike tunu kadhaa kuliko nyingine.
Na tafakuri ya kitheolojia imejiambatanisha
na aina hiyo ya mtaala, iliyo ya kifasihi tu, kwa sababu imezingatiwa kuwa
Maandiko Matakatifu yana maumbile ya masimulizi, na hivyo ya ushuhuda pia; na
jambo hilo lina uzito wake kwa ajili ya kuishikilia imani. Tena, toka mbinu hii
imechimbuka hemenetiki inayolenga katika utendaji na uchungaji. Na hiyo ni njia
mojawapo iliyoshikwa ili kuzuia matini iliyovuviwa (ya Biblia) isishushwe
katika hali ya kutazamwa tu kama mkusanyo wa hoja za kitheolojia zinazoelezwa
mara nyingi kadiri ya mitindo na lugha isivyotokana na Maandiko. Hivyo,
ufafanuzi wa kisimulizi unapewa wajibu – katika mazingira mapya ya kihistoria –
wa kuzirudishia heshima yake namna za mawasiliano na uashiriaji zilizo mahsusi
za masimulizi ya kibiblia. Nalo kwa lengo la kuifungulia mlango mpana zaidi
nguvu ya Biblia kwa ajili ya wokovu. Unasisitizwa pia ulazima wa “kuusimulia
wokovu” (mandhari ya “kitaarifa” ya simulizi) na tena wa “kusimulia kwa
minajili ya wokovu” (mandhari ya “kiutendaji”). Maana simulizi la kibiblia lina
ndani yake – ama kwa wazi ama sivyo, kadiri ya nafasi mbalimbali – mwito kwa
msomaji uhusuo maisha yake yote.
Kwa ajili ya ufafanuzi wa Biblia, uchanganuzi wa
kisimulizi ni msaada wazi, kwa sababu unawiana na maumbile ya kisimulizi ya
sehemu nyingi za matini ya Biblia. Hivyo, uchanganuzi huo unaweza kuchangia
kuwezesha kupita toka maana ya matini ndani ya mazingira yake ya kihistoria –
inavyopatikana kadiri ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki – hadi kufikia maana
iliyo nayo kwa msomaji wa siku za leo; kazi ambayo mara nyingi ni ngumu.
Lakini, kwa upande mwingine, kutofautisha kati ya “mwandishi halisi” na
“mwandishi mdokezwa” kunaongeza ugumu wa masuala ya ufasiri.
Aidha, uchanganuzi wa kisimulizi hauwezi tu
kutumia taratibu zile zilizokwisha kupangwa ili kuzifasiri matini za Biblia;
bali unapaswa kufanya bidii kusudi ujilinganishe na upekee wa kila matini.
Mkabala (approach) wake wa kisinkronia unadai kukamilishwa na mitaala ya
kidiakronia. Lakini, kwa upande mwingine, uchanganuzi huo unapaswa
kujitahadhari na mwelekeo wowote ule ukanyao kila tengenezo la kimafundisho la
yale yaliyomo katika masimulizi ya Biblia. Ungefanya hivyo ungepingana na
mapokeo ya kibiblia yenyewe ambayo yanalitenda tengenezo la namna hii; tena
ungepingana na mapokeo ya kikanisa yaliyoendelea kuitumia njia hii. Na hatimaye
inafaa kusisitiza kuwa haiwezekani kuitazama ile nguvu ambayo Neno la Mungu –
katika umbo lake la kisimulizi – linayo juu ya maisha ya watu kama kigezo
kitoshacho cha kwamba limefahamika barabara.
Kati ya mbinu ziitwazo za kisinkronia, yaani
zilizomakinika juu ya utafiti wa matini ya Biblia kama ilivyo katika hatua yake
ya mwisho, upo pia uchanganuzi wa kisemiotiki; nao tangu miaka ishirini
iliyopita umejiendeleza sana katika mazingira fulani ya kitaaluma. Mwanzoni
mbinu hii iliitwa kwa neno la jumla “Umuundo” (Structuralism), na
inaweza kujisifia kumhesabu kama mwasisi wake mwanaisimu mswisi Ferdinand de
Saussure. Huyo, mwanzoni mwa karne hii alitengeneza nadharia ambayo kwayo kila
lugha ni mfumo wa mahusiano yanayofuata kanuni maalumu. Wanaisimu wengi na
wasomi wa fani za kifasihi walichangia sana kwa maendeleo ya mbinu hii. Walio
wengi zaidi wa wasomi wa Biblia wanaoitumia semiotiki kwa mtaala wa Biblia
hurejea kwa Algirdas J. Greimas na kwa Shule ya Paris aliyoiasisi mwenyewe.
Njia au mbinu nyinginezo za kufanana na hiyo ya kisemiotiki, ambazo zimeasisika
katika isimu ya kisasa, zinajiendeleza mahali pengine. Hapo tutaeleza na
kuichambua kifupi mbinu ya Greimas.
Semiotiki ina misingi yake juu ya kanuni au
dhanio hizi tatu zilizo kuu:
Kanuni ya kujitimiliza (immanence): kila matini
inaunda umoja wa uashiriaji; na uchanganuzi huzingatia matini yote, lakini
matini hiyo tu; wala hauzitafuti data nyingine nje yake, kama vile mwandishi,
walengwa, matukio yasimuliwayo, na historia ya uhariri.
Kanuni ya muundo wa maana: hakuna maana nyingine ya matini isipokuwa kwa
njia ya mahusiano na katika mahusiano, na hasa uhusiano wa utofauti; hivyo
uchanganuzi wa matini ni juhudi ya kuugundua mfumo wa mahusiano yaliyopo katika
matini (k.m. uhusiano wa upinzani, wa uthibitisho, n.k.). Na kutokana na mfumo
huo maana ya matini inajengwa.
Kanuni ya sarufi ya matini: kila matini yafuata sarufi maalum, yaani
utaratibu fulani wa kanuni na miundo; na katika ujumla wa sentensi tunaouita
usemi (discourse) kuna viwango mbalimbali, kila kimoja kikiwa na sarufi
yake.
Maudhui ya jumla ya matini huweza kuchanganuliwa
katika viwango vitatu tofauti:
Kiwango cha kisimulizi. Katika masimulizi yanachunguzwa mabadiliko
yanayopeleka tokea hali ya mwanzo hadi ya mwisho. Na ndani ya mwendo huo wa
kisimulizi, uchanganuzi unajaribu kuzigundua awamu mbalimbali zinazofuatana
kimantiki kati yake na ambazo zinapigisha hatua za mabadiliko toka hali moja
hadi nyingine. Aidha, katika kila awamu yanaelezwa mahusiano kati ya “dhima”
zilizo nazo baadhi ya “atanti” (au “wahusika”) ambazo zasababisha hali mbalimbali
na mabadiliko yake.
Kiwango cha kiusemi. Uchanganuzi huo una vitendo vitatu: (a) kugundua
na kuziainisha tamathali, yaani elementi za uashiriaji wa matini (yaani
watendaji, nyakati, na mahali); (b) kuueleza mwendo inaoufuata kila tamathali
katika matini, ili kuelewa namna matini inavyoitumia; (c) kuzitafiti thamani za
kidhamira za tamathali. Na kitendo hicho cha mwisho kinalenga katika kutambua
ni “kwa ajili ya nini” (=thamani) tamathali hizo zinafuata mwendo fulani katika
matini.
Kiwango cha kimantiki-kisemantiki: Ni kiwango kiitwacho cha kina; tena ni cha
kidhahania zaidi. Nacho hutokana na dhana ya kwamba nyuma ya miundo ya
kisimulizi na kiusemi ya kila usemi hufichama fani za kimantiki na viashiria.
Katika kiwango hicho uchanganuzi unashughulikia kuieleza mantiki inayoratibisha
miundo ya msingi ya miendo ya kisimulizi na kitamathali ya matini. Kwa
kuitekeleza kazi hiyo yanatumika maarifa yaitwayo “mraba wa kisemiotiki”, yaani
tamathali inayotumia mahusiano baina ya misamiati miwili iliyo “kinyume” kati
yake na misamiati miwili “inayopingana” (k.m. nyeupe na nyeusi; nyeupe na si
nyeupe; nyeusi na si nyeusi).
Wanadharia wa mbinu ya kisemiotiki hawamalizi
kuleta maendeleo katika mbinu hii. Na tafiti za kisasa zinahusu hasa utamkaji (enunciation) na
mwingiliano matini (intertextuality). Mwanzoni mbinu hii
ilitumika kwa matini za kisimulizi za Maandiko – na hapo ni rahisi zaidi;
lakini siku hizi inazidi kutumika pia kwa aina nyingine za semi za kibiblia.
Maelezo ya hapo juu mintarafu semiotiki, na hasa
kuhusu dhanio zake, yanahisisha michango na pia mipaka ya
mbinu hii. Maana, yenyewe inakazia kwamba kila matini ya Biblia ina mshikamano
ndani yake ambao unafuata taratibu maalum za kiisimu; hivyo semiotiki
inachangia katika ufahamu wetu wa Biblia, iliyo neno la Mungu lielezwalo kwa
lugha ya kibinadamu.
Semiotiki yaweza kutumika kwa mtaala wa
kibiblia, ila kwa sharti ya kwamba mbinu hii itenganishwe na dhanio
zilizoendelezwa katika falsafa ya Umuundo, yaani ukanushaji wa wahusika na wa
elementi mbalimbali zipatikanazo nje ya matini. Biblia ni Neno juu ya uhalisi,
ambalo Mungu amelitamka katika historia, na ambalo anatuelekezea leo kwa njia
ya waandishi wa kibinadamu. Njia ya kisemiotiki haina budi kuwa wazi mbele ya
historia: kwanza historia ya watendaji katika matini, na baadaye historia ya
waandishi wake na wasomaji wake. Hivyo kwa wale wanaoutumia uchanganuzi wa
kisemiotiki hatari ni kubwa ya kukwama katika utafiti wa nje wa maudhui, lakini
pasipo kuukamata ujumbe wa matini.
Uchanganuzi wa kisemiotiki unaweza kuiamsha
katika wakristo hamu ya kuzichunguza matini za Biblia na kuvumbua baadhi ya
maana zake bila ya kuwa na maarifa yote ya kihistoria yanayohusu utungaji wa
matini na mazingira yake ya kijamii-kiutamaduni. Ila uchanganuzi huo usipotee
katika vificho vya lugha yenye utata; na tena ufundishwe kwa namna iliyo rahisi
katika vipengele vyake vya msingi. Kwa jinsi hiyo unaweza kufaa katika kazi
yenyewe ya kichungaji, ili pia watu wasio na utaalamu wa pekee wapate kwa namna
fulani kujitwalia Maandiko Matakatifu katika maisha yao.
Mbinu za kifasihi tulizozieleza huhitilafiana na
mbinu ya kihistoria-kiuhakiki kwa sababu humakinika zaidi katika umoja uliomo
ndani ya matini zinazochunguzwa; lakini hata hivyo hazitoshelezi kwa ajili ya
ufasiri wa Biblia, kwa maana hulizingatia kila andiko kwa lenyewe. Sasa, Biblia
haijidhihirishi kama mkusanyo wa matini zisizo na uhusiano wowote kati yake,
bali kama jumla ya shuhuda za Mapokeo makuu yaleyale. Ili kuiridhisha kwa
ukamilifu mada ya mtaala wake, ufafanuzi wa kibiblia hauna budi ulitilie
maanani jambo hilo. Nao ndio mtazamo uliotumika na njia mbalimbali
zilizojitokeza hivi karibuni.
Njia ya “kikanoni” ilizaliwa mnamo miaka
ishirini iliyopita huko Marekani; asili yake ilikuwa pale ilipogunduliwa kwamba
mbinu ya kihistoria-kiuhakiki mara nyingine inashindwa kukifikia kiwango cha
kitheolojia katika hatima zake. Hivyo, njia hii inanuia kuufikisha ufasiri
kwenye hatua ya kushikilia wajibu wake wa kitheolojia, kuanzia na fremu wazi la
imani, yaani, Biblia katika umoja wake.
Ili kutekeleza wajibu huo inafasiri kila matini
ya Biblia katika mwanga wa kanoni ya Maandiko, yaani wa Biblia ipokelewayo na
jumuiya ya waamini kama kanuni ya imani. Inajaribu kuingiza kila matini ndani
ya mpango ule mmoja wa Mungu, kwa minajili ya kuufikia uhusisho (actualization)
wa Maandiko Matakatifu katika nyakati zetu. Ila njia hii haijidai kuchukua
nafasi ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki, bali inatarajia kuikamilisha.
Mitazamo miwili tofauti imetolewa:
Brevard S. Childs anazingatia hasa matini katika
sura yake ya kikanoni ya mwisho (kitabu au mkusanyo), iliyokubalika na jumuiya
kama mamlaka ili kueleza imani ya jumuiya yenyewe na kuyaelekeza maisha yake.
Kumbe, James A. Sanders, kuliko kuzingatia sura
hiyo ya mwisho ya matini iliyokubalika, anatilia maanani hasa “mchakato wa
kikanoni” wa Maandiko, au kukua kwake hatua kwa hatua, ambayo jumuiya ya
waamini imeyakubali kuwa na mamlaka ya kikanuni. Uchambuzi wa kiuhakiki wa
mchakato huo unachunguza jinsi mapokeo ya kale yalivyotumika upya katika
mazingira mapya, kabla hayajaunda umoja wa kudumu, lakini unaoweza kukamilishwa
tena, wenye mshikamano, na unaopatanisha yale yasiyoafikiana. Na kutoka kwake
jumuiya ya waamini huchota kitambulisho chake. Wakati wa mchakato huo,
yalitumika maarifa ya kihemenetiki ambayo bado yanatumika, hata baada ya kuweka
kanoni rasmi; mara nyingi maarifa hayo yanaingia katika utanzu wa “kimidrashi”;
nayo yanalenga katika kuzilinganisha na wakati huu matini za Biblia na kuusaidia
mwingiliano wa kudumu baina ya jumuiya na Maandiko yake, yakitafiti ufasiri
unaokusudia kuyafanya mapokeo yawiane na wakati huo.
Njia ya kikanoni kwa haki inapinga uthamini wa
kupita kiasi wa kile kinachodhaniwa kuwa cha asili na cha kale kana kwamba chenyewe
tu ni halisi. Kumbe Maandiko yaliyovuviwa ndiyo yale ambayo Kanisa limeyakubali
kama kanuni ya imani yake. Na kuhusu hilo, huwezekana kuitilia mkazo hali ya
mwisho ambayo kila kitabu kinayo siku hizi, na pia umoja ambao vitabu vinauunda
kwa pamoja kama kanoni. Kila kitabu kinakuwa cha Biblia katika mwanga tu wa
kanoni nzima.
Jumuiya ya waamini ndiyo mazingira yanayofaa kwa
ufasiri wa matini za kikanoni. Imani na Roho Mtakatifu hutajirisha ufafanuzi
ndani ya jumuiya yenyewe; na hatimaye mamlaka ya Kanisa, yafanyayo kazi kwa
huduma ya jumuiya, lazima yahakikishe kuwa ufasiri ni mwaminifu kwa mapokeo
makuu yaliyotunga matini (taz. Dei Verbum, 10).
Njia ya kikanoni inapambana na matatizo mengi,
hasa inapojaribu kueleza “mchakato wa kikanoni”. Je, kutokana na nini
yawezekana kusema kuwa matini fulani ni ya kikanoni? Inaonekana kwamba
yawezekana mara tu jumuiya inapoipa mamlaka ya kikanuni, hata kabla matini
yenyewe haijafikia hali yake ya mwisho. Hivyo, hemenetiki ya “kikanoni” inaweza
kuzungumziwa tangu pale ambapo marudio ya mapokeo, yanayofanyika kwa kuzingatia
mandhari mpya za mazingira (ya kidini, kiutamaduni, kitheolojia), yanatunza
umoja wa ujumbe. Lakini hapo swali linazuka: Je, mchakato wa ufasiri ulioleta
kwenye uundaji wa kanoni unapaswa kukubalika kama kanuni ya ufasiri wa Maandiko
hadi siku za leo?
Kwa upande mwingine, mahusiano changamano baina
ya kanoni ya kiyahudi ya Maandiko na kanoni ya kikristo yanazusha masuala mengi
mintarafu ufasiri. Kanisa la kikristo limepokea kama “Agano la Kale” maandishi
yaliyokuwa na mamlaka katika jumuiya ya kiyahudi-kiyunani, lakini baadhi yake
hayapo katika Biblia ya kiyahudi, au yapo lakini kwa tungo tofauti. Kwa
hiyo kongoo (corpus) ni tofauti. Ndiyo
maana ufasiri wa kikanoni hauwezi kuwa sawa kwa vile kila matini lazima isomwe
kwa kuhusiana na mshikamano wa kongoo nzima. Lakini, zaidi ya hayo, Kanisa
lasoma Agano la Kale katika mwanga wa tukio la kipasaka – yaani kifo na ufufuko
wa Yesu Kristo –, ambayo linaleta kitu kilicho kipya kabisa na kinachotimiliza
na kuikamilisha maana ya Maandiko kwa mamlaka yake yenye enzi (taz. Dei Verbum, 4). Na
upambanuzi huo mpya wa maana ya maandiko ni sehemu halisi ya imani ya kikristo.
Lakini hauwezi kubatilisha ufasiri wa kikanoni ulioitangulia Pasaka ya
kikristo, kwa sababu ni lazima kuiheshimu kila hatua ya historia ya wokovu.
Kwani kubatilisha uzito wa maana ya Agano la Kale kungekuwa kung’oa mizizi ya
Agano Jipya kutoka katika historia.
Agano la Kale lilichukua sura yake ya mwisho
katika mazingira ya Uyahudi (Judaism) wa karne nne ama tano kabla ya
nyakati za kikristo. Nayo yalikuwa pia mazingira ya asili ya Agano Jipya na ya
Kanisa changa. Wingi wa uchunguzi kuhusu historia ya kale ya Uyahudi – na hasa
tafiti zilizochochewa na uvumbuzi wa Kumrani – umeonyesha mchangamano wa
ulimwengu wa kiyahudi, katika nchi ya Israeli na katika Mtawanyiko (diaspora), katika
kipindi hicho.
Ufasiri wa Biblia umeasilika katika mazingira
haya. Ushuhuda mmojawapo wa kale zaidi wa ufasiri wa kiyahudi wa Biblia ni
tafsiri yake ya Kigiriki iitwayo ya Septuajinta. Kadhalika targumim za
Kiaramu ndio ushuhuda mwingine wa jitihada ileile iliyoendelezwa hadi siku za
leo, kwa kulimbikiza mkusanyo wa ajabu wa mbinu za kitaaluma kwa ajili ya
uhifadhi wa matini ya Agano la Kale na ufafanuzi wa maana ya matini za Biblia.
Tangu mwanzo wafafanuzi wa kikristo walio bora, kuanzia na Orijene na Mt.
Yeronimo, walijitahidi kupata faida kutokana na elimu ya kibiblia ya kiyahudi kwa
minajili ya ufahamu ulio mzuri zaidi wa Maandiko. Na wafafanuzi wengi wa
nyakati zetu wanafuata mfano wao.
Mapokeo ya kale ya kiyahudi yanatusaidia hasa
kuijua Septuajinta, iliyo Biblia ya kiyahudi, na ambayo imekuwa baadaye sehemu
ya mwanzo ya Biblia ya kikristo, walau katika karne nne za kwanza za Kanisa, na
huko Mashariki hadi siku za leo. Aidha, maandishi ya kiyahudi yaliyo nje ya
kanoni na yaitwayo “apokrifa” au “ya kati ya maagano”, yametufikia kwa wingi na
ya aina aina; hata hayo ni chemchemi muhimu kwa ufasiri wa Agano Jipya. Mbinu
za kifafanuzi zilizotumika na Uyahudi wa mielekeo mbalimbali, zinapatikana
katika Agano la Kale lenyewe, kwa mfano katika vitabu vya Mambo ya Nyakati kwa
kuhusiana na vitabu vya Wafalme; pia katika Agano Jipya, mathalani katika
baadhi ya hoja za Mt. Paulo kuhusu Maandiko. Utofauti wa tanzu (mifano,
istiari, diwani na koja, kusoma upya (relectures), mbinu
za “pesher”, namna ya kuunganisha matini ambazo vinginevyo
zingekuwa za aina mbalimbali, zaburi na tenzi, maono, funuo na ndoto, maandishi
ya kihekima) umo katika Agano la Kale, na Agano Jipya pia, kama vile katika
fasihi ya mazingira yoyote ya kiyahudi kabla na baada ya wakati wa Yesu. Targumim na Midrashim ni
namna ya kuhutubia na kufasiri Biblia katika sekta nyingi za Uyahudi wa karne
za mwanzoni.
Wafafanuzi walio wengi wa Agano la Kale
wanatafuta msaada kwa wafasiri, wanasarufi na wanamsamiati wa kiyahudi wa Enzi
ya Kati (mediaeval) na wa baadaye ili kuzielewa sehemu za
kizakiza ama maneno yanayotumika kwa nadra au mara moja tu. Na siku hizi katika
majadiliano ya kifafanuzi marejeo kwa maandishi hayo ya kiyahudi yanaonekana
kuwa mengi zaidi kuliko hapo nyuma.
Utajiri wa elimu ya kiyahudi uliowekwa
kuitumikia Biblia, tangu asili yake wakati wa kale hadi siku za leo, ni msaada
kati ya ile yenye kipaumbele kwa ajili ya ufafanuzi wa Maagano yote mawili, ila
kwa sharti ya kuutumia kwa upambanuzi mzuri. Uyahudi wa kale ulikuwa na mitindo
mbalimbali. Mtindo wa kifarisayo, ambao baadaye ulishinda kati ya marabi,
haukuwa mtindo pekee. Matini za kale za kiyahudi zilienea katika muda wa karne
kadhaa; hivyo, ni muhimu kuzipanga kadiri ya nyakati zake kabla ya kuanza
kuzilinganisha. Lakini hasa mazingira ya jumla ya jumuiya hizi mbili, yaani ya
kiyahudi na ya kikristo, ni tofauti kabisa: kwa namna nyingi mbalimbali dini ya
kiyahudi inaainisha taifa fulani na pia utendaji wa kimaadili kutokana na
andiko lililofunuliwa na Mungu na kutokana na mapokeo simulizi; kumbe,
kinachokusanya jumuiya ya kikristo ni imani katika Bwana Yesu aliyekufa na
kufufuka, na ambaye sasa yu hai, ndiye Masiya na Mwana wa Mungu. Basi, kuhusu
ufasiri wa Maandiko vyanzo hivi viwili tofauti vinaleta mazingira mawili ambayo
ni tofauti kabisa, ijapo vipengele vinavyoelekeana na kufanana ni vingi.
Njia hii ina misingi yake juu ya kanuni mbili:
a) matini inapata kuwa kazi ya kifasihi pindi tu inapokutana na wasomaji ambao
wanaihuisha kwa kuitwaa; b) kuitwaa huko kwa matini kunaweza kuwa tendo la mtu
binafsi au la kijumuiya; tena ni tendo linaloweza kutekelezwa katika nyanja
mbalimbali (wa kifasihi, kisanaa, kitheolojia, kiroho, kitawa); na hatimaye
kunachangia katika kufanya matini yenyewe ieleweke vizuri zaidi.
Ijapokuwa njia hii ilikuwa inafahamika kwa kiasi
fulani tangu nyakati za kale, siku hizi imejiendeleza zaidi kati ya miaka 1960
na 1970 katika mitaala ya kifasihi, wakati uhakiki ulipojihusisha kuchunguza
mahusiano kati ya matini na wasomaji wake. Ufafanuzi wa kibiblia ulikuwa hauna
budi kufaidika kutokana na utafiti huo, na zaidi kufuatana na kwamba hemenetiki
ya kifalsafa kwa upande wake ilikuwa ikisisitiza ya kuwa ni lazima umbali
fulani uwepo baina ya maandishi na mwandishi wake, kama vile kati ya maandishi
na wasomaji wake. Kadiri ya mtazamo huo, ilianza kuingizwa katika kazi ya
ufasiri historia ya athari zilizoletwa na kitabu au sehemu fulani ya Maandiko
(“Wirkungsgeschichte”). Na bidii inafanyika i1i kupima
maendeleo ya ufasiri katika mtiririko wa nyakati kuhusiana na kero za wasomaji,
pia ili kutathmini umuhimu wa dhima ya mapokeo katika kuiweka wazi maana ya
matini za Biblia.
Kuhojiana kati ya matini na wasomaji wake
kunaleta mkikimkiki fulani, kwa sababu matini inawaathiri wasomaji na
kuwazushia hisia kadhaa; tena inasikiza mwaliko wake unaoitikiwa nao kibinafsi
au kijumuiya. Naye msomaji kwa vyovyote si mtu aishiye peke yake, bali daima
hushiriki mazingira fulani ya kijamii, naye yumo ndani ya mapokeo fulani.
Hivyo, huikaribia matini kwa maswali yake, tena hufanya uchambuzi na
kupendekeza ufasiri wake, na hatimaye huweza kutunga maandishi mengine ama
kujishughulisha na mambo mengine yatokanayo moja kwa moja na anavyosoma yeye
Maandiko.
Mifano ya namna hii imeshakuwa mingi. Historia
ya usomaji wa Wimbo ulio Bora inatupatia ushuhuda bora; nao huonyesha jinsi
kitabu hiki kilivyopokelewa siku za Mababa wa Kanisa, au kwenye mazingira ya
kimonaki ya kilatini katika Enzi za Kati (mediaeval); au
tena kwa mtu mshiriki Mungu (mystical writer) kama Mt. Yohane wa
Msalaba. Hivyo, njia hii inatuwezesha kuvumbua kiundani zaidi vipengele vyote
vya maana za andiko hilo. Kadhalika, mintarafu Agano Jipya yawezekana na yafaa
kuiangaza maana ya kifungu fulani (kwa mfano, cha kijana tajiri wa Mt 19:16-26)
kwa kuonyesha wingi wa matunda kilichouleta katika mtiririko wa historia ya
Kanisa.
Lakini, historia huthibitisha pia kuwepo kwa
mitindo ya ufasiri yenye kupotosha na ya uongo, iletayo matokeo mabaya na
ambayo ilisababisha, kwa mfano, madhulumu ya Wayahudi, au ubaguzi wa kikabila,
au mauzauza za kimilenia. Hivyo basi, huonekana kwamba njia hii haiwezi kuwa
fani inayojitegemea, bali ambayo hudai upambanuzi. Ni lazima kujitahadhari na
tabia ya kuibagua awamu moja au nyingine ya historia ya athari ya matini fulani
na kuiweka kama kanuni pekee ya ufasiri wake.
Ili kujishirikisha, Neno la Mungu limetia mizizi
yake ndani ya maisha ya jumuiya za kibinadamu (taz. YbS 24:12) na kujipasulia
njia katika mielekeo ya kisaikolojia ya watu mbalimbali waliotunga maandishi ya
Biblia. Katika hilo yatokana kwamba sayansi za kibinadamu – hasa sosholojia,
anthropolojia na saikolojia – zaweza kuchangia kwa ajili ya ufahamu bora zaidi
wa mandhari kadhaa za matini. Walakini yafaa kukumbuka kwamba ziko shule
mbalimbali, zenye kuhitilafiana kwa vikubwa kuhusu maumbile yenyewe ya sayansi
hizo. Ikiisha semwa hivyo, basi wafafanuzi sio wachache wamenufaika hivi
karibuni kutokana na aina hiyo ya utafiti.
Matini za kidini zinafungamana na jamii zile
zilipoasilika. Ni wazi kwamba kauli hiyo yazihusu pia matini za Biblia. Hivyo,
uchambuzi wa kiuhakiki wa Biblia hudai ujuzi ulio kamili zaidi, iwezekanavyo,
wa desturi za kijamii zilizokuwa kawaida ya mazingira ambamo mapokeo ya
kibiblia yalitengenezwa. Na aina hiyo ya taarifa za kijamii-kihistoria haina
budi kukamilishwa kwa maelezo sahihi ya kisosholojia ambayo, kwa vyovyote,
yatapaswa kufasiri kisayansi uzito wa mazingira ya kijamii ya maisha.
Katika historia ya ufafanuzi, tangu muda mrefu
mtazamo wa kisosholojia umepata nafasi yake; na ushuhuda wa nafasi hiyo ndio
mkazo ambao uchambuzi wa kiuhakiki wa fani (“Formgeschichte”) umeyatilia
mazingira ya asili ya matini (“Sitz im Leben”): inakubalika kuwa mapokeo
ya kibiblia yanabeba athari ya mazingira ya kijamii-kiutamaduni yaliyoyafikisha
kwetu. Katika miaka thelathini ya kwanza ya karne ya ishirini, Shule ya Chicago
ilichunguza hali ya kisosholojia-kihistoria ya Ukristo wa mwanzoni; na hivyo
iliutilia uhakiki wa kihistoria hamasa maridhawa katika mwelekeo huo. Na
hatimaye katika miaka hiyo ishirini ya mwisho (1970-1990) njia ya kisosholojia
imekuwa sehemu husika ya ufafanuzi wa matini za Biblia.
Mengi ndiyo maswali yanayozuka katika uwanja huo
kwa ufafanuzi wa Agano la Kale. Mathalani, ni lazima kujiuliza ni ipi mitindo
mbalimbali ya mifumo ya kijamii na kidini iliyofahamika na Israeli katika
mwenendo wa historia yake. Ukizingatiwa muhula uliotangulia uundaji wa dola
kamili, je yawezekana kuwa mtindo wa kiethnolojia wa jamii iliyogawanyika
kikabila na isiyo na uongozi kamili uwe msingi maridhawa kwa kujenga chochote?
Je, imekuwaje kuwa shirikisho la makabila mbalimbali yasiyo na mshikamano imara
lipate kuwa dola yenye mfumo wa kiufalme, na tokea hapo tena lipate kuufikia
uundaji wa jumuiya inayoasilika tu katika vifungo vya kidini na kinasaba? Je,
ni mageuzi yapi ya kiuchumi, kijeshi au ya namna nyingine yoyote ile
yaliyoletwa katika muundo wa jamii, kutokana na kuyaunganisha makabila yote
chini ya mamlaka moja ya kisiasa na kidini, hadi kuufikia mfumo wa kiufalme?
Je, uchunguzi wa kanuni za kimwenendo zilizokuwepo katika Mashariki ya kale na
katika Israeli hausaidii kuzielewa Amri Kumi (za Mungu) kwa manufaa zaidi
kuliko majaribio ya uchanganuzi wa kifasihi pekee yanayotaka kuithibitisha
matini ya asili?
Kuhusu ufafanuzi wa Agano Jipya ni wazi kwamba
maswali ni tofauti. Tunayataja baadhi yake: ili kueleza mtindo wa maisha ya
Yesu na wanafunzi wake kabla ya Pasaka, je, yaweza kupewa uzito gani nadharia
ya “uamsho wa kikarama” (charismatic movement) wa watu wenye
kutembeatembea, wasio na makao kamili, wala familia, wala mali? Tena kutokana
na wito wa Yesu wa kuzifuata nyayo zake, je, kulikuwa na uwiano halisi baina ya
tabia ya Yesu ya kuacha kabisa yote na tabia ya washiriki wa uamsho wa kikristo
baada ya Pasaka, katika mazingira mbalimbali ya Ukristo wa mwanzoni? Na
hatimaye, je, tuna habari gani kuhusu muundo wa kijamii wa jumuiya
zilizoanzishwa na Mt. Paulo, kwa kuuzingatia kwa kila moja utamaduni ulioenea
katika miji zilimoishi?
Kwa ujumla, njia ya kisosholojia inailetea kazi
ya ufafanuzi mtazamo ulio mpana zaidi na kutoa michango mingi mizuri. Ujuzi wa
data za kisosholojia, zinazosaidia kuelewesha mwendo wa kiuchumi, kiutamaduni
na kidini wa mazingira ya Biblia, ni wa lazima katika fani ya uhakiki wa
kihistoria. Wajibu unaoukabili ufafanuzi, wa kuzingatia kwa makini ushuhuda wa
imani ya Kanisa la kitume, hauwezi kutekelezwa hadi mwisho na kwa utaratibu
sahihi pasipo utafiti wa kisayansi kufanyika, ambao uchunguze mahusiano ya
ndani kati ya matini za Agano Jipya na maisha ya kijamii ya Kanisa la mwanzoni.
Matumizi ya mitindo inayotolewa na sayansi ya kisosholojia yanawapatia wasomi
wa historia wanaozichunguza nyakati za Biblia uwezo mkubwa wa kutengeneza upya
mbinu zao; ila mitindo itumiwayo haina budi kulinganishwa na masuala
yanayopelelezwa.
Na hapo yafaa kusisitiza pia hatari zilizopo
katika njia ya kisosholojia pindi inapotumika katika ufafanuzi. Kwa kuwa kazi
ya sosholojia ni kuchunguza jamii zilizo hai, basi shida lazima itokee pale
mbinu zake zinapodaiwa kutumika kwa kuchunguza mazingira ya kihistoria yahusuyo
nyakati za kale. Maana matini za Biblia na za nje ya Biblia hazitupatii habari
na hati za kutosha ili kutoa picha ya jumla ya jamii za nyakati hizo. Aidha,
mbinu ya kisosholojia inatilia maanani zaidi vipengele vihusuvyo uchumi na
taasisi za maisha ya kibinadamu, kuliko masuala yanayoelekea maisha ya
kibinafsi na ya kidini.
Njia ichunguzayo matini za Biblia kwa kutumia
tafiti za anthropolojia ya kiutamaduni inahusiana kiundani na njia ya
kisosholojia. Upambanuzi baina ya njia hizo mbili waweza kufanyika
yakizingatiwa kwa wakati mmoja masuala mbalimbali, kama vile uelekeo wa njia
hizo, mbinu zake na vipengele vya maisha vinavyovuta zaidi kila moja ya njia
hizo. Maana, kwa upande mmoja, njia ya kisosholojia – tulivyosema hapo juu –
inachunguza hususan vipengele vihusuvyo uchumi na taasisi; kwa upande mwingine,
njia ya kianthropolojia inajishughulisha na jumla ya vipengele vingine vingi
vinavyoakisiwa katika lugha, sanaa na dini; lakini pia katika mavazi, mapambo,
sherehe, dua, visasili na hadithi za kale, ngano na kila chote kihusucho
ethnografia.
Aghalabu, anthropolojia ya kiutamaduni inajaribu
kuzieleza sifa bainifu za watu wa aina mbalimbali katika mazingira yao ya
kijamii – kama vile, k.m., “mtu wa kimediterania” –; na kazi hiyo inadai
utafiti mintarafu mazingira ya shambani au mjini, na pia kuzingatia tunu
zinazokubalika na jamii yenyewe (heshima na aibu, siri, uaminifu, mapokeo,
mtindo wa malezi na wa elimu); tena inadai utafiti kuhusu namna udhibiti wa kijamii
unavyotekelezwa, na hata kuzingatia mawazo yaliyoenea mintarafu familia,
nyumba, ukoo, hali ya mwanamke; na hatimaye kuzichunguza zile dhima za kijamii
zenye kupambana baina yake (bwana / mtumishi; mmilikaji / mpangaji; mfadhili /
mfadhiliwa; mwungwana / mtumwa); nayo yote bila kusahau dhana za utakatifu na
unajisi, miiko, ibada za kutoka katika hali moja hadi kuingia nyingine, uchawi,
asili ya mali, ya madaraka, ya taarifa, n.k.
Katika msingi wa masuala hayo mbalimbali
“ainisho” (typologies) na “mitindo” (models) kadhaa vinaweza
kutengenezwa, vyenye kuzihusu tamaduni nyingi.
Aina hiyo ya uchunguzi yaweza kuwa na manufaa
kwa ufasiri wa matini za Biblia, na kweli inatumika kwa kuchunguza dhana kama
ukoo na nasaba katika Agano la Kale, au ya hali ya mwanamke katika jamii ya
kiyahudi, ya athari ya ibada zihusuzo kilimo, n.k. Katika matini zinazosimulia
mafundisho ya Yesu – mathalan mifano – hata vipengere vidogo vidogo vinaweza
kuangazwa kwa msaada wa njia hiyo. Ndivyo itokeavyo pia kwa dhana kadhaa za msingi,
kama ile ya Ufalme wa Mungu, au kwa jinsi ya kujali wakati katika historia ya
wokovu, au tena kwa hatua zilizofanya Wakristo wa mwanzoni waunganike pamoja
katika jumuiya. Njia hii inawezesha kutofautisha vizuri zaidi katika ujumbe wa
kibiblia mambo yale yadumuyo, ambayo yana msingi wake katika maumbile ya
binadamu, na yale yalinganayo zaidi na masuala ya muda ya tamaduni fulani. Hata
hivyo, pia njia hii, sawa na nyingine zenye mtazamo ya pekee, haiwezi kwa
yenyewe kueleza michango maalum ya Ufunuo. Yafaa kulishika jambo hilo pindi
matokeo ya kazi yake yatathminiwapo.
Saikolojia na theolojia hazikuacha kamwe
kuzungumzana. Katika nyakati zetu, tafiti za kisaikolojia zimepanua na
kuelekezwa kwenye uchunguzi wa miundo ya kimkikimkiki ya ung’amuzi fiche (subconscious);
nazo zimeleta majaribio mapya ya ufasiri wa matini za kale, na hivyo pia za
Biblia. Vitabu vizima vimeandikwa kuhusu ufasiri wa kiudodosinafsi wa matini za
Biblia. Na majadiliano ya motomoto yamefuata: je, kwa kipimo gani na kwa
masharti yapi tafiti za kisaikolojia na kiudodosinafsi zaweza kuchangia katika
kuelewa kwa undani zaidi Maandiko Matakatifu?
Chunguzi za kisaikolojia na kiudodosinafsi
zinaleta utajiri fulani kwa ufafanuzi wa Biblia, kwa sababu kwa njia yake
matini za Biblia zaweza kueleweka vizuri zaidi kama mang’amuzi ya maisha na
kanuni za mwenendo. Inavyoeleweka wazi, dini ipo daima katika hali ya
majadiliano na ung’amuzi fiche. Tena, inashiriki kwa vikubwa katika kuzielekeza
vema ari za kibinadamu. Hatua ambazo uhakiki wa kihistoria unazipita kadiri ya
mbinu yake zinahitaji kukamilishwa kwa uchunguzi wa viwango mbalimbali vya hali
halisi iliyoelezwa katika matini. Saikolojia na udodosinafsi hujibidisha
kusonga mbele katika utafiti wa namna hiyo. Zenyewe zinafungua njia kwa ufahamu
wa Maandiko katika viwango vyake vingi, na zinasaidia kufumbua lugha ya
kibinadamu ya Ufunuo.
Saikolojia na, kwa namna nyingine, udodosinafsi
zimeleta hasa ufahamu mpya wa ishara (symbol). Lugha ya kiishara
inawezesha kueleza sehemu za mang’amuzi ya kidini ambazo hazifikiki kwa mantiki
ya kidhana tu, lakini ambazo, hata hivyo, zina thamani kuhusu suala la ukweli.
Kwa hiyo, upelelezi unaoshirikisha mbinu mbalimbali, unaoongozwa na wafafanuzi
pamoja na wanasai-kolojia au na wanaudodosinafsi, hakika unaleta manufaa yenye
misingi ya uhalisia na yanayothibitishwa katika uchungaji.
Mifano mingi ingeweza kutolewa inayoonyesha
ulazima wa juhudi ya pamoja ya wafafanuzi na wanasaikolojia: nalo kwa minajili
ya kuelewa vizuri zaidi maana ya kanuni za ibada, ya sadaka na ya miiko; tena
kwa kuieleza lugha ya kitaswira ya Biblia, maana ya kiistiari ya masimulizi ya
miujiza, na nguvu ya kidrama ya maono au ya maneno ya kiapokaliptiki. Siyo tu
suala la kulifasiri lugha ya kiishara ya Biblia, bali pia la kuielewa dhima
yake katika kulifunua fumbo na kuzusha hoja: ndipo uhalisi wenye kutisha (“numinous”)
wa Mungu unapokutana na binadamu.
Ni wazi kwamba mazungumzano kati ya ufafanuzi na
saikolojia ama udodosinafsi kwa lengo la kuifahamu vizuri zaidi Biblia lazima
yaongozwe kwa vigezo vya kiuhakiki na kuijali mipaka ya kila fani. Kwa
vyovyote, saikolojia au udodosinafsi zenye tabia ya kukana Mungu (atheistic) zisingeweza
kufasiri mambo ya imani. Saikolojia na udodosinafsi zinafaa kwa kusisitiza
upana wa uwajibikaji wa binadamu, lakini haziwezi kufuta ukweli wa dhambi na wa
wokovu. Kwa upande mwingine, inabidi kujitahadhari ili hisia binafsi za kidini
(spontaneous religiosity) zisichanganywe na ufunuo wa kibiblia; tena ili
isisahauliwe tabia ya kihistoria ya ujumbe wa Biblia ambayo inauhakikishia
ujumbe wenyewe thamani ya tukio pekee.
Aidha, tunasisitiza kwamba haiwezekani
kuuzungumzia “ufafanuzi wa kiudodosinafsi” kana kwamba ungekuwepo wa mtindo
mmoja tu. Kwa kweli, kutokana na nyanja mbalimbali za saikolojia, na kufuatana
na shule tofauti, kuna wingi wa maarifa unaoweza kuleta mwanga wa kufaa kwa
ufasiri wa kibinadamu na wa kitheolojia wa Biblia. Kuyapendelea maoni ya shule
moja tu kama yangekuwa ukweli pekee hakuyasaidii mafanikio ya juhudi
inayofanyika kwa pamoja, bali zaidi huyadhuru.
Sayansi za kibinadamu haziwezi kufungwa katika
mipaka tu ya sosholojia, anthropolojia ya kiutamaduni na saikolojia. Fani
nyingine za sayansi nazo zinaweza kufaa kwa ufasiri wa Biblia. Na katika nyanja
hizo zote ni lazima kuuheshimu utaalamu wa kila fani na pia kutambua kwamba si
rahisi mtu mmoja awe ni stadi katika ufafanuzi na wakati huohuo pia katika
sayansi hii au hiyo ya kibinadamu.
Ufasiri wa matini fulani daima hutegemea msimamo
wa mawazo wa wasomaji wake na kero zao. Hao wanazingatia hasa baadhi ya
mandhari na, hata pasipo kujitambua, wanaziacha nyingine. Kwa hiyo, hapana budi
baadhi ya wafafanuzi katika kazi yao watumie mitazamo mipya inayolingana na mikondo
ya mawazo ya kisasa na ambayo hadi leo haijapewa nafasi ya kutosha. Inafaa
wafanye hivyo kwa upambanuzi wa kiuhakiki. Siku hizi makini inavutwa hasa na
vuguvugu za ukombozi na ufeministi (utetezi wa usawa wa wanawake)
Theolojia ya ukombozi ni suala changamano ambalo
haliwezi kuchukuliwa vyepesi. Kama harakati ya kitheolojia, iliimarika mnamo
mwanzoni mwa miaka ya sabini. Asili yake, pamoja na mazingira ya kiuchumi,
kijamii na kisiasa ya nchi za Amerika ya Kusini, inapatikana katika matukio
makuu mawili ya kikanisa: mosi, Mtaguso Mkuu wa Vatikano II ambao ulitamka wazi
azimio lake la “aggiornamento” (= kujiweka kisasa) na la kuzielekeza
kazi za kiuchungaji za Kanisa kwenye mahitaji ya ulimwengu wa leo; pili,
Mkutano Mkuu wa II wa Maaskofu wa Amerika ya Kusini uliofanyika Medellin mwaka
1968, ambao ulilinganisha mafundisho ya Mtaguso na mahitaji ya Amerika ya
Kusini. Halafu harakati hii imesambaa hata katika nchi nyingine za dunia
(Afrika, Asia, na watu weusi wa Marekani).
Ni vigumu kupambanua kama ipo theolojia “moja”
ya ukombozi na kuainisha mbinu yake. Kadhalika, ni vigumu kueleza ipasavyo
namna yake ya kusoma Biblia, na baadaye kuonyesha michango inayotoa na mipaka
yake pia. Yawezekana kusema kwamba theolojia hiyo haitumii mbinu maalum, bali,
kutokana na mitazamo yake maalum ya kijamii-kiutamaduni na ya kisiasa, inasoma
Biblia kwa kuyalenga mahitaji ya watu, ambao wanatafuta ndani ya Biblia chakula
cha kulisha imani yao na maisha yao.
Badala ya kujifungia ndani ya ufasiri unaoitazama
matini ilivyo, na kuyazingatia yale matini ambayo inayasema kulingana na
mazingira ilipoasiliwa, basi inatafuta ufasiri unaozaliwa kutokana na hali
halisi ya maisha ya watu. Ikiwa hao wanaishi katika hali ya kugandamizwa,
Biblia inakimbiliwa ili kutafuta ndani yake chakula kiwezacho kuwategemeza watu
katika mapambano yao na matarajio yao. Maana hali iliyopo haipaswi kusahauliwa,
bali, kinyume chake, kuzingatiwa ili iangazwe kwa mwanga wa Neno la Mungu.
Hivyo, kutokana na mapambano hayo, utendaji halisi wa kikristo utajitokeza, nao
utaelekea kuibadili jamii kwa njia ya haki na upendo. Katika imani, Maandiko
yanageuka kuwa mkikimkiki wa ukombozi wa binadamu katika hali yake yote.
Kanuni zake ndizo zifuatazo:
Mungu yupo katika historia ya watu wake ili
kuwakomboa. Naye ndiye Mungu wa walio maskini, ambaye hawezi kuvumilia
ugandamizaji wala udhalimu.
Ndiyo sababu ufafanuzi hawezi kutojihusisha,
bali, kwa kumfuata Mungu, ni lazima ujipange upande wa maskini na kujibidiisha
katika mapambano kwa ajili ya ukombozi wa wanaogandamizwa.
Kushirikiana katika mapambano hayo kunawezesha
maana mpya za matini za Biblia zidhihirike, ambazo zinavumbuliwa tu pindi
matini zenyewe zinaposomwa katika mazingira ya mshikamano wa kweli na
wanaogandamizwa.
Maadamu ukombozi wa wanaogandamizwa ni mchakato
wa pamoja, jumuiya ya maskini ndiyo mahali bora pa kuipokea Biblia kama neno la
ukombozi. Aidha, madhali matini za Biblia ziliandikwa kwa ajili ya jumuiya,
usomaji wa Biblia unakabidhiwa kwanza kwa jumuiya zenyewe. Neno la Mungu linahusiana
kabisa na zama za leo, kwa sababu hasa ya uwezo wa “matukio kadhaa yenye kuweka
msingi” (kutoka katika Misri, mateso na ufufuko wa Yesu) ya kusababisha
matekelezo mapya katika mtiririko wa historia.
Theolojia ya ukombozi ina mambo ndani yake
ambayo thamani yake haiwezi kukanwa: utambuzi wenye kina wa kuwepo kwa Mungu
mwenye kuokoa; msisitizo juu ya hali ya kijumuiya ya imani; hima ya utendaji
uletao ukombozi wenye mizizi yake katika haki na upendo; usomaji upya wa Biblia
unaojaribu kulifanya Neno la Mungu liwe mwanga na chakula cha watu wa Mungu
katika mapambano yao na matarajio yao. Ndiyo inavyosisitizwa nguvu kamili iliyo
nayo kwa siku za leo matini iliyovuviwa.
Lakini usomaji wa Biblia wenye juhudi za namna
hii unaleta hatari kadhaa ndani yake. Maadamu unahusiana na harakati
inayoendelea bado, misisitizo inayofuata haina budi kuwa ya kitambo tu.
Aina hii ya usomaji unamakinika hasa juu ya
matini za kisimulizi na za kinabii (za Biblia) ambazo zinaangaza hali ya
ugandamizaji na zinauchochea utendaji unaotaka kuleta mageuzi ya kijamii; hivyo
yawezekana kuwa njia hii pengine inatazama sehemu tu ya ukweli, pasipo
kuzingatia kwa mkazo ulio sawa matini nyingine za Biblia. Ni sahihi kusema
kwamba ufafanuzi hauwezi kutojihusisha, lakini pia lazima ujitahadhari usifungamane
na upande mmoja tu. Kwa upande mwingine, kushiriki katika harakati za kijamii
na kisiasa si jukumu la moja kwa moja la mfafanuzi.
Tena, baadhi ya wanatheolojia na wafafanuzi, kwa
kutaka kupenyeza ujumbe wa kibiblia katika mazingira ya kijamii-kisiasa,
walipaswa kutumia zana mbalimbali za uchanganuzi wa hali ya kijamii. Katika
mtazamo huo, shule nyingine za theolojia ya ukombozi zilifanya uchanganuzi
uliovuviwa na nadharia za kiyakinifu, na kuisoma Biblia ndani pia ya muundo
huo; nalo halikukosa kuleta matatizo, hususan mintarafu kanuni ya kimaksi ya
mapambano ya kitabaka.
Kwa msukumo wa shida kubwa za kijamii, mkazo
ulitiliwa zaidi juu ya eskatolojia ya kidunia, na pengine ukalidhuru suala la
eskatolojia ya mbinguni ya Maandiko.
Mageuzo ya kijamii na ya kisiasa yanafanya njia
hiyo ijihoji upya na kutafuta maelekeo mapya. Kwa maendeleo yake ya baadaye na
kwa manufaa yake katika Kanisa, suala kuu litakuwa kuainisha dhanio zake za
kihemenetiki, kama vile mbinu zake na mshikamano wake na imani na Mapokeo ya
Kanisa zima.
Hemenetiki ya kifeministi (au ya mtazamokike) ya
Biblia ilianzishwa mnamo mwishoni mwa karne XIX huko Marekani, katika mazingira
ya kijamii-kiutamaduni ya mapambano kwa ajili ya haki za wanawake; ndipo kamati
ya matengenezo ya Biblia ilipotoa “The Woman’s Bible” (“Biblia ya
mwanamke”) katika vitabu viwili (New York 1885, 1898). Vuguvugu hiyo
ilijidhihirisha kwa nguvu mpya na kuonyesha maendeleo makubwa kuanzia miaka ya
sabini, ikifungamana na harakati ya ukombozi wa wanawake, hasa katika Amerika
ya Kaskazini. Kwa kueleza kwa usahihi, inabidi kutofautisha aina mbalimbali za
hemenetiki ya kifeministi ya Biblia, maana mbinu zinazotumika zahitilafiana
sana. Umoja wake unatokana na dhamira hiyo moja, yaani wanawake, na pia na
lengo linalokusudiwa: ukombozi wa wanawake na upatikanaji wa haki zilizo sawa
na zile za wanaume.
Inafaa kuzitaja hapa aina tatu za msingi za
hemenetiki ya kifeministi ya Biblia: mtindo mkali, mtindo halisi-mamboleo, na
mtindo wa kiuhakiki.
Mtindo mkali unakataa kabisa
mamlaka ya Biblia, na kushikilia nadharia ya kuwa Biblia ilitungwa na wanaume
kwa madhumuni ya kuhakikisha utawala wa mwanaume juu ya mwanamke
(androsentrismi).
Mtindo halisi-mamboleo unaikubali
Biblia kama neno la kinabii; nayo Biblia inasemwa kuwa inafaa kwa kadiri
inavyoegemea upande wa wadhaifu na kwa hiyo pia upande wa wanawake; mtazamo huo
unachukulika kama “kanoni ndani ya kanoni”, ili kudhihirisha wazi yale yote
yanayosaidia ukombozi wa wanawake na haki zao.
Mtindo wa kiuhakiki unatumia
mbinu nyerevu ili kujaribu kuvumbua tena wadhifa na jukumu la wanawake wa
kikristo katika kundi la wafuasi wa Yesu na katika Makanisa ya Mt. Paulo.
Wakati huo – inavyodaiwa – kulikuwepo hali ya usawa; lakini hali hiyo
ilisitiriwa katika maandishi ya Agano Jipya, kwa kiasi kikubwa, na hata zaidi
baadaye, wakati ubabedume na androsentrismi vilipozidi kushinda.
Hemenetiki ya kifeministi haikutengeneza mbinu
mpya. Inatumia mbinu za kawaida za ufafanuzi, hasa ile ya kihistoria-kiuhakiki.
Ila inaongeza vigezo viwili vya utafiti.
Kigezo cha kwanza ndicho cha kifeministi,
kinachofuata harakati ya ukombozi wa wanawake, katika mkondo mpana zaidi wa
harakati ya theolojia ya ukombozi. Nacho kinatumia hemenetiki ya tuhuma:
maadamu kwa kawaida historia imeandikwa na washindi, ili kufukua ukweli inafaa
kutotegemea matini zenyewe, bali kutafuta ndani yake vidokezo vinavyoweza
kuonyesha hali iliyo tofauti.
Kigezo cha pili ni cha kisosholojia; hicho kina
misingi yake katika utafiti wa jamii za nyakati za Biblia, wa tabaka zake za
kijamii na wa nafasi ya wanawake ndani yake.
Mintarafu maandishi ya Agano Jipya, mada ya
uchunguzi si zaidi dhana ya mwanamke inavyoelezeka katika Agano Jipya, bali ni
kuelewa kihistoria hali mbili tofauti za wanawake katika karne ya kwanza: yaani,
kwa upande mmoja, hali yake ya kawaida katika jamii ya kiyahudi na ya
kigiriki-kirumi; na kwa upande mwingine, hali iletayo mambo mapya iliyoanzishwa
katika vuguvugu ya Yesu na katika Makanisa ya Mt. Paulo, ambapo iliundwa –
inavyosemwa – “jumuiya ya wafuasi wa Yesu, wote wenye hali moja”. Matini
mojawapo inayodaiwa kuwa msingi wa mtazamo huo ni Gal 3:28. Na lengo ni
kuivumbua upya, kwa ajili ya nyakati zetu, historia iliyosahauliwa ya wadhifa
wa wanawake katika Kanisa la mwanzoni.
Michango mingi mizuri imeletwa kutokana na
ufafanuzi wa kifeministi. Kwa njia hii wanawake wameshiriki kama watendaji hai
katika utafiti wa kifafanuzi; nao wamefaulu kuvihisi – mara nyingi vizuri zaidi
kuliko wanaume – uwepo, maana, na dhima vya mwanamke katika Biblia, katika
historia ya asili za kikristo na katika Kanisa. Upeo wa utamaduni wa kisasa
unazingatia kwa makini zaidi heshima ya mwanamke na dhima yake katika jamii na
katika Kanisa; hivyo unafanya yaulizwe maswali mapya kwa matini ya Biblia, na
kwa njia hii unaleta chanzo cha uvumbuzi mpya. Aidha, hisia za kike zinasaidia
kufichua na kusahihisha baadhi ya fasiri zilizokuwa zinakubalika, zenye ubaguzi
ndani yake na zilizolenga kuthibitisha kuwa ni halali utawala wa mwanamume juu
ya mwanamke.
Mintarafu Agano la Kale, chunguzi nyingi
zimejibidisha kuufikia ufahamu mzuri zaidi wa sura ya Mungu. Mungu wa Biblia si
matokeo ya muundo wa mawazo wa kiubabedume. Yeye ndiye Baba, lakini pia ni
Mungu mwenye huruma na upendo wa kimama.
Ila, ufafanuzi wa kifeministi, kwa kadiri unavyotokana
na msimamo wa kiubaguzi, unaingia hatari ya kufasiri matini za Biblia kwa namna
isiyo halisi, tena inayoweza kupingwa. Ili kuthibitisha msimamo wake mara
nyingi ufafanuzi huo hauna njia nyingine isipokuwa kuzikimbilia hoja “ex
silentio” (= zilizo kimya). Nazo, inavyoeleweka, haziaminiki sana, wala
haziwezi kamwe kutosha ili kulifikia hitimisho lililo imara. Kwa upande
mwingine, ufafanuzi huo umefanya jitihada ili kuielewa hali fulani ya
kihistoria kwa kuvizingatia vidokezo vyepesi vinavyopatikana katika matini;
tena unadhani kuwa matini hizo zinataka kuificha hali hiyo ya kihistoria. Kumbe
hii si tena kazi ya ufafanuzi timamu, kwa maana inafikia hatua ya kukataa
maudhui ya matini zilizovuviwa ili kupendekeza badala yake mtungo mpya tofauti
na wa kinadharia tete tu.
Mara nyingi ufafanuzi wa kifeministi unazusha
pia suala la utawala katika Kanisa; suala ambalo, inavyojulikana, ni mada ya
majadiliano na pia ya migongano. Katika uwanja huo, ufafanuzi wa kifeministi
utaweza kuleta manufaa kwa Kanisa kwa kadiri tu utakavyoepukana na mitego
ileile inayoilaumu, na pia utakavyozingatia mafundisho ya kiinjili kuhusu
utawala kama utumishi, mafundisho yaliyoelekezwa na Yesu kwa wanafunzi wote,
wanaume kwa wanawake[2].
Usomaji wa kifundamentalisti una asili yake
katika kanuni ya kwamba Biblia, maadamu ni Neno la Mungu lenye kuvuviwa na
lisilopatwa na kosa, haina budi kusomwa na kufasiriwa kisisisi katika vipengere
vyake vyote. Ila usomaji huo unafasili “ufasiri sisisi” (literal
interpretation) ukimaanisha ufasiri “wa kiherufi” (naively literalist),
ambao unajikita katika usisisi na kukataa kila jitihada ya kuielewa Biblia kwa
kuzingatia ukuzi wake katika mfululizo wa historia na maendeleo yake. Hivyo,
unapinga matumizi ya mbinu ya kihistoria-kiuhakiki kwa ufasiri wa Maandiko
Matakatifu, kama vile ya mbinu yoyote nyingine ya kisayansi.
Usomaji wa kifundamentalisti ulianzishwa,
nyakati za Matengenezo (Reformation), kutokana na kero ya kuwa waaminifu
kwa maana sisisi ya Maandiko. Baada ya karne ya Mwangazo (Enlightenment),
ulijifahamisha katika Uprotestanti kama kinga dhidi ya ufafanuzi huria (liberal
exegesis). Jina “Ufundamentalisti” lilitumika kwa mara ya kwanza katika
Warsha ya Kibiblia ya Kimarekani iliyofanyika huko Niagara, jimbo la New York,
mwaka 1895. Katika nafasi hiyo wafafanuzi waprotestanti wahifadhina (conservative)
waliweka “pointi tano za ufundamentalisti”: kutokukosa kwa kila neno la
Maandiko (verbal inerrancy), umungu wa Kristo, kuzaliwa kwake kutoka kwa
bikira, mafundisho ya fidia kaimu (vicarious expiation), na ufufuko wa
miili wakati wa ujio wa pili wa Kristo. Pindi usomaji wa kifundamentalisti
ulipotapakaa katika sehemu nyingine za ulimwengu ulizalisha namna nyingine za
kusoma Biblia, nazo zenye tabia ya “usisisi wa kiherufi” (literalist),
katika Ulaya, Asia, Afrika na Amerika ya Kusini. Mtindo huo wa usomaji unazidi
kupata washiriki wengi, katika miaka ya mwisho ya karne ya ishirini, miongoni
mwa vikundi vya kidini na madhehebu, na pia kati ya Wakatoliki.
Ufundamentalisti unaweza kuwa na haki kukazia
uvuvio wa kimungu wa Biblia, kutokukosa kwa Neno la Mungu na kweli nyingine za
kibiblia zilizomo katika pointi zile tano za msingi; lakini namna yake ya
kueleza kweli hizo ina mizizi yake katika itikadi isiyo ya kibiblia, yawayo
yote wayaseme wawakilishi wake. Maana, itikadi hiyo inadai kuambatana imara na
kwa hakika na mazoea makali ya kimafundisho, pia inauweka kama sharti, kama
chemchemi pekee ya ufundishaji kuhusu maisha ya kikristo na ya wokovu, usomaji
wa Biblia unaokataa kila tabia au utafiti vya kiuhakiki.
Shida ya msingi ya usomaji huo wa
kifundamentalisti ni kwamba unakataa kujali tabia ya kihistoria ya ufunuo wa
Biblia, na hivyo unajifanya hauwezi kuupokea kikamilifu ukweli wa Umwilisho
wenyewe. Ufundamentalisti unakwepa uhusiano wa kiundani uliopo kati ya kilicho
cha kimungu na kilicho cha kibinadamu katika kuhusiana na Mungu. Tena unakataa
kukubali kwamba Neno la Mungu lililovuviwa lilielezwa kwa lugha ya kibinadamu
na kuhaririwa, chini ya uvuvio wa kimungu, na waandishi wa kibinadamu ambao
uweza na maarifa vyao vilikuwa na mipaka. Ndiyo sababu mwelekeo wake ni kujali
matini ya Biblia kana kwamba imeandikwa mfano wa imla, neno kwa neno, kwa kazi
ya Roho Mtakatifu; wala haufikii kutambua kuwa Neno la Mungu lilitungwa kwa
lugha na semi zilizoathiriwa na mazingira ya nyakati fulani. Na kadiri yake
hakuna uzingativu wowote kwa fani za kifasihi na kwa miundo ya kibinadamu ya
mawazo iliyopo katika matini za Biblia, ambazo nyingi zake ndizo tunda la
mchakato ulioendelea kwa muda mrefu na kubeba athari za hali mbalimbali za
kihistoria.
Aidha, ufundamentalisti hukazia kwa namna
isivyofaa kutokukosa hata kwa vipengele vidogo vidogo (details) vya
matini za Biblia, hasa kuhusu matukio ya kihistoria au mintarafu kweli
zinazodaiwa kuwa na uzito wa kisayansi. Mara nyingi hukitilia maana ya
kihistoria kile kisichokuwa na dai hilo, kwa sababu huyahesabu kama matukio ya
kihistoria yale yote yaelezwayo au kusimuliwa kwa vitenzi vinavyotumika katika
wakati uliopita; wala hauzingatii kama ipasavyo uwezekano wa kuwepo maana ya
kiishara au ya kitamathali.
Mara nyingi ufundamentalisti una tabia ya
kutojali au kukanusha matata yaliyopo katika matini ya Biblia katika utungo
wake wa Kiebrania, Kiaramu au Kigiriki. Mara nyingi hufungamana na tafsiri
fulani maalum (ya Biblia), ya zamani au ya kisasa. Na vilevile huacha
kuzingatia “kusoma upya” (relectures) kwa sehemu kadhaa za Biblia
kunakofanyika katika Biblia yenyewe.
Kuhusu Injili, ufundamentalisti haujali ukuzi wa
mapokeo ya kiinjili, bali unachanganya moja kwa moja hatua ya mwisho ya mapokeo
hayo (yaani waliyoyaandika wainjili) na hatua yake ya kwanza (yaani matendo na
maneno ya Yesu wa kihistoria). Na wakati huohuo lapuuzwa suala lililo muhimu:
yaani namna jumuiya zenyewe za kwanza za kikristo zilivyoelewa athari
iliyoletwa na Yesu wa Nazareti na ujumbe wake. Kumbe, papo hapo tunao ushuhuda wa
asili ya kitume ya imani ya kikristo, na pia ujumbe wake wazi. Kwa njia hii,
ufundamentalisti unaumbua hulka ya wito unaotolewa na Injili yenyewe.
Aidha, ufundamentalisti unaleta mitazamo finyu
sana: maana unaamini kuwa kosmolojia ile ya kale, iliyokwisha futwa, bado
inalingana na ukweli; na sababu yake ni kwamba inaelezwa hivyo katika Biblia.
Hali hii inazuia isifanyike dialogia na upeo mpana zaidi wa mahusiano yaliyopo
baina ya utamaduni na imani. Tena hutegemea usomaji usio wa kiuhakiki wa matini
kadhaa za Biblia ili kuthibitisha maoni ya kisiasa na mitazamo ya kijamii
vinavyoathiriwa na ubaguzi, kwa mfano ubaguzi wa kikabila, ambao haulingani
katu na Injili ya Kristo.
Na hatimaye, katika kushikamana kwake na kanuni
ya “Maandiko tu” ufundamentalisti hutenganisha ufasiri wa Biblia na Mapokeo
yanayoongozwa na Roho Mtakatifu, na ambayo hujiendeleza kwa namna iliyo halisi
kwa kuungana na Maandiko ndani kabisa ya jumuiya ya imani. Ufundamentalisti
hauna utambuzi wa kwamba Agano Jipya limeumbika (took form) ndani ya
Kanisa la kikristo na kwamba ndilo Maandiko Matakatifu ya Kanisa hili, ambalo
kuwepo kwake kuliutangulia utungaji wa matini zake. Ndiyo maana, mara nyingi
ufundamentalisti unapinga Kanisa, kwa kupuuza kanuni za imani, dogma na ibada
za kiliturujia ambazo zimekuwa sehemu muhimu za mapokeo ya kikanisa; hali
kadhalika, kwa kupuuza jukumu la kufundisha la Kanisa lenyewe. Hivyo
unajionyesha kama namna ya ufasiri wa kibinafsi, ambao hautambui kuwa Kanisa
limejengwa juu ya Biblia na kuchota uzima wake na msukumo wake katika Maandiko.
Njia ya kifundamentalisti ni ya hatari, kwa
sababu huwavuta watu wanaotafuta majibu katika Biblia kwa matatizo ya maisha
yao. Na njia hiyo huweza kuwatia mauzauza kwa kutoa fasiri zenye hali ya
utakatifu lakini yanayodanganya, badala ya kuwaambia wao kwamba Biblia si
lazima iwe na jibu la mara moja kwa kila moja ya matatizo hayo. Bila ya
kutamka, ufundamentalisti huwaalika watu katika aina fulani ya kujiua kwa
mawazo. Tena unatia maishani uhakika wa uongo, kwa maana huichanganya pasipo
kutambua mipaka ya kibinadamu ya ujumbe wa Biblia na udhati wa kimungu wa
ujumbe huo.
Mwendo wa ufafanuzi unaitwa kufikiriwa tena kwa
kuzingatia hemenetiki ya kifalsafa ya siku hizi, ambayo imesisitiza dhima ya
hisia-mtu (subjectivity) katika mchakato wa ujuzi, na hasa katika ujuzi
wa kihistoria. Tafakuri ya kihemenetiki imepata mwamko mpya kwa uchapishaji wa
kazi za Friedrich Schleiermacher, Wilhelm Dilthey, na hasa vya Martin
Heidegger. Katika mkondo wa wanafalsafa hao – lakini pia kwa kutofautiana nao –
wasomi kadhaa wamechimba kiundani zaidi nadharia ya hemenetiki ya siku za leo,
na matumizi yake kwenye Maandiko Matakatifu. Miongoni mwao tutawataja hasa
Rudolf Bultmann, Hans Georg Gadamer na Paul Ricoeur. Haiwezekani hapa kueleza
kwa muhtasari wa kuridhisha fikra zao. Itoshe tu kusisitiza baadhi ya mawazo ya
msingi ya falsafa yao ambayo huathiri ufasiri wa matini za Biblia [3].
Akitambua umbali wa kiutamaduni uliopo baina ya
ulimwengu wa karne ya kwanza na ule wa karne ya ishirini, Bultmann amejibidisha
ili uhalisi unaoongelewa na Maandiko Matakatifu uongee pia na binadamu wa
nyakati zetu. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa ufahamu tangulizi unaohitajika kwa
kila ufahamu, na ametengeneza nadharia ya ufasiri wa kiudhanaishi (existential)
wa maandishi ya Agano Jipya. Kwa kutegemea fikra za Heidegger, Bultmann asema
kwamba ufafanuzi wa matini fulani ya Biblia hauwezekani pasipo dhanio tangulizi
(presuppositions) kadhaa zenye kuuongoza ufahamu wake. Na ufahamu
tangulizi (“Vorverständnis”) una msingi wake katika uhusiano wa kimaisha
(“Lebenverhältnis”) baina ya mfasiri na lile jambo linaloongelewa na matini.
Ili kukwepa ufasiri unaotawaliwa na uhisiamtu, ufahamu tangulizi ni lazima
ukubali kuongezewa kina na kutajirishwa na kile kinachoongelewa na matini, na
hata kurekebishwa na kusahihishwa nacho.
Tena, Bultmann anajihoji ni muundo upi wa fikra
ulio sahihi kwa minajili ya kutunga maswali ambayo kuanzia nayo matini za
Maandiko zitaeleweka kwa watu wa nyakati zetu. Naye anadai kuwa jawabu
hupatikana katika uchanganuzi wa kiudhanaishi wa Heidegger. Kadiri yake kanuni
za kiudhanaishi za ki-Heidegger zaweza kutumika katika nyanja zote, nazo
zinaweka miundo na dhana zenye kufaa zaidi kwa ufahamu wa maisha ya kibinadamu
yanavyofunuliwa katika ujumbe wa Agano Jipya.
Gadamer vilevile akaza umbali wa kihistoria uliopo baina ya matini na
mfasiri wake. Naye anafuata na kuendeleza nadharia ya “duara ya kihemenetiki” (hermeneutical
circle). Vitarajio (anticipations) na dhana tangulizi (preconceptions)
vinavyoathiri ufahamu wetu hutokana na mapokeo yanayotutegemeza. Nao ni jumla
ya data za kihistoria na kiutamaduni zilizo mazingira yetu ya kimaisha na upeo
wetu wa ufahamu. Basi, mfasiri anawajibika kuingia katika mjadala na uhalisi
unaozungumziwa katika matini. Na ufahamu hupatikana katika muungano wa peo
mbili tofauti, yaani upeo wa matini na ule wa msomaji wake
(“Horizontverschmelzung”); nao ufahamu huwezekana ikiwa tu kuna mwingiliano (belonging,
“Zugehörigkeit”), yaani uwiano wa kimsingi kati ya mfasiri na matini anayozingatia.
Hemenetiki ni mchakato wa kimjadala (dialectical process): maana ufahamu
wa matini fulani u daima pia ufahamu mpana zaidi apatao mfasiri juu yake
mwenyewe.
Mintarafu fikra za kihemenetiki za Ricoeur,
awali ya yote yabidi kusisitiza umuhimu wa “dhima ya kujiweka mbali”; nayo ni
utangulizi wa lazima wa kujitwalia matini kisahihi. Maana, kwanza upo umbali
baina ya matini na mwandishi wake, kwa sababu matini ikiisha tungwa, kwa kiasi
fulani inaanza kujitegemea yenyewe mbali na mtungaji wake; nayo inaanza safari
ya ile iliyo maana yake. Pili, upo umbali baina ya matini na wasomaji wake wa
baadaye; hawa hawana budi kuyaheshimu mazingira ya matini katika hali yake ya
utofauti. Hivyo, mbinu za uchanganuzi wa kifasihi na wa kihistoria ni za lazima
kwa ufasiri. Walakini maana ya matini fulani yaweza kupatikana kikamilifu ikiwa
tu yenyewe inahusishwa (is actualized) katika maisha ya wasomaji
wanaojitwalia. Nao, kutokana na hali yao, watakiwa kuzidokeza maana mpya
zinazoendana na ile ya msingi inayoonyeshwa na matini. Ujuzi wa kibiblia
hauwezi kujikita katika lugha tu, bali unajibidisha kuufikia uhalisi
unaoongelewa na matini. Lugha ya kidini ya Biblia ni lugha ya kiishara
“inayofikirisha” (“gives rise to thought”), tena ni lugha ambayo
binadamu hakomi kuuvumbua utajiri mwingi wa maana yake; na hatimaye ni lugha
inayolenga katika kikomo kinachopita ufahamu, na wakati huohuo inayomfanya
binadamu afahamu ukweli wenye kina wa maisha yake (personal existence).
Je, tuseme nini juu ya nadharia hizo za nyakati
zetu zihusuzo ufasiri wa matini? Biblia ndilo Neno la Mungu kwa nyakati zote
zifuatanazo katika historia. Na kutokana na hilo haiwezekani kutojali nadharia
ya kihemenetiki inayowezesha kuingiza mbinu za uhakiki wa kifasihi na wa
kihistoria katika mtindo wa ufasiri ulio mpana zaidi. Ni suala la kuuvuka
umbali uliopo baina ya wakati wa waandishi na walengwa wa kwanza wa hizo matini
za Biblia na ule wa kwetu, hivi kwamba iwezekane kuuhusisha (actualization)
kwa usahihi ujumbe wa matini ili kulisha maisha ya imani ya wakristo. Kila
ufafanuzi wa matini unaitwa kukamilishwa kwa njia ya “hemenetiki”, kadiri ya
maana hilo neno liliyopewa siku za karibuni.
Ulazima wa hemenetiki, yaani wa ufasiri wa
matini katika mazingira ya siku za leo ya ulimwengu wetu, una msingi wake
katika Biblia yenyewe na katika historia ya ufasiri wake. Jumla ya maandishi ya
Agano la Kale na Agano Jipya hujionyesha kama tunda la mchakato wa muda mrefu
wa kufasiri upya matukio ya kuweka misingi, kwa kuyahusianisha kiundani na
maisha ya jumuiya za waamini.
Katika mapokeo ya Kanisa wafasiri wa kwanza wa
Maandiko Matakatifu, ndio Mababa wa Kanisa, walidhani kwamba ufafanuzi wao
umekamilika ukiwa tu walifaulu kuitokeza maana ya matini kwa ajili ya wakristo
wa nyakati zao na katika mazingira yao. Ufafanuzi ni mwaminifu kwa nia ya
matini za Biblia kwa kadiri ile tu ambayo unajitahidi kupata – katika mtima wa
mitungo ya matini yenyewe – uhalisi wa imani ambayo matini zinaonyesha; tena
ikiwa unaunganisha uhalisi huo na mang’amuzi ya kiimani ya ulimwengu wetu.
Hemenetiki ya siku za leo ni jibu lifaalo kwa
falsafa umbile ya kihistoria na kwa kishawishi cha kuvitumia katika mtaala wa
Biblia vile vigezo visivyoathiriwa na hisia za kibinafsi (objective), ambavyo
hutumika katika sayansi asilia (natural science). Kwa upande
mmoja, matukio yasimuliwayo katika Biblia ni matukio yaliyofasiriwa; kwa upande
mwingine, kila ufafanuzi wa masimulizi ya matukio hayo hauna budi kuhusisha
athari ya hisia (subjectivity) za mfafanuzi mwenyewe.
Ufahamu sahihi wa matini ya Biblia unapatikana tu kwake yeye aliye na uhusiano
wa kimaisha na kile kinachoongelewa na matini. Suala linalomkabili kila mfasiri
ndilo hili lifuatalo: je, ni nadharia ipi ya kihemenetiki inayowezesha ufahamu
sahihi wa uhalisi kiundani unaoongelewa na Maandiko Matakatifu; na ni nadharia
ipi inayowezesha kuelezea uhalisi huo kwa namna iliyo na maana kwa binadamu wa
siku za leo?
Kwa kweli, inabidi kutambua kwamba baadhi ya
nadharia ya kihemenetiki hazitoshi ili kuyafasiri Maandiko Matakatifu. K.m.
ufasiri wa kiudhanaishi wa Bultmann unaelekeza kufunga ujumbe wa kikristo
katika mipaka ya falsafa moja ya pekee. Aidha, kwa ajili ya dhanio tangulizi (presuppositions) zilizo
misingi ya hemenetiki hiyo, ujumbe wa kidini wa Biblia unanyimwa sehemu kubwa
ya uhalisia (objective reality) wake (kwa sababu ya
kupunguza mno utakatifu wake – démytholygization); hivyo unawekwa
chini ya utawala wa ujumbe wa kianthropolojia. Falsafa inakuwa kanuni ya
ufasiri badala ya kuwa chombo cha ufahamu wa kile kilicho kiini kabisa cha kila
ufasiri: yaani nafsi ya Yesu Kristo na matukio ya wokovu yaliyotimizwa katika
historia yetu. Hivyo, ufasiri wa Maandiko, awali ya yote ni kuipokea maana
iliyopo katika matukio kadhaa na, kwa namna iliyo bora zaidi, katika nafsi ya
Yesu Kristo.
Hii ndiyo maana ielezwayo katika matini. Na ili
kuepukana na namna za usomaji zinazotegemea hisia za kibinafsi tu (purely
subjective readings), ni lazima ufasiri ufaao kwa wakati huu (actualization)
uwe na msingi katika uchunguzi wa matini, na dhanio tangulizi za ufasiri huo
hazina budi kuhakikishwa tena na tena katika matini yenyewe.
Hemenetiki ya kibiblia, ijapo ni sehemu ya
hemenetiki ya jumla ya kila matini ya kifasihi na kihistoria, wakati huohuo ni
kipengere pekee cha hemenetiki hiyo. Na upekee wake hutokana na kile
kinachochunguzwa nayo. Kwani matukio ya wokovu na utimilifu wake katika nafsi
ya Yesu Kristo vinaipa historia yote ya kibinadamu maana yake halisi. Fasiri
mpya za kihistoria zitaweza tu kuwa ufunuo au uonyesho wa utajiri huo wa maana.
Simulizi la kibiblia la matukio hayo haliwezi kueleweka kikamilifu na akili
peke yake. Ufasiri wake hauna budi kuongozwa na matukio tangulizi (presuppositons)
kadhaa, yaani, k.m. kuishi imani katika jumuiya ya kikanisa, na kuwa na mwanga
wa Roho Mtakatifu.
Jinsi yanavyokua maisha katika Roho, ndivyo
ukuavyo pia ufahamu wa msomaji kuhusu yale yote yanayoongelewa na matini ya
Biblia.
Mchango wa siku za leo wa hemenetiki za
kifalsafa na maendeleo ya hivi karibuni ya mtaala wa kisayansi wa fasihi
mbalimbali vinauwezesha ufafanuzi wa kibiblia kuchimba ndani ya ufahamu wa
wajibu wake, ambao uchangamano (complexity) wake umekuwa dhahiri zaidi.
Ufafanuzi wa kale, ambao yakini haukuweza kuzingatia madai ya kisayansi ya
nyakati zetu, uliihesabia kila matini ya Maandiko viwango mbalimbali vya maana. Upambanuzi
uliotangaa zaidi ulikuwa kati ya maana sisisi (literal sense) na
maana ya kiroho (spiritual sense). Ufafanuzi wa Enzi ya Kati
(Medieval exegesis) ulipambanua katika maana ya kiroho mandhari tatu
tofauti: mandhari ya kwanza inahusiana na ukweli uliofunuliwa; ya pili,
inahusiana na mwenendo unaotakiwa kufuatwa; na ya tatu, na utimilifu wa nyakati
za mwisho. Tokea hayo ilitungwa beti maarufu, inayojulikana kuwa ya Augustino
wa Denmark (karne ya 13): “Littera gesta docet, quid credas allegoria,
moralis quid agas, quid speres anagogia” (= “Maana sisisi hufunza matukio;
maana ya mifano, nini usadiki; maana ya maadili, ufanye nini; maana za umilele,
wapi unakoelekea”).
Dhidi ya uwingi huo wa maana, ufafanuzi ya
kihistoria-kiuhakiki umeshikilia – kwa wazi ama sivyo – nadharia ya umoja wa
maana, ambayo kadiri yake matini haiwezi kuwa na maana mbalimbali kwa wakati
mmoja. Bidii zote za ufafanuzi wa kihistoria-kiuhakiki zinalenga kufasili ile maana
halisi ya matini fulani ya Biblia kadiri ya mazingira ambamo imetungwa.
Lakini nadharia hiyo hugongana sasa na fikra za
sayansi za lugha na za hemenetiki za kifalsafa, zisemazo kwamba maandishi
huleta maana nyingi (plurality of meanings).
Suala hili si sahili, wala haliwezi kukabiliwa
kwa mtazamo uleule mmoja katika tanzu zote za matini: k.m., masimulizi ya
kihistoria, mifano, maaguzi, sheria, mithali, sala, tenzi, n.k. Hata hivyo,
yawezekana kueleza kanuni kadhaa, tukizingatia daima tofauti ya rai mbalimbali.
Si halali tu, bali ni ya lazima kujaribu
kuifasili maana kamili ya matini kadiri zilivyotungwa na waandishi wake; na
hiyo maana huitwa “sisisi”. Mt. Thomaso wa Akwino alikuwa amekwisha kusisitiza
umuhimu wake wa msingi (S. Th., I, q. 1, a. 10, ad 1).
Maana sisisi haipaswi kuchanganywa na maana ya
“kiherufi” ambayo wafundamentalisti hushikamana nayo. Haitoshi kuitafsiri
matini neno kwa neno ili kupata maana yake sisisi. Kwani ni lazima kuielewa
matini kwa mujibu wa kaida za kifasihi za wakati wake. Ikiwa ni matini ya
kiistiara, maana yake sisisi si ile itokanayo moja kwa moja na maneno yenyewe,
(kwa mfano; “Viuno vyenu na viwe vimefungwa”, Lk 12:35), bali ile inayolingana
na matumizi ya kiistiara ya maneno yale (“Mwe tayari kila wakati”). Tena ikiwa
ni masimulizi, maana sisisi si lazima idai kuwa matukio yaliyosimuliwa hakika
yamejiri; maana masimulizi hayo hayaingii moja kwa moja utanzu wa kihistoria,
bali yaweza kuwa yamebuniwa tu.
Maana sisisi ya Maandiko Matakatifu ndiyo ile
iliyowekwa moja kwa moja na wanadamu walioyatunga kwa uvuvio wa kimungu. Nayo
maana, maadamu ni tunda la uvuvio huo, ilikusudiwa na Mungu pia, aliye mtunzi
mkuu. Tena inagunduliwa kwa njia ya uchanganuzi maalumu wa matini, baada ya
kuiweka katika mazingira yake ya kifasihi na ya kihistoria. Jukumu la kwanza la
ufafanuzi ndilo la kuongoza katika uchanganuzi huo, kwa kuzitumia fursa zote
zinazowezekana za tafiti za kifasihi na za kihistoria, kwa madhumuni ya
kuifasili maana sisisi ya matini za Biblia kwa usahihi kamili iwezekanavyo (Divino
afflante Spiritu, EB 550). Kwa lengo hilo, mtaala wa tanzu za fasihi
andishi za zamani hasa hudaiwa (ibid. 560).
Je, na maana sisisi ya matini fulani ni
moja tu? Kwa kawaida, ndiyo. Lakini si lazima iwe hivyo kila mara; na
sababu zake ni hizo mbili zifuatazo. Kwa upande mmoja, mwandishi mtu anaweza
kudhamiria maana mbili tofauti kwa wakati mmoja; nalo ni la kawaida katika
ushairi. Uvuvio wa Biblia haudharau mtazamo huo wa kisaikolojia na wa lugha ya
kibinadamu; na Injili ya nne huleta mifano mingi ya jambo hilo. Kwa upande
mwingine, hata pale usemi wa kibinadamu unapoonekana kuleta maana moja tu,
ndipo uvuvio wa kimungu huweza kuongoza huo usemi na hivi kusababisha kuwepo
zaidi ya maana moja (ambivalence). Ndivyo inavyotokea katika usemi wa
Kayafa katika Injili ya Yohane 11:50, ambao kwa wakati mmoja humaanisha hila
potofu ya kisiasa na pia ufunuo wa kimungu. Mandhari hizo mbili zinaingia zote
katika maana sisisi, kwani zote zinaeleweka kufuatana na muktadha. Na ijapo huo
ni mfano wa pekee, hata hivyo ni wa maana sana; tena, lazima ututahadharishe
dhidi ya dhana iliyo finyu mno ya maana sisisi ya matini zilizovuviwa.
Kwa namna ya pekee, yafaa kuzingatia hali ya
kimkikimkiki (dynamic aspect) ya matini zilizo nyingi. Kwa
mfano, maana ya zaburi za kifalme lazima isifungwe tu ndani ya mazingira ya
kihistoria ambamo zilitungwa. Akimzungumzia mfalme, mtunga zaburi alikuwa
anadokeza kwa wakati mmoja mtindo wa asasi ya ufalme uliokuwepo, na mwingine
unaotarajiwa na unaolingana na mpango wa Mungu; hivyo matini ya huyo mtunzi
ilikuwa ikitazama mbele zaidi kuliko ile asasi ya ufalme uliojidhihirisha
katika historia. Mara nyingi mno ufafanuzi wa kihistoria-kiuhakiki umeelekea
katika kupunguza maana ya matini kwa kuifungamanisha tu na mazingira maalumu ya
kihistoria. Badala yake, ingebidi huo ufafanuzi ujitahidi kubainisha mwelekeo
wa fikra zinazoelezwa katika matini; nao mwelekeo, mbali na kumsukuma mfafanuzi
kuiwekea mipaka maana ya matini, kinyume chake umsaidie kuhisi miendelezo yake
inayotabirika wazi ama sivyo.
Mkondo mmojawapo wa hemenetiki ya kisasa
umesisitiza tofauti ya hadhi ambayo neno la binadamu linafaidi pale
linapoandikwa. Matini iliyoandikwa inaweza kutiwa katika mazingira mapya
yanayoiangaza kwa namna tofauti, na yenye kuziongeza maana (meanings) mpya
kwa maana, au fahiwa, (sense) yake asilia. Uwezo huo wa
matini iliyoandikwa unadhihirika hasa katika matini za Biblia, zinazokubaliwa
kuwa neno la Mungu. Na kweli, kitu kilichofanya jumuiya ya waamini izihifadhi
hizo matini kilikuwa kusadiki kwamba zitaendelea kuleta mwanga na uzima kwa
vizazi vijavyo. Hivyo, tangu awali maana sisisi ina muundo wa kuyapokea
maendelezo mapya, kwa njia ya “kuzisoma upya” (relectures) matini
ndani ya mazingira mapya.
Ila kinachotokana na hayo si kwamba huwezekana
kuipa matini ya Biblia maana yoyote ile, kwa kuifasiri kila mtu anavyopenda.
Kinyume chake, ni lazima kukataa kama ufafanuzi usio wa kweli kila ufasiri ulio
“mgeni” (alien) kulingana na maana iliyokusudiwa na wanadamu
walioandika matini yao. Kuzikubali maana zilizo ngeni (Kifr. hétérogènes)
ingekuwa sawa na kung’oa ujumbe wa Biblia katika mizizi yake, yaani neno la
Mungu lililowasilishwa katika historia; na vilevile ni kuyafungulia mlango
maoni ya kibinafsi yasiyoweza kudhibitiwa.
Hata hivyo; haifai kulichukua neno “ugeni” (hétérogènes) katika
maana iliyo finyu, yaani yenye kupinga kila uwezekano wa utimilifu ulio bora
zaidi. Tukio la Pasaka, la kifo na ufufuko wa Yesu, limeyaweka mazingira ya
kihistoria yaliyo mapya kabisa, ambamo huangaza upya matini za kale na
kusababisha mabadiliko katika maana yake ya kwanza. Kwa namna ya pekee, matini
kadhaa ambazo, katika mazingira ya kale, zilitazamwa kuwa kama chuku (hyperbole) (k.m. uaguzi
ambao kwao Mungu, akiongelea mwana wa Daudi, aliahidi kwamba atauweka imara ufalme
wake hata milele: 2Sam 7:12-13; 1Nya 17:11-14), matini hizo hazina budi
kuchukuliwa sasa katika maana yake sisisi, kwa kuwa “Kristo akiisha kufufuka
katika wafu hafi tena” (Rum 6:9). Na hapo, wale wafafanuzi walio na dhana
finyu, ya “kihistoria”, ya maana sisisi, inayokubali tu ile maana itokanayo na
mazingira ya kihistoria ambamo matini zilitungwa, hao watafikiri kwamba pana
“ugeni” kati ya ufafanuzi huo na matini asilia. Bali wale wanaoikubali “hali ya
kimkikimkiki” ya matini watatambua kuwepo mwendelezo mkubwa, na wakati huohuo
kuwepo pia njia ya kuingia katika kiwango kilicho tofauti: Kristo hutawala hata
milele, lakini si kwa kukikalia kiti cha kidunia cha mfalme Daudi (taz. pia Zab
2:7-8; 110:1-4).
Katika nafasi kama hizo linatumika neno “maana ya
kiroho”. Kwa ujumla, kadiri ya imani ya kikristo, twaweza kufasili “maana ya
kiroho” kuwa ile maana inayoonyeshwa na matini za Biblia zinaposomwa chini ya
uongozi wa Roho Mtakatifu na ndani ya mazingira ya fumbo la kipasaka la Kristo
na ya maisha mapya yanayotokana nalo. Nayo mazingira ni ya kweli kabisa. Agano
Jipya hutambua ndani yake utimilifu wa Maandiko Matakatifu. Hivyo ni kawaida
kuyasoma upya Maandiko katika mwanga wa mazingira haya mapya, ndiyo yale ya
maisha katika Roho.
Kutokana na fasili hiyo, mengi yaweza
kusisitizwa mintarafu uhusiano baina ya maana ya kiroho na maana sisisi.
Kinyume cha kauli ya kawaida, si lazima kuwepo
tofauti kati ya maana hizo mbili. Kwani, pale matini ya Biblia ilizungumziapo
moja kwa moja fumbo la kipasaka la Kristo ama maisha mapya yatokanayo nalo,
ndipo maana yake sisisi ni tayari maana mojawapo ya kiroho. Ndicho kitokeacho
kama kawaida yake katika Agano Jipya. Hivyo hutokana kwamba ufafanuzi wa
kikristo mara nyingi zaidi huongelea maana ya kiroho ukilielekea Agano la Kale.
Lakini hata kuanzia katika Agano la Kale pana sehemu nyingi ambapo matini zina
maana ya kidini na ya kiroho kama maana yake sisisi. Na katika sehemu hizi
imani ya kikristo inatambua dalili za kwanza za uhusiano wake na maisha mapya
yaletwayo na Kristo.
Iwapo kuna tofauti, maana ya kiroho haiwezi
kamwe kunyimwa uhusiano wake na maana sisisi ambayo inaendelea kuwa msingi wake
wa lazima; kama sivyo, isingewezekana kuuzungumzia “utimilifu” (fulfilment) wa
Maandiko. Na kwa kweli, ili tuweze kuuzungumzia utimilifu, ni sharti uwepo
uhusiano wa mfulizo na uwiano maridhawa baina ya maana hizo mbili. Lakini pia
ni lazima iwepo njia ya kuingia katika kiwango kilicho bora zaidi cha uhalisi.
Maana ya kiroho isichanganywe na fasiri
zinazojengwa juu ya hisia za watu binafsi na zitokanazo na ubunifu wao au na
utafiti wa kiakili (intellectual speculation). Maana hiyo ya
kiroho inazaliwa na uhusiano wa matini na matukio ya kweli yasiyo mageni kwake,
yaani tukio la kipasaka na neema zake zisizokoma; nayo ndiyo kilele cha kazi za
Mungu katika historia ya Israeli, kwa manufaa ya wanadamu wote.
Usomaji wa kiroho, uwe umefanyika kijumuiya ama
kibinafsi, unatambua maana ya kiroho ikiwa tu utajitunza ndani ya mitazamo
hiyo. Ndipo vinaweza kuhusianishwa viwango vitatu hivyo vya uhalisi: matini ya
Biblia, fumbo la kipasaka, na hali halisi ya maisha katika Roho.
Ufafanuzi wa kale ulikuwa na hakika kuwa fumbo
la Kristo ni ufunguo wa kuyafasiria Maandiko yote; hivyo ulijibidisha kuipata
maana ya kiroho katika mambo madogo madogo ya matini za Biblia – kwa mfano,
katika hila agizo la sheria za kiibada – ukitumia mbinu za kirabi au
ukiathiriwa na mbinu za kiistiari za kigiriki (Hellenistic allegorical
method). Ufafanuzi wa siku hizi hauwezi kuzitazama mbinu za
namna hii kama mtindo halisi wa ufasiri, yoyote yale yaliyokuwa manufaa yake ya
kichungaji katika nyakati zilizopita (taz. Divino afflante Spiritu,
EB 553).
Mandhari mojawapo inayokubalika ya maana ya
kiroho ni maana ya kifananisho (typological); nayo kawaida inasemwa kuwa
haiyahusu Maandiko yenyewe, bali yale mambo yanayoelezwa na Maandiko: Adamu ni
mfano wa Kristo (taz. Rum 5:14), gharika ni mfano wa ubatizo (1Pet 3:20-21),
n.k. Ni kweli kwamba uhusiano huo, wa kitu kimoja kuwa mfano wa kingine, kwa
kawaida una msingi wake katika jinsi Maandiko yanavyoeleza kile kitu cha kwanza
(taz. sauti ya Abeli: Mwa 4:10; Ebr 11:4; 12:24), wala si katika kitu kile cha
kwanza chenyewe. Kwa hiyo, hapo tunaweza kusema kwamba hiyo maana imo kweli
katika Maandiko yenyewe.
Jina hili, “maana timilifu” (sensus plenior),
ni msamiati usio wa muda mrefu, nalo linazusha mijadala. Kwa jina “maana
timilifu” inaelezwa maana ya kina zaidi katika matini, maana iliyotakiwa na
Mungu, lakini bila kudhihirishwa wazi na mwandishi mtu. Inawezekana kuigundua
katika matini fulani ya Biblia ikichunguzwa katika mwanga wa sehemu nyingine za
Biblia zinazoitumia, au katika uhusiano wake na maendeleo ya ndani ya ufunuo.
Hapo [maana timilifu] ni maana ile ambayo
mwandishi mtakatifu anaiona katika matini iliyotangulia kuandikwa kabla yake,
pale anapoinukulu katika muktadha unaoipa maana sisisi mpya; au ni maana ile
ambayo mapokeo ya kimafundisho yaliyo halisi, au tamko la Mtaguso, huitia kwenye
matini fulani ya Biblia. Kwa mfano, muktadha wa Mt 1:23 unaleta maana timilifu
kwa maneno ya unabii ya Isa 7:14 kuhusu almah atakayechukua
mimba, kwa kutumia tafsiri ya Septuajinta parthenos: “Bikira atachukua
mimba”. Mafundisho ya Mababa wa Kanisa na ya Mitaguso kuhusu Utatu Mtakatifu
yaleta maana timilifu ya mafundisho ya Agano Jipya kuhusu Mungu Baba, Mwana na
Roho Mtakatifu. Tamko la ufasiri juu ya dhambi ya asili lililotolewa na Mtaguso
wa Trento laleta maana timilifu ya mafundisho ya Paulo katika Rum 5:12-21
kuhusu mapokeo ya kosa la Adamu kwa ajili ya wanadamu wote. Lakini, endapo
udhibiti wa aina hii haupo – ama kutokana na matini ya Biblia iliyo dhahiri ama
na mapokeo ya kimafundisho halisi – kudai kuikimbilia maana timilifu kungeweza
kupeleka kwenye fasiri za kibinafsi zisizo na uzito wowote.
Kwa kifupi, ingewezekana kuitambua maana
timilifu kama njia nyingine ya kuitaja maana ya kiroho ya matini fulani ya
Biblia, pale ambapo maana ya kiroho inatofautiana na maana sisisi. Msingi wake
ni kwamba Roho Mtakatifu, aliye mtunzi mkuu wa Biblia, aweza kuongoza mwandishi
mtu katika kuchagua maneno na sentensi kwa namna ya kwamba zenyewe zaelezea
kweli ambayo yeye haitambui katika kina chake chote. Kweli hiyo yafunuliwa kwa
upana zaidi baada ya muda, kwa njia ya matendo mengine ya Mungu
yanayodhihirisha wazi zaidi maana ya matini, na pia – kwa upande mwingine – kwa
njia ya kuingizwa matini hizo katika orodha rasmi (= “kanoni”) ya Maandiko
Matakatifu.
Kwa namna hiyo unaundwa muktadha mpya,
unaoonyesha uwezekano wa maana nyingine tena, ambazo muktadha wa asili ulikuwa
ukiziacha kivulini.
Ufasiri wa kikatoliki hautafuti kutambulikana
kwa kutumia mbinu ya kisayansi iliyo yake peke yake. Hukubali kwamba moja ya
tabia za matini za Biblia ni kwamba ni kazi ya waandishi watu, waliotumia
nyenzo zao na vyombo ambavyo nyakati zao na mazingira yao viliwapatia. Kwa
hiyo, ufasiri wa kikatoliki unatumia kwa uhuru mbinu na njia za kisayansi
zinazowezesha kuelewa vizuri zaidi maana ya matini, katika muktadha wake wa
lugha, wa kifasihi, kijamii-utamaduni, kidini na kihistoria, kwa kuiangaza pia
kwa uchunguzi wa machimbuko yake na kwa kujali tabia ya kila mwandishi
(taz. Divino afflante Spiritu, EB 557). Kwa maana hiyo, hutoa
mchango kiutendaji kwa kukuza mbinu na kwa maendeleo ya utafiti.
Sifa yake inayoubainisha ni kwamba unajitia kwa
dhati katika mkondo wa mapokeo hai ya Kanisa, ambayo juhudi yake ya kwanza ni
uaminifu kwa ufunuo ulioshuhudiwa na Biblia. Hemenetiki za siku hizi
zimedhihirisha, kama tulivyokumbusha, kwamba haiwezekani kufasiri matini bila
kuanzia toka kwa “ufahamu tangulizi” wa namna moja au nyingine. Ufafanuzi wa
kikatoliki hukaribia maandiko ya Biblia kwa ufahamu tangulizi unaounganisha kwa
ndani utamaduni wa kisayansi wa leo na mapokeo ya kidini yanayotokea kwa
Israeli na kwa jumuiya ya Wakristo wa mwanzoni. Hivyo, ufasiri wake unaendeleza
mkikimkiki wa kihemenetiki unaojionyesha ndani ya Biblia yenyewe, na
unaoendelea halafu katika maisha ya Kanisa. Unalingana na dai la kuwepo mvuto
hai kati ya mfasiri na kitu chake, mvuto ulio moja la masharti yanayowezesha
kazi yake ya ufafanuzi.
Lakini kila ufahamu tangulizi una hatari zake.
Kwa upande wa ufafanuzi wa kikatoliki kuna hatari ya kuzipa matini kadhaa za
Biblia maana zisiyo nayo, bali ambayo ni tunda la ukuaji wa baadaye ya mapokeo.
Mfafanuzi ajitahadhari na hatari hiyo.
Matini za Biblia ni matokeo ya mapokeo ya kidini
yaliyokuwapo kabla yake. Jinsi zinavyounganika na mapokeo hayo ni tofauti kila
mara, kwa sababu ubunifu wa waandishi huonyesha ngazi mbalimbali. Mwaka nenda
mwaka rudi, mapokeo kadhaa yameingiliana kuunda mapokeo makuu ya pamoja. Biblia
ni onyesho bora la mchakato huo, ambao yenyewe ilichangia kuutekeleza na
inaendelea kuuratibu.
“Ufasiri katika mapokeo ya kibiblia” huweza
kutazamwa kwa namna nyingi mbalimbali. Kwa usemi huo inawezekana kumaanisha
jinsi Biblia inavyofasiri mang’amuzi ya msingi ya kibinadamu, au matukio ya
pekee ya historia ya Israeli, au tena jinsi matini za Biblia zinavyotumia, kwa
kuyafasiri, machimbuko mbalimbali, andishi au simulizi, ambayo baadhi yao
huweza kutoka katika utamaduni au dini nyinginezo. Lakini, kwa sababu mada yetu
ni ufasiri wa Biblia, hatutaki kujadili hapa masuala makuu hayo, bali kutoa mawazo
kadhaa kuhusu ufasiri wa matini za Biblia ndani ya Biblia yenyewe.
Kinachosaidia kuipa Biblia umoja wake kiundani,
wa pekee katika aina yake, ni kwamba maandiko ya kibiblia ya baadaye mara
nyingi hutegemea maandiko yaliyotangulia. Yanayadokeza, au yanaleta “kusoma
upya” kunakoendeleza mambo mapya katika maana yake, mara nyingine tofauti sana
na maana ya asili, au tena yanayarejea kwa wazi kabisa, ama kwa ajili ya kwenda
kina katika maana yake, au kwa kudhihirisha utimilifu wake.
Hivyo urithi wa nchi, iliyoahidiwa na Mungu kwa
Ibrahimu kwa ajili ya uzao wake (Mwa 15:7.18), hugeuka kuwa kuingia katika
patakatifu pa Mungu (Kut 15:17), ushirikiano wa raha ya Mungu (Zab 132:7-8)
iliyowekwa kwa waamini wa kweli (Zab 95:8-11; Ebr 3:7-4:11) na, mwishowe,
kuingia katika patakatifu pa mbinguni (Ebr 6:12.18-20), ulipo “urithi wa
milele” (Ebr 9:15).
Uaguzi wa nabii Nathani, unaomwahidia Daudi
“nyumba”, yaani ukoo wa kifalme, “ulio imara milele” (2Sam 7:12-16),
hukumbushwa mara nyingi (2Sam 23:5; 1Nya 17:11-14), hasa katika nyakati za
taabu (Zab 89:20-38), wala si pasipo mabadiliko yenye maana, nao huendelezwa na
maaguzi mengine (Zab 2:7-8; 110:1.4; Amo 9:11; Isa 7:13-14; Yer 23:5-6; n.k.),
ambayo baadhi yake hutangaza kurejeshwa kwa ufalme wa Daudi mwenyewe (Hos 3:5;
Yer 30:9; Eze 34:24; 37:24-25; taz. Mk 11:10). Ufalme ulioahidiwa ukawa ufalme
wa watu wote jumla (Zab 2:8; Dan 2:25.44; 7:14; taz. Mt 28:18). Hutimiza
kikamilifu mwito wa binadamu (Mwa 1:28; Zab 8:6-9; Hek 9:2-3; 10:2).
Uaguzi wa Yeremia kuhusu miaka sabini ya adhabu
waliyostahili Yerusalemu na Yuda (Yer 25:11-12; 29:10) umekumbushwa katika 2Nya
25:20-23, panapohakikisha utekelezaji; lakini hupata maendelezo zaidi, baada ya
muda mrefu, na mwandishi wa kitabu cha Danieli, akiwa na hakika kuwa neno hilo
la Mungu linashika bado maana iliyofichwa, inayopaswa kuangaza hali ya sasa
(Dan 9:24-27).
Tamko la kimsingi la haki ya Mungu katika kutoa
thawabu, ambaye anawajazi wema na kuwaadhibu wabaya (Zab 1:1-6; 112:1-10; Law
26:3-33; n.k.), linagongana na mang’amuzi tunayokuta ambayo mara nyingi
hayapatani nalo. Basi, Maandiko yanaachia kujitokeza kwa nguvu mateto na
upinzani (Zab 44; Ayu 10:1-7; 13:3-28; 23-24) na kuendelea kuchunguza kina cha
fumbo hilo (Zab 37; Ayu 38-42; Isa 53; Hek 3-5).
Mahusiano kati ya matini za Biblia yanaongezeka
sana katika maandiko ya Agano Jipya, ambayo yamejaa madokezo ya Agano la Kale,
na pia nukuu wazi. Waandishi wa Agano Jipya wanatambua kuwa Agano la Kale lina
hadhi ya ufunuo wa kimungu. Wanatangaza kuwa ufunuo huo umepata utekelezaji
wake katika maisha, mafundisho na hasa katika kufa na kufufuka kwake Yesu,
aliye asili ya msamaha na ya uzima wa milele. “Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi
zetu, kama yanenavyo Maandiko; na (...) alizikwa. Na (...)
alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo Maandiko; na alimtokea
Kefa... ” (1Kor 15:3-5): hiki ndicho kiini kamili cha mahubiri ya mitume (1Kor
15:11).
Jinsi ilivyo daima, baina ya Maandiko na matukio
yanayoyatimiza, mahusiano sio ya ulinganifu yakinifu (material
correspondence), bali ya kumulikana hayo kwa hayo, na ya maendeleo ya
kiupembuzi (dialectical): yawezekana kutambua kwa wakati mmoja kuwa
Maandiko hufunulia maana ya matukio, na matukio hufunulia maana ya Maandiko,
yaani yanashurutisha kukataa mambo fulani ya ufasiri uliopokelewa, na kuchukua
ufasiri mwingine mpya.
Tangu wakati wa utume wake hadharani, Yesu
alichukua msimamo wa pekee, mbali na ufasiri wa wakati wake, uliokuwa ule “wa
Mafarisayo na waandishi” (Mt 5:20). Kuna shuhuda nyingi: tabaini (antithesis)
za mafundisho ya mlimani (Mt 5:21-48), uhuru mkuu wake Yesu katika kushika
sheria ya sabato (Mk 2:27-28 na nd.), jinsi yake ya kupunguza ukali wa kanuni
za usafi wa kiibada (Mk 7:1-23 na nd.); na, kinyume chake, madai yake ya lazima
katika mada nyingine (Mt 10:2-12; 10:17-27 na nd.), na hasa msimamo wake wa
kuwakaribisha “watoza ushuru na wakosefu” (Mk 2:15-17 na nd.). Nia yake haikuwa
shauri la ubishi, bali, la uaminifu kamili kwa mapenzi ya Mungu
yalivyodhihirishwa katika Maandiko (rej. Mt 5:17; 9:13; Mk 7:8-13 na nd.;
10:5-9 na nd.).
Kifo na ufufuko wake Yesu vilisukuma hadi mwisho
maendeleo ya ufasiri aliyoanza, na kusababisha, katika mambo kadhaa, utengano
kamili, na, wakati huohuo, ufunguzi usiotarajiwa. Kifo cha Masiya, “mfalme wa
Wayahudi” (Mk 15:26 na nd.), kilisababisha mabadiliko katika ufasiri wa kidunia
wa zaburi za kifalme na wa maaguzi ya kimasiya. Ufufuko wake na kutukuzwa kwake
mbinguni kama Mwana wa Mungu, vilitilia matini hizohizo utimilifu wa maana
usioweza kudhaniwa kabla. Semi fulani zilizoonekana za chuku (hyperbole),
sasa zilipaswa kuchukuliwa jinsi zilivyo. Ikaonekana kwamba ziliandaliwa na
Mungu ili kutambulisha utukufu wa Kristo Yesu, kwa sababu Yesu ni kweli “Bwana”
(Zab 110:1) kwa nguvu kamili ya neno (Mdo 2:36; Flp 2:10-11; Ebr 1:10-12); yeye
ni Mwana wa Mungu (Zab 2:7; Mk 14:62; Rum 1:3-4), Mungu pamoja na Mungu (Zab
45:7; Ebr 1:8; Yn 1:1; 20:28); “Ufalme wake hautakuwa na mwisho” (Lk 1:32-33;
rej. 1Nya 17:11-14; Zab 45:7; Ebr 1:8); na hapohapo yeye ndiye “kuhani wa
milele” (Zab 110:2; Ebr 5:6-10; 7:23-24).
Kwenye mwanga wa matukio ya Pasaka waandishi wa
Agano Jipya walisoma upya Agano la Kale. Roho Mtakatifu aliyepelekwa na Kristo
mtukufu (rej. Yn 15:26; 16:7) aliwafunulia maana yake ya kiroho. Hivyo
walipaswa kukiri kwa nguvu thamani ya kinabii ya Agano la Kale, lakini pia
kupunguza sana thamani yake ya kuwa asasi ya kuleta wokovu. Mtazamo huo wa
pili, ambao huonekana tayari katika Injili (taz. Mt 11:11-13 na nd.; 12:41-42
na nd.; Yn 4:12-14; 5:37; 6:32), unajionyesha kwa nguvu yake yote katika
nyaraka kadhaa za Paulo na katika waraka kwa Waebrania. Paulo na mwandishi wa
waraka kwa Waebrania hudhihirisha kuwa Torati, kwa jinsi ilivyo ufunuo,
hutangaza yenyewe mwisho wake wa kuwa mfumo wa kisheria (taz. Gal 2:15-5:1; Rum
3:20-21; 6:14; Ebr 7:11-19; 10:8-9). Hutokana kwamba wapagani wanaomwamini
Kristo hawapaswi kuwa chini ya amri zote za mfumo wa sheria wa kibiblia, ambao
kwa ujumla, umegeuzwa kuwa asasi ya kisheria kwa taifa maalum, lakini wanapaswa
kulishwa na Agano la Kale kama Neno la Mungu, linalowezesha kugundua vizuri
zaidi upeo wote wa fumbo la kipasaka wanaloishi kwalo (taz. Lk 24:25-27.44-45;
Rum 1:1-2).
Ndani ya Biblia ya kikristo, mahusiano baina ya
Agano Jipya na Agano la Kale hayakosi magumu. Kuhusu namna ya kutumia matini
maalum, waandishi wa Agano Jipya hakika walitumia ujuzi na njia za ufasiri za
wakati wao. Kuwadai wawe wametumia mbinu za kisayansi za leo kungekuwa
kutozingatia utofauti wa nyakati. Badala yake, mfafanuzi lazima ajipatie ujuzi
wa mbinu za kale ili kufasiri kisahihi matumizi yake. Ni kweli, lakini, kuwa
mfafanuzi hatakiwi kutilia tunu kamilifu kwa mambo ambayo hutokana na ujuzi
pungufu wa kibinadamu.
Hatimaye yafaa kuongeza kwamba ndani ya Agano
Jipya, kama ilivyokuwa pia kwa Agano la Kale, hugundulika kupangiliwa pamoja
mitazamo tofauti, na mara nyingine yenye mvutano kati yao, kwa mfano kuhusu
hali ya Yesu (Yn 8:29; 16:32 na Mk 15:34), au kuhusu tunu ya sheria ya Musa (Mt
5:17-19 na Rum 6:14), au kuhusu ulazima wa matendo ili kuhesabiwa haki (Yak
2:24 na Rum 3:28; Efe 2:8-9). Moja ya sifa bainifu za Biblia, kweli, ni kukosa
tabia ya kuratibu, bali kuwemo mivutano ya kimkikimkiki. Biblia imepokea aina
mbalimbali za kufasiri matukio yaleyale, au ya kutazama masuala yaleyale, na
hivyo hualika kukataa kurahisisha mno (excessive simplification), na
ufinyu wa roho.
Kutokana na yale tuliyosema tunaweza kuhitimisha
kwa kusema kuwa Biblia inashika maelekezo na maonyo mengi kuhusu usanii wa
kuifasiri. Naam, Biblia, toka mwanzo, ndiyo yenyewe ufasiri. Matini zake
zimetambuliwa na jumuiya za Agano la Kale na za wakati wa mitume kama uonyesho
na thibitisho halisi ya imani yao. Ni kadiri ya ufasiri wa jumuiya hizo na
kuhusiana nao kwamba matini hizo zilikubaliwa kama Maandiko Matakatifu (ndivyo
ilivyo, k.m., kwa Wimbo ulio Bora uliokubaliwa kama Maandiko Matakatifu kwa
kuutazama uhusiano kati ya Mungu na Israeli). Wakati wa utungaji wa Biblia,
maandiko yaliyomo mara nyingi yametengenezwa upya, na kufasiriwa upya, ili
kuambatana na hali mpya, zisizojulikana kwanza.
Namna ya kufasiri matini, inayoonekana katika
Maandiko Matakatifu, inadokeza maonyo yafuatayo:
Kwa kuwa Maandiko Matakatifu yalikuja kupatikana
kwa msingi wa ukubaliano kamili wa jumuiya za waamini zilizotambua katika
matini yake uonyesho wa imani iliyofunuliwa, ufasiri wake lazima uwe, kwa imani
hai ya jumuiya za kikanisa, chemchemi ya ukubaliano katika mambo ya lazima.
Kwa vile uonyesho wa imani, jinsi ulivyokuwa
ulionekana katika Maandiko Matakatifu yaliyokubaliwa na wote, ulipaswa daima
kutengenezwa upya ili upate kukabili hali mpya – ndiyo sababu ya “kusoma upya”
matini nyingi za Biblia – ufasiri wa Biblia lazima upate kuwa na ubunifu fulani
na kuyakabili masuala mapya yanayojitokeza, ili kuyajadili kwa kuanzia na
Biblia.
Kwa kuwa matini za Maandiko Matakatifu mara
nyingine zina mvutano kati yao, ufasiri unapaswa kuwa wa namna nyingi
mbalimbali. Hakuna ufasiri mmoja pekee unaoweza kutimiza maana ya matini kwa
ujumla, iliyo daima kama sinfonia ya sauti nyingi. Ufasiri wa matini maalumu
unapaswa kuepa kujidai kuwa ule mmoja peke yake.
Maandiko Matakatifu yana mazungumzo na jumuiya
za waamini: yalitokana na mapokeo yao ya imani. Matini zake zimekua katika
mahusiano na mapokeo hayo na kuchangia, wao kwa wao, kwa ukuzaji wake. Hutokea
kwamba ufasiri wa Maandiko hufanyika ndani ya Kanisa katika uwingi wake na
katika umoja wake, na katika mapokeo yake ya imani.
Mapokeo mbalimbali ya imani yalijenga mazingira
hai, ambamo ndani yake ilipatikana amali ya kifasihi ya waandishi wa Maandiko
Matakatifu. Hali hiyo ya kuwemo ndani yake ilihusu pia ushiriki katika maisha
ya kiliturujia, na katika kazi ya nje ya jumuiya, katika ulimwengu wao wa
kiroho, utamaduni wao, na matatizo ya safari yao kihistoria. Ufasiri wa
Maandiko Matakatifu, kwa namna sawia, hudai ushiriki wa wafafanuzi katika
maisha yote na imani yote ya jumuiya ya waamini ya wakati wao.
Mazungumzo na Maandiko Matakatifu kwa ujumla, na
hivyo pia ufahamu wa imani iliyo pekee ya kila zama zilizotangulia, hupaswa
kuandamana na mazungumzo na kizazi cha sasa. Hayo yadai kujiunga na uhusiano wa
mfulizo, lakini pia kutambua tofauti zilizopo. Hutokana kwamba ufasiri wa
Maandiko unapaswa kufanya kazi ya kuhakikisha na kuchambua; unadumu katika
mfulizo na mapokeo ya kifafanuzi yaliyotangulia. ambayo hutunza mambo yake
mengi na kuyafanya kuwa yake; lakini kuhusu mengine unajitenga, ili upate
kuendelea.
Kanisa, taifa la Mungu, linatambua kuwa
linasaidiwa na Roho Mtakatifu katika kuelewa na kufasiri Maandiko. Wanafunzi wa
kwanza wa Yesu walijua kwamba hawakuwa na uwezo wa kufahamu mara katika sura
zake zote utimilifu waliopokea. Kwa kadiri walivyodumu katika maisha yao kama
jumuiya, wao walikuwa wanang’amua kuongezewa zaidi na zaidi ufahamu na
dhihirisho vya kina vya ufunuo waliopokea. Katika hayo walikuwa wakitambua
athari na kazi za “Roho wa kweli”, ambaye Kristo aliahidi kupeleka ili
kuwaongoza awatie katika kweli yote (Yn 16:12-13). Ndivyo Kanisa linavyoendelea
katika safari yake, likitegemezwa na ahadi ya Kristo: “Huyo Msaidizi, huyo Roho
Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote na
kuwakumbusha yote niliyowaambia” (Yn 14:26).
Likiongozwa na Roho Mtakatifu na katika mwanga
wa mapokeo hai liliyopokea, Kanisa lilitambua maandiko yanayopaswa kukubaliwa
kama Maandiko Matakatifu, yaani yale ya [vitabu vile] ambavyo “kwa vile
viliandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu, Mungu mwenyewe ndiye mtunzi wake; na
katika hali hiyo vimekabidhiwa kwa Kanisa lenyewe” (Dei Verbum, 11) na yanashika “ukweli
ambao Mungu alitaka ukabidhiwe kwa Maandiko Matakatifu kwa ajili ya wokovu
wetu” (ibid.).
Kuthibitisha “kanoni” ya Maandiko Matakatifu
kumekuwa hatima ya mchakato mrefu. Jumuiya za Agano la Kale (toka vikundi
maalum, kama duru za kimanabii, au mazingira ya makuhani, hadi taifa kwa
ujumla) zilitambua katika matini kadhaa Neno la Mungu lililoamsha imani yao na
kuwaongoza katika maisha yao; wakapokea matini hizo kama urithi wa kutunzwa na
kupokezwa. Hivyo matini hizo ziliacha kuwa ishara ya kariha ya waandishi
binafsi, na kuwa mali jamii ya taifa la Mungu. Agano Jipya linashuhudia heshima
yake kwa matini hizo takatifu, lilizopokea kama urithi wa thamani kubwa
uliopokelewa kutoka kwa taifa la Waebrania. Linayatambua kama “Maandiko
Matakatifu” (Rum 1:2), “yenye pumzi” la Roho wa Mungu (2Tim 3:16; rej. 2Pet
1:20-21), ambayo “hayawezi kutanguliwa” (Yn 10:35).
Kwa matini hizo ziundazo “Agano la Kale” (taz.
2Kor 3:14), Kanisa liliunganisha maandiko ambamo lilitambua, kwa upande mmoja,
ushuhuda halisi utokao kwa mitume (taz. Lk 1:2; 1Yoh 1:1-3) na kudhaminiwa na
Roho Mtakatifu (taz. 1Pet 1:12), kuhusu “mambo yote aliyoanza Yesu kufanya na
kufundisha” (Mdo 1:1); na, kwa upande mwingine, mafundisho ya mitume wenyewe na
wanafunzi wengine, ili kusimika jumuiya ya waamini. Safu hizi mbili za maandiko
zimepata baadaye jina la “Agano Jipya”.
Katika mchakato huo yaliingia mambo mengi:
uhakika wa kuwa Yesu – na mitume pamoja naye – walitambua Agano la Kale kama
Maandiko yenye pumzi la Mungu, na kuwa fumbo la Pasaka la Yesu lilikuwa
utimilifu wake; imani ya kuwa maandiko ya Agano Jipya yanatokana kwa namna
halisi na mafundisho ya mitume (lakini bila kudai kuwa yalitungwa yote na
mitume wenyewe); kutambua utumiaji wake katika liturujia ya kikristo, na
ulinganifu na mwongozo wa imani; hatimaye, mang’amuzi ya uafikiano wake na
maisha ya kikanisa ya jumuiya na uwezo wake wa kulisha maisha hayo.
Kwa kuthibitisha kanoni (orodha rasmi) ya
Maandiko, Kanisa lilithibitisha pia na kutambulisha tabia yake lenyewe, na
hivyo Maandiko sasa ni kama kioo ambamo Kanisa daima linaweza kujigundua upya
na kupima, karne hadi karne, jinsi linavyoitikia daima Injili, na kujiweka
lenyewe kuwa chombo cha upokezaji (taz. Dei Verbum, 7). Hayo yatilia
maandiko ya kikanoni tunu ya kuleta wokovu na tunu ya kitheolojia mbali kabisa
na maandiko mengine ya kale. Na ikiwa hayo ya mwisho yanaweza kutupia mwanga
kwenye asili ya imani, hayawezi kuchukua kamwe nafasi ya mamlaka ya maandiko
yaliyohesabiwa kuwa ya kikanoni (=rasmi), na hivyo ya msingi kwa ufahamu wa
imani ya Kikristo.
Toka zama za mwanzoni kulikuwa na uhakika
thabiti kuwa Roho Mtakatifu mwenyewe, aliyewasukuma waandishi wa Agano Jipya
kutilia kwenye maandishi ujumbe wa wokovu (taz. Dei Verbum 7; 18), hulipa
pia Kanisa usaidizi wa daima kwa kufasiri maandiko yake yaliyovuviwa (taz.
Ireneo, Adv. Haer. 3.24.1; taz. 3.1.1; 4.33.8; Orijene, De
Princ., 2.7.2; Tertuliani, De Praescr.; 22).
Mababa wa Kanisa, waliokuwa na dhima muhimu
katika mchakato wa uundaji wa kanoni, vilevile walikuwa na dhima ya waanzilishi
kuhusu mapokeo hai yanayosindikiza bila kukoma na kuliongoza Kanisa katika
kusoma na kufasiri Maandiko (taz. Providentissimus Deus, EB
110-111; Divino afflante Spiritu, 28-30: EB 554; Dei Verbum, 23; TKB, Instr.
de Evang histor., 1). Katika mkondo wa Mapokeo makuu, mchango wa pekee wa
ufafanuzi wa Mababa umekuwa hivi: umetokeza kutoka kwa Maandiko kwa ujumla
maelekeo ya msingi yaliyounda mapokeo ya kimafundisho ya Kanisa, na kuleta
utajiri wa mafundisho ya kitheolojia kwa ajili ya kuwafundisha waamini na
kuwalisha kiroho.
Kwao Mababa wa Kanisa, kusoma Maandiko na
kuyafasiri huchukua nafasi muhimu. Ushuhuda hutolewa hasa na kazi zao
zilizounganika moja kwa moja na ufahamu wa Maandiko, yaani homilia na mafasiri
(commentaries); lakini pia kazi za mabishano na za theolojia, ambamo
marejeo ya Maandiko ni hoja muhimu.
Mahali pa kawaida pa kusoma Biblia ilikuwa
kanisani, wakati wa Liturujia. Ndiyo sababu, ufasiri wanaotoa ni daima wenye
tabia ya kitheolojia na ya kiuchungaji, wenye kugusa uhusiano na Mungu, kwa
huduma ya jumuiya na ya waamini binafsi.
Mababa wanatazama Biblia awali ya yote kama
Kitabu cha Mungu, kazi moja ya Mtunzi mmoja; lakini sio kwamba wanawadhania
waandishi binadamu kama vyombo vitupu tu; wanakitia kila kitabu, kimoja kimoja,
lengo pekee. Lakini taratibu yao hutoa uangalifu haba kwa ukuaji kihistoria wa
ufunuo. Mababa wengi wa Kanisa wanamwonyesha Logos, Neno wa Mungu,
kama mtunzi wa Agano la Kale, na kusisitiza, hivyo, kuwa Maandiko yote
yanaongelea Kristo.
Mbali na wafafanuzi wachache wa shule ya
Antiokia (kwa namna ya pekee Theodori wa Mopsuestia), Mababa wanajiona kuwa na
mamlaka ya kuchukua sentensi moja nje ya muktadha wake na kutambua humo ukweli
mmoja uliofunuliwa na Mungu. Katika mabishano na Wayahudi au yale ya kidogma na
wanatheolojia wengine, hawasiti kutegemea fasiri za aina hiyo.
Wakisukumwa hasa na jitihada ya kuishi Biblia
katika ushirika na ndugu zao, Mababa mara nyingi waliridhika kutumia matini ile
ya Biblia ambayo huwa ilitumika katika maeneo yao. Orijene, katika kufanya
juhudi kuiangalia Biblia ya Kiebrania, alisukumwa hasa na bidii ya kutafuta
hoja kwa kupinga Wayahudi, kutokana na matini wanazokubali pia wao. Yeronimo,
akitukuza ukweli wa Kiebrania (veritas ebraica), anachukua msimamo wa
pembezoni.
Mababa wanatumia, zaidi au pungufu, mbinu ya
kiistiari, kwa nia ya kutupilia mbali kwazo ambalo wangeweza kulipata Wakristo
fulani na pia wapinzani wapagani wa Ukristo katika kusoma sehemu hii au ile ya
Biblia. Lakini mara chache sana wanaachana na maana sisisi na tabia ya
kihistoria ya matini. Matumizi ya istiari kwa upande wa Mababa, lazima
yaeleweke tofauti sana na kawaida ya waandishi wapagani ya kutumia mbinu ya
istiari.
Matumizi ya istiari hutokana pia na uhakika kuwa
Biblia, kitabu cha Mungu, kimetolewa naye kwa taifa lake, yaani Kanisa. Kwa
kawaida, hakuna kitu kinachopaswa kuachwa kama kitu kilichopita, au
kimeharibika kabisa. Katika kueleza Biblia, Mababa wanachanganya na kushona
fasiri za ufananisho (typological) na za kiistiari kwa namna isiyoweza
kutengana, daima kwa lengo la kiuchungaji na kimalezi; [wakiamini kuwa] “yote
yaliyoandikwa, yameandikwa kwa kutufundisha sisi (taz. 1Kor 10:11).
Huku wakiwa na hakika kuwa Biblia ni Kitabu cha
Mungu, kwa hiyo kisicho na kina, Mababa wanaamini kuweza kufasiri dondoo fulani
kadiri ya utaratibu maalum wa kiistiari; lakini wanadhani kuwa kila mmoja
anaweza kutokeza kitu tofauti, ilimradi azingatie ulinganifu wa imani.
Ufasiri wa kiistiari wa Maandiko ulio tabia
bainifu ya ufafanuzi wa Mababa, una hatari ya kuyumbisha mtu wa leo; lakini
mang’amuzi ya Kanisa yaliyodokezwa na ufafanuzi huo yanatoa mchango wenye
manufaa daima (taz. Divino afflante Spiritu, 31-32; Dei Verbum, 23). Mababa
wafundisha kusoma Biblia kitheolojia ndani ya Mapokeo hai, kwa roho ya kikristo
halisi.
Kwa vile Maandiko yalitolewa kwa Kanisa, basi,
ni hazina jamii ya mwili wote na waamini: “Mapokeo Matakatifu na Maandiko
Matakatifu yanaunda hazina moja takatifu ya Neno la Mungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa.
Taifa lote takatifu, pamoja na wachungaji wake, likishikamana na hazina hiyo,
linadumu daima aminifu katika mafundisho ya Mitume...” (Dei Verbum, 10; taz. pia 21).
Ni kweli kuwa uzoefu wa waamini wa kusoma Maandiko ulikuwa mkubwa zaidi katika
zama fulani za historia ya Kanisa kuliko zama nyingine. Lakini Maandiko
yalichukua nafasi ya mbele katika nyakati muhimu zote za upyaisho wa maisha ya
Kanisa, toka uamsho wa kimonaki wa karne za kwanza, hadi zama za siku hizi za
Mtaguso wa Vatikano II.
Mtaguso huuhuu unafundisha kuwa wabatizwa wote,
wanaposhiriki, katika imani kwa Kristo, maadhimisho ya Ekaristi, wanatambua
kuwemo kwa Kristo pia katika Neno lake, “kwa sababu ni yeye anayesema wakati
Maandiko Matakatifu yanaposomwa katika Kanisa” (Sacrosanctum Concilium, 7).
Wanakuja kusikiliza neno hilo kwa “utambuzi wa kiimani” (sensum fidei)
iliyo sifa pekee ya taifa lote la Mungu. “Kwa sababu ya utambuzi huo wa imani,
ulioamshwa na kutegemezwa na Roho wa ukweli, taifa la Mungu, chini ya uongozi wa
Majisterio takatifu, linayoifuata kwa uaminifu, lapokea si neno la kibinadamu,
bali kwa hakika neno la Mungu (taz. 1The 2:13). Tena, laishika daima imani
waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu (Yda 3), na kwa hukumu iliyo nyofu
laipenya kwa undani zaidi na kuitia kikamilifu katika maisha yake” (Lumen Gentium, 12).
Hivyo, basi, wanakanisa wote wana dhima yao
katika ufasiri wa Maandiko. Katika utekelezaji wa huduma yao ya
kiuchungaji, maaskofu, wakiwa waandamizi wa mitume, ni mashahidi wa
kwanza na wadhamini wa mapokeo hai ambamo Maandiko yanafasiriwa katika kila
zama. “Hao, wakiangazwa na Roho wa ukweli, kwa njia ya kuhubiri kwao, wanapaswa
kuhifadhi kiaminifu Neno la Mungu, kulifasiri na kulieneza” (Dei Verbum, 9; taz. Lumen Gentium, 25). Wakiwa
wasaidizi wa maaskofu, mapadre wana wajibu wao wa kwanza wa
kutangaza Neno (taz. Presbyterorum Ordinis, 4). Nao
wana karama pekee ya kufasiri Maandiko, pale wanapolinganisha kweli za milele
za Injili na hali halisi ya maisha (ibid.), huku wakitoa siyo maoni yao
binafsi, bali Neno la Mungu. Ni wajibu ya mapadre na mashemasi,
hasa wanapoadhimisha sakramenti, kudhihirisha wazi umoja wa Neno na sakramenti
katika huduma ya Kanisa.
Wakiwa viongozi wa jumuiya ya kiekaristi na
walezi wa imani. wahudumu wa Neno wana kama wajibu wao muhimu sio tu kutoa
mafundisho, bali kusaidia waamini kufahamu na kupambanua Neno linasema nini
moyoni mwao wanaposikiliza na kutafakari Maandiko. Hivyo Kanisa mahalia
lote, kadiri ya mfano wa Israeli, taifa la Mungu (Kut 19:5-6), linakuwa jumuiya
inayojua kuwa Mungu anaongea nayo (taz. Yn 6:45), nalo hufanya juu chini ili
kumsikiliza kwa imani, upendo na utiifu kwa Neno (Kum 6:4-6). Jumuiya hizo,
wanaosikiliza kweli, wanakuwa, katika mazingira yao – ilimradi zadumu zimeungana
na Kanisa lote katika imani na mapendo – moto unaowaka wa uinjilishaji na
dialogia, pia watendaji wa mabadiliko kijamii (taz. Evangelii Nuntiandi,
57-58; CDF, Mafundisho kuhusu uhuru wa kikristo na ukombozi,
69-70).
Roho ametolewa, hakika, hata kwa wakristo
mmoja mmoja ili mioyo yao iweze kuwa “imewaka moto” (taz. Lk 24:32),
wanaposali na kuchunguza Maandiko kisala katika mazingira ya maisha yao
binafsi. Kwa sababu hiyo Mtaguso wa Vatikano II umetaka kwa nguvu kuwafungulia
wazi Maandiko kwa kila namna iwezekanayo (taz. Dei Verbum, 22; 25). Yafaa
kusisitiza kwamba aina hii ya kusoma si ya binafsi hata kidogo, kwa sababu
mwamini husoma na kufasiri daima Maandiko katika imani ya Kanisa, na halafu
huiletea jumuiya matunda ya kusoma kwake, ili kutajirisha imani jamii.
Mapokeo yote ya kibiblia na, kwa namna ya pekee,
mafundisho ya Yesu katika Injili, yadhihirisha kwamba wasikilizaji wapendelevu
wa Neno la Mungu ni wale ambao ulimwengu huwadhania kuwa watu wa hali duni.
Yesu alitambua kuwa mambo mengine yalifichwa kwa wenye akili na hekima, na
kufunuliwa wadogo (Mt 11:25; Lk 10:21), na kwamba Ufalme wa Mungu ni wao walio
kama watoto wadogo (Mk 10:14 na nd.).
Hali kadhalika, Yesu alisema: “Heri ninyi mlio
maskini, kwa sababu Ufalme wa Mungu ni wenu” (Lk 6:21; taz. Mt 5:3). Kati ya
ishara za nyakati za kimasiya linapatikana tangazo la habari njema kwa maskini
(Lk 4:18; 7:22; Mt 11:5; taz. CDF, Mafundisho kuhusu uhuru wa kikristo
na ukombozi, 47-48). Wale ambao, kwa kukosa nguvu na kukosa vifaa vya
kibinadamu, wanasukumwa kuweka matumaini yao kwa Mungu pekee na katika haki
yake, wanao uwezo wa kusikiliza na kufasiri Neno la Mungu unaopaswa kuchukuliwa
maanani na Kanisa zima, pamoja na kudai pia jawabu kijamii.
Kwa kutambua vipaji na wadhifa mbalimbali ambazo
Roho huweka kwa huduma ya jumuiya, na hasa kipaji cha kufundisha (1Kor
12:28-30; Rum 12:6-7; Efe 4:11-16), Kanisa linawapa heshima yake wale
wanaoonyesha uwezo wa pekee wa kusaidia kujenga Mwili wa Kristo kwa umilisi wao
katika ufasiri wa Maandiko (taz. Divino afflante Spiritu, 46-48, EB
564-565; Dei Verbum, 23; TKB, Fundisho
kuhusu tabia ya kihistoria ya Injili, Utangulizi). Ijapo chunguzi zao
hazikupata daima pongezi wanazopokea siku hizi, wafafanuzi (exegetes)
wanaotumikia Kanisa kwa ujuzi wao wanajikuta kuwa katika utajiri wa mapokeo
yanayoenea toka karne za mwanzoni, pamoja na Orijene na Yeronimo, hadi nyakati
za karibuni, pamoja na padre Lagrange na wengine, na kuendelea hadi siku hizi.
Hasa, utafiti wa maana sisisi ya Maandiko, ambayo leo hukaziwa sana, hutaka
jitihada jamii ya wale walio na umilisi wa lugha za kale, wa historia na
utamaduni, wa uhakiki wa matini na wa uchanganuzi wa fani za kifasihi, na ambao
wanajua kutumia mbinu za uhakiki wa kisayansi. Licha ya kujali matini katika
muktadha wake wa asili kihistoria, Kanisa linawategemea wafafanuzi wanaosukumwa
na Roho yuleyule aliyevuvia Maandiko, ili kuhakikisha kuwa “watumishi wa Neno,
kwa wingi uwezekanavyo, waweze kweli kuwaandalia taifa la Mungu lishe ya
Maandiko” (Divino afflante Spiritu, 24; 53-55; EB 551, 567; Dei Verbum, 23; Paulo
VI, Sedula Cura, 1971). Sababu ya kuridhika imetolewa,
katika nyakati zetu, na idadi inayoongezeka ya wanawake wafafanuzi,
wanaotoa mara nyingi, katika ufasiri wa Maandiko, mitazamo mipya na ya kina, na
kutilia nuru mandhari zilizokuwa zimesahauliwa.
Ikiwa Maandiko, tulivyokumbusha hapo juu, ni
hazina ya Kanisa zima na sehemu ya “urithi wa imani” ambao wote, wachungaji kwa
waamini, “wanatunza, wanaungama na kutekeleza kwa jitihada jamii”, lakini ni
kweli kuwa “jukumu la kutoa ufasiri halisi wa Neno la Mungu lililoandikwa au
kupokewa umekabidhiwa tu kwa Majisterio hai ya Kanisa, ambayo mamlaka yake
inatekelezwa kwa jina la Yesu Kristo” (Dei Verbum, 10). Basi,
mwishowe, ni jukumu la Majisterio kuhakikisha uhalisi wa ufasiri na kuonyesha,
ikitakiwa, kuwa ufasiri huu ama huo haupatani na uhalisi wa Injili. Hutekeleza
jukumu hilo ndani ya koinonia (ushirika) ya Mwili, kwa
kukiri rasmi imani ya Kanisa kwa ajili ya kutumikia Kanisa; kwa lengo hilo,
huhoji wanatheolojia, wafafanuzi na wataalamu wengine, ambao inatambua haki ya
uhuru wao, na pamoja nao imo katika muungano kwa lengo la pamoja la “kulinda
taifa la Mungu katika ukweli unaofanya huru” (CDF, Mafundisho kuhusu
wito wa mwanatheolojia katika Kanisa, 21).
Jukumu la mfafanuzi mkatoliki lina dhima nyingi.
Ni jukumu la kikanisa, kwa sababu ni kuchunguza na kueleza Maandiko Matakatifu
kwa jinsi ya kuweka utajiri wake wote kwa matumizi ya wachungaji na waamini.
Lakini, wakati huohuo, ni jukumu la kisayansi, linalomweka mfafanuzi mkatoliki
kuhusiana na wasomi wenzake wasio wakatoliki na katika sekta nyingi za utafiti
wa kisayansi. Kwa upande mwingine, jukumu hilo linashika wakati huohuo kazi ya
utafiti na ya ufundishaji. Zote mbili kwa kawaida hupeleka kwenye kuandika
makala na vitabu.
Wakijitahidi katika jukumu lao, wafafanuzi
wakatoliki wanapaswa kuchukua mtazamo nyeti wa tabia ya
kihistoria ya ufunuo wa kibiblia. Maana, Maagano yote mawili
yanatokeza kwa maneno ya kibinadamu, yanayobeba alama za nyakati zao, ufunuo wa
kihistoria aliofanya Mungu, kwa namna nyingi, kuhusu Yeye mwenyewe na kuhusu
mpango wake wa wokovu. Kwa hiyo, wafafanuzi lazima watumie mbinu ya
kihistoria-kiuhakiki, lakini bila kutaka kuitumia pekee (exclusivity).
Mbinu zote zinazohusu ufasiri wa matini zinaruhusiwa kuleta mchango wao kwa
ufafanuzi wa Biblia. Katika kazi yao ya kufasiri, wafafanuzi wakatoliki
wasisahau kamwe kwamba wanachofasiri ni Neno la Mungu. Jukumu lao
haliishi baada ya kubainisha machimbuko, kuainisha fani au kueleza taratibu za
kifasihi. Lengo la kazi yao litakuwa limetimia pale tu wanapodhihirisha wazi
maana ya matini ya Biblia kama Neno la Mungu kwa siku za leo. Kwa hiyo, lazima
watilie maanani mitazamo mbalimbali ya kihemenetiki inayosaidia kudaka nguvu
kwa leo ya ujumbe wa Biblia na kuuwezesha kuitikia mahitaji ya wasomaji wa siku
hizi wa Maandiko.
Jukumu la wafafanuzi ni pia kueleza maana ya
kikristolojia, ya kikanoni, na ya kikanisa, ya Maandiko ya Biblia.
Maana ya kikristolojia ya matini za Biblia si dhahiri kila mara; lazima
kuiweka nuruni kila inapowezekana. Ijapo Kristo alifunga Agano Jipya katika
damu yake, vitabu vya Agano la Kwanza havikupoteza thamani yao. Kwa vile
vimechukuliwa katika tangazo la Injili, vinapata na kuonyesha maana yake kamili
katika “fumbo la Kristo” (Efe 3:4), kwa kuangaza mandhari zake mbalimbali, na,
wakati huohuo, kwa kuangazwa nalo. Kwani, vitabu hiyo vilitayarisha taifa la
Mungu kwa ujio wake (taz. Dei Verbum, 14-16).
Kila kitabu cha Biblia, ijapo kimeandikwa kwa
lengo maalum na kuwa na maana yake pekee, hujionyesha kuleta maana ya ziada kinapokuwa
kimeingizwa katika jumla ya kanoni rasmi ya vitabu vitakatifu.
Jukumu la wafafanuzi linahusu pia kuonyesha ukweli wa usemi wa Mt. Augustino:
“Novum Testamentum in Vetere latet, et in Novo Vetus patet” (“Agano Jipya
hufichika katika Agano la Kale, na katika Agano Jipya hudhihirika la Kale”;
taz. Mt. Augustino, Quaest. in Hept., 2:73: CSEL 28, III, 3, p.
141).
Wafafanuzi wanapaswa pia kueleza uhusiano uliopo
kati ya Biblia na Kanisa. Biblia imezaliwa katika jumuiya za
waamini. Hudhihirisha imani ya Israeli, na halafu imani ya jumuiya za kikristo
za mwanzoni. Ikiunganika na Mapokeo hai yaliyoitangulia, yanayoisindikiza na
yanayolishwa nayo (taz. Dei Verbum, 21), Biblia ni
chombo kiteule, ambacho Mungu anakitumia kwa kuongoza, hata sasa, ujenzi na
ukuzaji wa Kanisa kama taifa la Mungu. Kisichotengana na eneo la kikanisa ni
mtazamo wazi wa kiekumeni.
Maadamu Biblia hudhihirisha zawadi ya wokovu
ambayo Mungu anawatolea watu wote, jukumu la wafafanuzi linaendana na tabia ya
kujali wote na yote, inayodai kuzingatia dini nyingine na matazamio ya
ulimwengu wa leo.
Jukumu la ufafanuzi ni pana mno, lisitimilizwe
vema na mtu mmoja tu. Hakuna budi kugawanya kazi, hasa kuhusu utafiti,
unaodai wataalamu kwa kila uwanja. Matatizo yatokanayo na kuwa na utaalamu wa
aina moja tu yataepukana kwa njia ya juhudi za kuhusiana kati ya wataalamu wa
fani mbalimbali.
Ni muhimu sana kwa manufaa ya Kanisa zima na kwa
uwezo wake wa kuuathiri ulimwengu wa leo kuwa idadi tosha ya watu
waliotayarishwa vizuri wajishughulishe kwenye utafiti katika sekta mbalimbali
za sayansi ya ufafanuzi. Wakijali mahitaji ya haraka ya huduma, maaskofu na
wakuu wa mashirika ya kitawa, mara nyingi hushawishiwa wasitilie maanani sana
wajibu unaowaangukia wa kushughulikia hitaji hilo la msingi. Lakini upungufu
katika jambo hilo hulihatarisha sana Kanisa, kwa sababu wachungaji na waamini
wangeweza kuelekea kwenye sayansi ya kiufafanuzi iliyo ngeni kwa Kanisa, na
isiyo na mahusiano na maisha ya kiimani. Kwa kukiri kuwa “mtaala wa
Maandiko Matakatifu” lazima uwe “kama roho ya theolojia” (Dei Verbum, 24), Mtaguso wa
Vatikano II ulionyesha umuhimu wote wa utafiti wa kiufafanuzi, na wakati
huohuo, ulitaka kuwakumbusha pia wafafanuzi wakatoliki kuwa utafiti wao una
uhusiano muhimu na theolojia, ambao wanapaswa kuutambua.
Tamko la Mtaguso hutufahamisha dhima ya msingi
ya ufundishaji wa ufafanuzi katika vyuo vya theolojia, katika seminari, na
katika shule za watawa. Ni wazi kuwa kiwango cha mitaala hakitakuwa kilekile
katika taasisi hizo mbalimbali. Ni matumaini kuwa mafunzo ya ufafanuzi yatolewe
na wanaume na wanawake. Yatakuwa ya kina zaidi kisayansi katika vyuo, ila
yatashika mwelekeo moja kwa moja wa kiuchungaji katika seminari; lakini
hayataweza kamwe kukosa eneo pana kielimu. Kufanya tofauti itakuwa kukosa
heshima kwa Neno la Mungu.
Maprofesa wa ufafanuzi lazima watilie kwenye
wanafunzi staha ya kina kwa Maandiko Matakatifu, wakionyesha kuwa yanastahili
somo angalifu na thabiti, linalowezesha kutambua vizuri zaidi thamani yake ya
kifasihi, kihistoria, kijamii na kitheolojia. Hawawezi kuridhika kutoa jumla ya
taarifa za kupokea hivihivi, bali wanapaswa kuwazoesha wanafunzi kuhusu mbinu
za ufafanuzi, kwa kueleza hatua zake maalum, ili kuwawezesha kujimudu kutoa
uamuzi wenyewe. Kwa sababu muda haumtoshi, yafaa mwalimu atumie kwa kubadilibadili
mifumo miwili ya kufundishia: kwa upande mmoja, kwa njia ya maelezo ya usanisi
kuwaingiza katika somo la vitabu vizima kadhaa vya Biblia bila kuacha pembeni
sekta yoyote muhimu ya Agano la Kale, na ya Agano Jipya; kwa upande mwingine,
kwa njia ya uchanganuzi wa kina wa matini zilizochaguliwa kwa makini, ambazo
zitakuwa nafasi za kuwaingiza wanafunzi kwenye mazoezi ya ufafanuzi. Kwa njia
hizo zote mbili, lazima kujitahadhari kutoegemea upande mmoja, yaani kutazama
tu maelezo ya kiroho bila ya msingi ya kihistoria-kiuhakiki, wala maelezo ya
kihistoria-kiuhakiki bila mafundisho ya kiroho (taz. Divino afflante
Spiritu, EB 551-552; TKB, De Sacra Scrittura recte docenda, EB
598). Mafundisho yaonyeshe, kwa wakati mmoja, misingi ya kihistoria ya Maandiko
ya Biblia, hali yake ya kuwa neno binafsi la Baba wa mbinguni anayewaelekea
wanae kwa upendo (taz. Dei Verbum, 21), na dhima yake
ya lazima katika huduma ya kiuchungaji (taz. 2Tim 3:16).
Kama tunda la utafiti na kikomo cha
mafundisho, machapisho yana dhima muhimu sana kwa maendeleo na
uenezi wa ufafanuzi.
Siku zetu hizi machapisho yanatolewa, si tu kwa
njia ya karatasi iliyochapwa, lakini pia kwa njia nyingine, za haraka zaidi na
zenye nguvu zaidi (redio, televisheni, na vyombo vya kielektroniki), ambazo
inafaa kujifunza kuzitumia.
Maandishi ya hali ya juu kisayansi ni chombo
muhimu kuliko vyote kwa ajili ya dialogia, majadiliano na ushirikiano kati ya
wachunguzi. Kwa njia yake, ufafanuzi wa kikatoliki unaweza kujiweka kwenye
uhusiano na shule nyingine ya utafiti wa kiufafanuzi, kama vile na ulimwengu wa
kisayansi kwa ujumla.
Kuna na machapisho mengine ambayo hutoa huduma
kubwa sana, kwa kulingana na tabaka mbalimbali za wasomaji, kuanzia wasomaji
wasomi hadi watoto wa katekisimu, kwa kupitia katika vikundi vya Biblia, vyama
vya kitume na mashirika ya kitawa. Wafafanuzi wenye uwezo wa kutekeleza
uenezaji sahihi wanafanya kazi ya kufaa sana na ya faida, kazi iliyo ya lazima
ili kuihakikishia mitaala ya kiufafanuzi uwezo wa kuathiri inaopaswa kuwa nao.
Katika sekta hiyo, hitaji la kutimiliza ujumbe wa Biblia kwa wakati huu (actualisation)
hutambulika kwa nguvu. Nalo linadai kwamba wafafanuzi watilie maanani mahitaji
halali ya wasomi na wataalamu wa nyakati zetu na kupambanua wazi kwa ajili yao
yale yasiyo muhimu kwa vile yanavyokwenda na nyakati, na yale yanayopaswa
kueleweka kama lugha ya kisasili, na hatimaye yale yanayopaswa kutambulika kama
maana halisi, ya kihistoria na ya kuvuviwa. Maandiko ya Biblia hayakutungwa
katika lugha ya leo, wala katika mtindo wa karne ya ishirini. Fani za usemi na
tanzu za fasihi zinazotumika katika matini za Kiebrania, Kiaramayo au Kigiriki
lazima zitafsiriwe kwa namna ya kufahamika kwa wanaume na wanawake wa leo,
ambao, pasipo hivyo, wangeshawishiwa ama kutojali Biblia ama kuifasiri kwa
namna duni: iwe ya kiherufi, au ya ubunifu.
Katika jukumu lake lenye dhima nyingi, mfafanuzi
Mkatoliki hana lengo lingine ila kulihudumia Neno la Mungu. Fahari yake si
kuweka matokeo ya kazi yake mahali pa matini za Biblia, iwe ni kutengeneza hati
za kale zilizotumiwa na waandishi waliovuviwa, ama kuelezea kisasa mahitimisho
ya mwisho ya sayansi ya ufafanuzi. Kinyume chake, fahari yake ni kuzitilia nuru
zaidi matini zenyewe za Biblia, kwa kusaidia kuzithamini zaidi na kuzifahamu
kwa hakika zaidi kihistoria na kwa kina zaidi kiroho.
Ufafanuzi, ukiwa wenyewe fani ya kitheolojia,
“fides quaerens intellectum” (imani inayotafuta ufahamu), una mahusiano na fani
nyingine za kitheolojia, yaliyo ya makini na uchangamano. Naam, kwa upande
mmoja theolojia mpangilio inaathiri ufahamu tangulizi (pre-comprehension)
ambao kwao wafafanuzi hukaribia matini za Biblia. Lakini, kwa upande mwingine,
ufafanuzi unazipa fani nyingine za kitheolojia data zilizo za msingi kwazo.
Basi, kati ya ufafanuzi na fani nyingine hujengwa mahusiano ya dialogia, kwa
kuheshimiana katika upekee wa kila moja.
Wanapochunguza matini za Biblia, wafafanuzi bila
shaka wanakuwa na ufahamu tangulizi. Kwa upande wa ufafanuzi wa kikatoliki, ni
ufahamu tangulizi unaotegemea hakika za imani: Biblia ni maandiko yaliyovuviwa
na Mungu na kukabidhiwa kwa Kanisa ili kuamsha imani na kuongoza maisha ya
kikristo. Hakika hizo za imani haziwafikii wafafanuzi katika hali ghafi, bali
baada ya kufasiriwa katika jumuiya ya kikanisa na utafakari wa kitheolojia.
Wafafanuzi, basi, wanaelekezwa katika utafiti wao na utafakari wa wanatheolojia
wa kidogma kuhusu uvuvio wa Maandiko na kuhusu dhima yake katika maisha ya
kikanisa.
Lakini, kwa kupeana, kazi ya wafafanuzi juu ya
matini zilizovuviwa huwapatia mang’amuzi ambayo wanatheolojia wa kidogma
wanapaswa kujali ili kudhihirisha zaidi theolojia ya uvuvio wa Maandiko na ya
ufasiri wa kikanisa wa Biblia. Ufafanuzi huamsha, kwa namna ya pekee, dhamiri
hai zaidi na sahihi zaidi kuhusu tabia ya kihistoria ya uvuvio wa Biblia.
Huonyesha kuwa mchakato wa uvuvio ni wa kihistoria si tu kwa sababu ulikuwako
katika historia ya Israeli na ya Kanisa la awali, lakini pia kwa sababu
umetekelezwa kwa njia ya wanadamu walioguswa na zama yao, na ambao, wakiongozwa
na Roho, walikuwa na dhima kiutendaji katika maisha ya taifa la Mungu.
Aidha, tamko la kitheolojia la kuwepo uhusiano
makini kati ya Maandiko yaliyovuviwa na Mapokeo ya Kanisa lilihakikishwa na
kukamilishwa kwa njia ya ukuaji wa mitaala ya kiufafanuzi, ambao uliwapa
wafafanuzi nafasi ya kuzingatia zaidi na zaidi uwezo wa kuathiri wa mazingira
hai ambamo matini zilitengenezwa (“Sitz im Leben”).
Maandiko Matakatifu, bila kuwa locus
theologicus (= chimbuko la theolojia) pekee, yamekuwa msingi ulio bora
zaidi wa mitaala ya kitheolojia. Ili kufasiri Maandiko kwa usahihi wa kisayansi
na kwa uhakika, wanatheolojia wanahitaji kazi ya wafafanuzi. Kwa upande wao,
wafafanuzi sharti waelekeze utafiti wao jinsi kwamba “mtaala wa Maandiko
Matakatifu” uweze kweli kuwa “kama roho ya theolojia” (Dei Verbum, 24). Kwa hiyo
lazima kutilia mkazo pekee maudhui ya kidini ya maandishi ya Biblia.
Wafafanuzi wanaweza kuwasaidia wanatheolojia
kuepa hatari mbili: kwa upande mmoja, thania (dualism), inayotenga
kabisa ukweli mmoja wa kimafundisho na usemi wake kisarufi, unaodhaniwa usio na
maana; kwa upande mwingine, ufundamentalisti, ambao, kwa kuchanganya kilicho
cha kibinadamu na kilicho cha kimungu, hudhania kuwa ni ukweli uliofunuliwa
hata zile mbinu zilizo za kupita za usemi wa kibinadamu.
Kwa ajili ya kuepa hatari hizo mbili, lazima
kubainisha bila kutenganisha, na kukubali, basi, mvutano unaodumu. Neno la
Mungu lilijidhihirisha kwa njia ya waandishi wanadamu. Fikra na semi ziko
wakati huohuo za Mungu na za binadamu; kwa hiyo yote katika Biblia hutoka kwa
Mungu na kwa mwandishi aliyevuviwa, kwa wakati mmoja. Lakini, si kusema kuwa
Mungu aliitia tunu kamilifu kwa athari ya kihistoria juu ya ujumbe wake. Maana,
huo ujumbe uko tayari kufasiriwa na kuhusishwa kisasa, yaani kutengwa, walau
kwa kiasi fulani, na taathira ya kihistoria ya zamani ili upandikizwe katika
taathira ya kihistoria ya sasa. Mfafanuzi huweka misingi ya shughuli hiyo,
ambayo mwanatheolojia wa kidogma anaendeleza, akizingatia loci
theologici nyingine zinazochangia ukuaji wa dogma.
Maoni kama hayo yanaweza kutolewa pia kuhusu
mahusiano kati ya ufafanuzi na theolojia ya maadili. Biblia huunganisha
barabara masimulizi ya historia ya wokovu na maonyo kadhaa kuhusu mwenendo
unaopasika: k. v. amri, makatalio, maagizo ya kisheria, maonyo na ole za
manabii, mashauri ya wenye hekima. Jukumu mojawapo la ufafanuzi ni kuhakikisha
uzito wa mambo mengi hayo na hivyo kuandaa kazi ya wanatheolojia ya maadili.
Jukumu hilo si rahisi, kwa sababu matini za
Biblia, hazishughulikii kupambanua kati ya amri za maadili zilizo za wote, na
miongozo ya usafi kiibada, na taratibu maalum za kisheria. Yote yamechanganyika
pamoja. Tena, Biblia huonyesha maendeleo ya kimaadili makubwa sana, yanayopata
utimilifu wake katika Agano Jipya. Basi, haitoshi kuwa msimamo fulani katika
maadili ushuhudiwe katika Agano la Kale (k. m. matumizi ya utumwa, au ya
talaka, au ya mauaji halaiki katika vita) ili uhesabiwe kuwa halali bado. Ni
lazima kuwepo upambanuzi unaozingatia maendeleo yaliyotokea ya dhamiri ya
kimaadili. Maandishi ya Agano la Kale yanayo ndani yake mambo “ambayo
hayajakamilishwa na ya muda” (Dei Verbum, 15), ambayo
utaratibu wa malezi ya Mungu haukuweza kuyafuta mara moja. Agano Jipya lenyewe
si rahisi la kufasiriwa katika uwanja wa maadili, kwa vile linatumia mara
nyingi semi za mifano au za mafumbo (paradoxical), au hata za kuchokoza;
na uhusiano wa wakristo na sheria ya kiyahudi ni hoja yenye mabishano makali.
Wanatheolojia ya maadili wana sababu tosha za
kuwawekea wafafanuzi maswali mengi na muhimu, yatakayochochea utafiti wao. Mara
nyingine inawezekana kupata jibu la kuwa haiko matini inayojadili kwa wazi
suala lililoulizwa. Lakini hata hapo ushuhuda wa Biblia, ukichukuliwa katika
mkikimkiki wake wa jumla wenye nguvu, hautakosa kusaidia kuhakikisha mwelekeo
mmoja wa kina. Kuhusu mambo muhimu zaidi, ni ya msingi maadili ya amri kumi za
Mungu. Agano la Kale hushika tayari ndani yake kanuni za msingi na tunu zinazoongoza
kutenda kikamilifu kulingana na hadhi ya mwanadamu, aliyeumbwa “kwa mfano wa
Mungu” (Mwa 1:27). Agano Jipya linazitilia nuru zaidi kanuni na tunu hizo,
kutokana na ufunuo wa upendo wa Mungu katika Kristo.
Katika hati yake ya 1988 kuhusu ufasiri wa
dogma, Tume ya Kitheolojia ya Kimataifa ilikumbusha kuwa, katika nyakati zetu,
yamelipuka mapambano kati ya ufafanuzi na theolojia ya kidogma; halafu
inatazama michango mizuri ya ufafanuzi wa leo kwa ajili ya theolojia mpangilio
(Ufasiri wa dogma; 1988, C, I, 2). Kwa usahihi zaidi inafaa kuongeza
kwamba mapambano yalisababishwa na ufafanuzi huria (liberal exegesis).
Baina ya ufafanuzi wa kikatoliki na theolojia ya kidogma hayakuwako mapambano
ya jumla, bali mvutano wa wakati fulani. Ni kweli, lakini, kwamba mvutano
unaweza kugeukia mapambano ikiwa toka upande huu ama huo, hukazika tofauti
halali za mitazamo, hadi kuzigeuza kuwa sababu ya upinzani mkali.
Naam, mitazamo ni tofauti, ya ndivyo
inavyopasika kuwa. Jukumu la kwanza la ufafanuzi ni kupambanua kikamilifu maana
ya matini za Biblia katika muktadha wake wenyewe, yaani katika muktadha wake
maalum wa kifasihi na kihistoria, halafu katika muktadha wa kanoni ya Maandiko.
Kwa kutekeleza jukumu hilo, mfafanuzi hutilia nuru maana ya kitheolojia ya
matini, zinapokuwa na uzito wa aina hii. Hivyo, uhusiano wa kudumu unawezekana
kati ya ufafanuzi na tafakari ya kitheolojia ya baadaye. Lakini mtazamo sio
uleule, kwa sababu kazi ya mfafanuzi ni hasa ya kihistoria na ya kutoa maelezo,
na hubaki kwenye ufasiri wa Biblia.
Mwanatheolojia ya kidogma, kumbe, anafanya kazi
ya kidhana (speculative) na ya kimpangilio (systematic), hasa.
Kwa sababu hiyo anashughulikia hasa matini kadhaa na mandhari fulani za Biblia
na, tena, hushughulikia data nyingine nyingi zisizo za kibiblia – k.v.,
maandishi ya Mababa, matamko ya Mitaguso, hati nyingine za Majisterio,
liturujia –, na pia mifumo ya kifalsafa, na hali ya kiutamaduni, kijamii na
kisiasa ya leo. Kazi yake si ile ya kufasiri Biblia tu, bali ya kuelekea kwenye
ufahamu wa dhati kabisa ya imani ya kikristo, katika maeneo yake yote, na hasa
katika mahusiano katakata na maisha ya kibinadamu.
Kwa sababu ya maelekeo yake ya kidhana na
kimpangilio, theolojia mara nyingi imeangukia kwenye kishawishi cha kuona
Biblia kama akiba ya dicta probantia (= semi zinazothibitisha)
kwa ajili ya kuthibitisha hoja za kimafundisho. Siku hizi zetu wanatheolojia ya
kidogma wamejipatia ufahamu mkali zaidi wa umuhimu wa muktadha wa kifasihi na
wa kihistoria kwa ajili ya ufasiri sahihi wa matini za kale, na kukimbilia
zaidi kutaka msaada wa wafafanuzi.
Kwa vile ni Neno la Mungu liliotiwa kimaandishi,
Biblia ina utajiri wa maana usioweza kudakwa kikamilifu, wala kufungwa katika
theolojia ya kimpangilio yoyote ile. Moja ya dhima muhimu za Biblia ni kuitupia
changamoto mifumo ya kitheolojia na kukumbusha daima kuwemo kwa mambo ya ufunuo
wa kimungu na ya hali halisi ya wanadamu, ambayo mara nyingine yalisahauliwa au
kupuuzwa kwenye juhudi za utafakari wa kimpangilio. Upyaisho wa mbinu za
ufafanuzi unaweza kuchangia kuja kutambua zaidi.
Na kwa upande wake, ufafanuzi hauna budi
kukubali kuangazwa na utafiti wa kitheolojia. Utafiti huo utauchochea kutilia
matini maswali muhimu na kufunua kwa wazi zaidi nguvu zake zote na utajiri
wake. Uchunguzi wa kisayansi wa Biblia hauwezi kuepa utafiti wa kitheolojia,
wala mang’amuzi ya kiroho na upambanuzi wa Kanisa. Ufafanuzi huzaa matunda bora
unapotekelezwa katika mazingira ya imani hai ya jumuiya ya kikristo,
inayotazamia wokovu wa ulimwengu mzima.
Ufasiri wa Biblia, ijapokuwa ni jukumu la pekee
la wafafanuzi, lakini si ukiritimba wao, kwa sababu unahusu, katika Kanisa,
vipengere ambavyo vyapita uchanganuzi wa kisayansi wa matini. Naam, Kanisa
halitazami tu Biblia kama jumla ya hati za kihistoria kuhusu asili yake;
linaipokea kama Neno la Mungu linaloelekezwa kwake, na kwa ulimwengu wote,
katika siku za leo. Hakika hiyo ya imani ina matokeo yake katika juhudi za
kuuhusisha na kuutamadunisha ujumbe wa Biblia, kama vile kuyaratibu matumizi
mbalimbali ya matini zilizovuviwa, katika liturujia, katika “lectio divina”,
katika huduma ya kiuchungaji, na katika harakati ya ekumeni.
Tayari ndani ya Biblia yenyewe – kama
tulivyodokeza katika sura iliyotangulia – tunaweza kuona matumizi ya uhusisho.
Yaani, matini za kale zaidi zimesomwa upya kwenye nuru ya mazingira mapya, na
kulinganishwa na hali ya sasa ya taifa la Mungu. Uhusisho, uliosimama kwenye
dhanio ileile, hauna budi kuendelea kutekelezwa katika jumuiya za waamini.
Kanuni za msingi za matumizi ya uhusisho ni hizi
zifuatazo:
Uhusisho unawezekana, kwa sababu matini ya
Biblia, kwa ajili ya utimilifu wake wa tunu na wa maana, unafaa kwa zama zote
na tamaduni zote (taz. Isa 40:8; 66:18-21; Mt 28:19-20). Ujumbe wa Biblia
unaweza kwa wakati mmoja kupunguza (relativize) na kutajirisha mifumo ya
tunu na kanuni za mwenendo za kila kizazi.
Uhusisho ni wa lazima, kwa sababu, ijapo ujumbe
wa Biblia una thamani ya kudumu, matini zake zilihaririwa kwa kuendana na hali
za mazingira za kale na katika lugha za nyakati zile. Ili kuonyesha uzito zilio
nao kwa wanaume na wanawake wa leo, ni lazima kuambatisha ujumbe wake na hali
ya leo, na kuuweka katika lugha inayolingana na wakati uliopo. Hayo yanadai
juhudi ya kihemenetiki inayotazamia kuzipambanua, ndani ya hali yake ya
kihistoria, pointi muhimu za pekee za ujumbe.
Uhusisho lazima uzingatie daima mahusiano
changamano yaliyomo, katika Biblia ya kikristo, kati ya Agano Jipya na Agano la
Kale, kwa vile Agano Jipya linavyojionyesha kama utimilifu wa Agano la Kale, na
wenye kulipita. Uhusisho hutendeka kulingana na umoja wa kimkikimkiki ulioundwa
hivyo.
Uhusisho hutekelezwa kwa njia ya mkikimkiki wa
mapokeo hai ya jumuiya ya imani. Hayo huwekwa wazi katika mwendelezo wa jumuiya
zile zilizoyazaa Maandiko Matakatifu, zilizoyatunza na kuyapokeza. Katika
kutekeleza uhusisho, mapokeo yatimiza dhima za aina mbili: kwa upande mmoja,
yanalinda dhidi ya ufasiri haramu, na kwa upande mwingine, yanahakikisha kwamba
mkikimkiki wa asili uendelee kupokezwa.
Uhusisho, basi, haumaanishi kuvuruga matini. Si
shauri la kutupia kwenye maandishi ya Biblia, maoni au itikadi mpya, bali ni
kutafuta, kwa unyofu, mwanga yanaoshika ndani yake kwa ajili ya wakati wa leo.
Matini ya Biblia ina mamlaka kwa nyakati zote juu ya Kanisa la kikristo na,
ijapo zimepita karne nyingi tangu utungaji wake, unaendelea kushika wadhifa
wake wa mwongozo mkuu usioweza kuvurugwa. Majisterio ya Kanisa “haiko juu ya
Neno la Mungu, bali hulitumikia, ikifundisha yale tu iliyoyarithi. Kwani, kwa
amri ya Mungu na kwa msaada wa Roho Mtakatifu, hulisikiliza Neno kwa uchaji,
kulihifadhi kitakatifu, na kulieleza kiaminifu” (Dei Verbum, 10).
Kutokana na kanuni hizo, inawezekana kutumia
mbinu anuwai za uhusisho.
Uhusisho, uliofanyika hata ndani ya Biblia,
uliendelea katika Mapokeo ya kiyahudi kwa njia ya mbinu zinazopatikana
katika Targumim na katika Midrashim: kutafuta
madondoo yaliyo sambamba (gezerah shawah), kubadili namna ya kusoma
matini (‘al tiqrey), kuchukua maana ya pili (tartey mishma’),
n.k.
Kwa upande wao, Mababa wa Kanisa walitumia
ufananisho (typology) na istiari ili kuhusisha matini za Biblia kusudi
ziifae hali ya Wakristo wa wakati wao.
Wakati wetu, uhusisho lazima uangalie mabadiliko
ya fikara na ukuaji wa mbinu za ufasiri.
Uhusisho hudai kuanzia na ufafanuzi sahihi wa
matini, wenye kupambanua maana yake sisisi. Ikiwa
mwenye kujishughulisha katika kazi hiyo ya uhusisho hana utaalamu wa ufafanuzi,
lazima ajipatie usaidizi wa miongozo ya kufaa kwa usomaji wake wa Biblia,
inayoweza kumwelekeza vizuri katika ufasiri.
Ili kutekeleza vema uhusisho, ufasiri wa
Maandiko kwa njia ya Maandiko ni mbinu iliyo salama zaidi na ya kufaa sana,
hasa kuhusu matini za Agano la Kale ambazo zilisomwa upya katika Agano la Kale
lenyewe (k. m. “mana” ya Kut 16 katika Hek 16:20-29) na/au katika Agano Jipya
(Yn 6). Uhusisho wa matini fulani ya Biblia katika maisha ya Kikristo hauwezi
kutekelezwa kisahihi yakikosekana mahusiano na fumbo la Kristo na la Kanisa.
Isingekuwa sahihi, kwa mfano, kuwawekea Wakristo, kama vielelezo vya mapigano
ya kujipatia uhuru, masimulizi tu ya Agano la Kale (Kutoka; 1-2 Makabayo).
Mbinu ya kihemenetiki, iliyo na misingi katika
falsafa za kihemenetiki, hudai hatua tatu: 1) kusikiliza Neno kuanzia na hali
ya kisasa; 2) kupambanua vile vipengele vya hali ya kisasa ambavyo matini ya
Biblia huviangaza au kutaka kuvijadili; 3) kuchota katika utimilifu wa maana ya
matini ya Biblia mambo yanayoweza kuendeleza hali ya kisasa kwa namna ya kufaa,
kadiri ya mapenzi ya Mungu ya kuleta wokovu katika Kristo.
Kwa njia ya uhusisho, Biblia huyaangaza masuala
mengi ya sasa, kwa mfano: suala la huduma za aina mbalimbali, tabia ya
kijumuiya ya Kanisa, uamuzi pendelevu kwa maskini, theolojia ya ukombozi, hali
ya wanawake. Uhusisho unaweza pia kuwa makini kwa tunu zilizo nyeti zaidi kwa
dhamiri ya leo, kama vile haki za binadamu, kulinda uhai wa binadamu, kuhifadhi
mazingira, mvuto kwa amani kwa wote.
Ili kuendelea kuafikiana na ukweli wenye kuokoa
ulivyo katika Biblia, uhusisho lazima kujali mipaka fulani na kujihadhari na
hatari ya kukengeuka.
Ijapo kila aina ya usomaji wa Biblia inafanya
uteuzi fulani, lazima kuepukana na usomaji wa kiuzushi, yaani ule ambao badala
ya kuitii matini, unaitumia kwa malengo yake yenye hitilafu (kama ilivyo kwa
uhusisho unaofanywa na madhehebu fulani, kama, k.m., Mashahidi wa Yehova).
Uhusisho hupoteza uhalali wote ukifanyika kadiri
ya kanuni za kinadharia zisizopatana na maelekeo ya kimsingi ya Biblia, kama k.
m., urazini ulio kinyume na imani, au uyakinifu wenye kukana Mungu.
Ni wazi kuwa ya kulaumiwa kila uhusisho
unaoelekea kinyume cha haki na upendo wa kiinjili: kwa mfano ule unaotaka
kusimika kwenye matini za Biblia ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Wayahudi, au
ubaguzi wa kijinsia, iwe wa wanaume au wa wanawake. Uangalifu wa pekee ni wa
lazima, kadiri ya roho ya Mtaguso wa Vatikano II (Nostra Aetate, 4), ili
kuepa kabisa kuzihusisha matini kadhaa za Agano Jipya kwa maana ambayo ingeweza
kuamsha au kutilia nguvu mitazamo hasi dhidi ya Waebrania. Kinyume chake,
matukio ya kutisha ya wakati uliopita yanapaswa kusukuma kukumbusha bila
kuchoka kuwa, kadiri ya Agano Jipya, Waebrania bado “wamekuwa wapenzi” wa Mungu
“kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake” (Rum 11:28-29).
Mikengeuko itaepushwa ikiwa uhusisho utaanzia
katika ufasiri sahihi wa matini na kuendelea katika mkondo wa Mapokeo hai,
chini ya uongozi wa Majisterio ya Kanisa.
Kwa vyovyote, kuwepo hatari za kukengeuka
hakuwezi kuwa upinzani halali dhidi ya utekelezaji wa jukumu la lazima la
kufiki-sha ujumbe wa Biblia hadi masikioni na moyoni mwa vizazi vyetu.
Kwa juhudi za uhusisho, unaowezesha Biblia
kulinda ufanisi wake hata kati ya mabadiliko ya nyakati, hulingana, kadiri ya
tofauti za mahali, juhudi za utamadunisho unaohakikisha kutia mizizi kwa ujumbe
wa Biblia katika nchi zilizo tofauti. Utofauti ambao, lakini, si katika mambo
yote kabisa, kamwe. Maana, kila utamaduni halisi huchukua, kwa namna yake, tunu
za jumla zilizowekwa na Mungu.
Msingi wa kitheolojia wa utamadunisho ni hakika
ya imani ya kwamba Neno la Mungu hupita tamaduni zote ambamo limetungwa, na
lina uwezo wa kuenea katika tamaduni nyingine, kwa jinsi ya kuwafikia wanadamu
wote katika mazingira ya kiutamaduni wanamoishi. Hakika hiyo hutoka katika
Biblia yenyewe, ambayo, tangu Kitabu cha Mwanzo, huchukua mwelekeo kwa wote
(Mwa 1:27-28), na kuushika halafu katika baraka kwa watu wote aliyoahidiwa
Ibrahimu na uzao wake (Mwa 12:3; 18:18), na kuuthibitisha kikamilifu kwa
kueneza kwa “mataifa yote” uinjilishaji wa kikristo (Mt 28:18-20; Rum 4:16-17;
Efe 3:6).
Hatua ya kwanza ya utamadunisho ni kutafsiri
katika lugha nyingine Maandiko yaliyovuviwa. Hatua hii ilianza tangu zama za
Agano la Kale, matini ya Kiebrania ya Biblia ilipotafsiriwa kisimulizi katika
lugha ya Kiaramayo (Neh 8:8.12) na, baadaye kimaandishi kwa Kigiriki. Maana,
utafsiri daima ni zaidi kuliko unukuzi tu wa maandishi ya asili. Kupita toka
lugha moja kwenda lugha nyingine kunadai kwa lazima mabadiliko ya muktadha wa kiutamaduni:
dhana si sawa, na maana ya viashirio ni tofauti, kwa sababu zinahusiana na
mapokeo mengine ya fikra na mitindo mingine ya maisha.
Agano Jipya, lililoandikwa kwa Kigiriki,
limeathiriwa lote na mkikimkiki wa utamadunisho, kwa sababu linatafsiri katika
utamaduni wa Wayahudi wa kiyunani ujumbe wa kipalestina wa Yesu, likionyesha
hivyo nia ya kuvuka mipaka ya eneo moja tu la kiutamaduni.
Kazi ya kutafsiri matini za Biblia, ni hatua ya
kimsingi, ambayo lakini haitoshi ili kuhakikisha utamadunisho wa kweli. Lazima
hiyo kazi ifuatwe na ufasiri unaohusianisha kwa wazi zaidi ujumbe wa Biblia na
aina za hisia, za fikra, za maisha na za kujieleza zilizo pekee za utamaduni
mahalia. Kutoka ufasiri hupigwa hatua nyingine za utamadunisho, ambazo zapeleka
kuunda utamaduni mahalia ulio wa kikristo, wenye kuenea katika sekta zote za
maisha (sala, kazi, maisha ya kijamii, desturi, muundo wa sheria, sayansi na
sanaa, tafakari za kifalsafa na za kitheolojia). Neno la Mungu, basi, ni mbegu
ambayo, kutoka kwa ardhi ilipo, inanyonya mambo ya kufaa kwa ukuaji na uzaaji
wake (taz. Ad Gentes, 22). Ndiyo sababu,
Wakristo wanapaswa kujitahidi kupambanua “utajiri gani Mungu mkarimu aliwajalia
mataifa. Wakati huohuo, inawapasa waamini wajaribu kuumulika utajiri huo na
nuru ya kiinjili, na pia kuuokoa na kuurejesha kwa utawala wa Mungu Mwokozi” (Ad Gentes, 11).
Inavyoonekana, si shauri la mchakato wa njia
moja, bali wa “kurutubishana”. Kwa upande mmoja, utajiri uliomo katika tamaduni
mbalimbali huliwezesha Neno la Mungu kuzaa matunda mapya na, kwa upande
mwingine, mwanga wa Neno la Mungu huwezesha kuchambua yale yanayoletewa na
tamaduni, ili kupinga mambo ya hasara na kuhimiza ukuaji wa yaliyo mema.
Uaminifu kamili kwa nafsi ya Kristo, kwa mkikimkiki wa fumbo lake la Pasaka na
kwa upendo wake kwa Kanisa, husaidia kuepukana na suluhisho za uongo: ile ya
“ulinganisho” wa juujuu wa ujumbe, na ile ya fujo ya mchanganyo-dini (syncretism)
(taz. Ad Gentes, 22).
Katika Ukristo wa Mashariki na wa Magharibi
utamadunisho wa Biblia ulitekelezwa tangu karne za mwanzoni na kuonyesha
matokeo makuu. Lakini, haiwezekani kamwe kuudhania kama umetimilika; kumbe,
sharti ufanyike daima, kuhusiana na mabadiliko endelevu ya tamaduni. Katika
nchi zilizopata uinjilishaji nyakati za karibu kuna suala la aina nyingine.
Naam, wamisionari hawakosi kuleta Neno la Mungu lilivyotamadunishwa katika nchi
zao asilia. Ni lazima Makanisa mapya yajitahidi sana kupita kutoka kwa aina
hiyo ngeni ya utamadunisho wa Biblia hadi aina nyingine, inayolingana na
utamaduni wa nchi yao wenyewe.
Tangu mwanzoni mwa Kanisa, usomaji wa Maandiko
Matakatifu ulihesabiwa kama sehemu muhimu ya liturujia ya kikristo, iliyorithi
kiasi cha liturujia ya sinagogi. Hadi leo Wakristo wanayakaribia Maandiko
Matakatifu sanasana kwa njia ya liturujia, hasa katika maadhimisho ya Ekaristi
ya Dominika.
Kwa ujumla, liturujia, hasa liturujia ya
sakramenti, ambazo adhimisho la Ekaristi ni kilele chake, hutekeleza kikamilifu
uhusisho wa matini za Biblia, kwa sababu huweka tangazo lake kati ya jumuiya ya
waamini waliokusanyika kandokando ya Kristo ili kumkaribia Mungu. Wakati huu
Kristo “yupo katika Neno lake, kwa kuwa ni Yeye anayesema wakati Maandiko
Matakatifu yanaposomwa katika Kanisa” (Sacrosanctum Concilium, 7).
Matini iliyoandikwa imekuwa tena Neno hai.
Marekebisho ya Liturujia yaliyoamuliwa na
Mtaguso wa Vatikano II yalijitahidi kuwaandalia Wakatoliki chakula cha Biblia
kwa wingi zaidi. Utaratibu wa miaka mitatu ya masomo katika Misa ya Dominika
unaipa Injili mahali pa pekee, kwa lengo la kudhihirisha vizuri fumbo la Kristo
kama asili ya wokovu wetu. Kwa kuweka kwa kawaida somo moja la Agano la Kale
kulingana na somo la Injili, utaratibu huo hudokeza mara nyingi njia za ufananisho
kuwa njia ya kufaa kwa ufasiri wa Maandiko. Hiyo, inavyoeleweka, si njia pekee
inayowezekana.
Homilia, inayohusisha kwa wazi zaidi Neno la
Mungu, ni sehemu halisi na muhimu ya liturujia. Tutairejea zaidi hapo mbele,
kuhusu huduma ya kiuchungaji.
Kitabu cha Masomo, kilichoandaliwa kutokana na
maagizo ya Mtaguso (Sacrosanctum Concilium, 35),
kilipaswa kuwezesha kusoma Biblia “kwa wingi zaidi, kutoka sehemu zake
mbalimbali na kwa jinsi inavyofaa zaidi”. Kilivyo sasa, kinatekeleza kwa kiasi
tu maelekeo hayo. Hata hivyo, kuwepo kwake kumeleta mafanikio kwa ekumeni.
Katika nchi kadhaa imesaidia pia kufichua utovu wa mazoea ya Wakatoliki na
Maandiko Matakatifu.
Liturujia ya Neno imekuwa jambo mkataa katika
adhimisho la kila sakramenti ya Kanisa. Si shauri la mfululizo wa masomo tu,
bali hudai pia nyakati za ukimya na sala. Liturujia hiyo, hasa Liturujia ya
Vipindi, huchota katika kitabu cha Zaburi sala ili kuziwezesha jumuiya za
kikristo kusali. Tenzi na maombi zimejaa lugha ya kibiblia na uashiriaji wake.
Hayo yote hudhihirisha jinsi ilivyo lazima ushiriki wa liturujia utayarishwe na
kusindikizwa na mazoea ya kusoma Biblia.
Ikiwa katika masomo “Mungu anasema neno lake kwa
watu wake” (Missale Romanum, n. 35), liturujia ya Neno hudai jitihada
kubwa katika kutangaza masomo, na pia kwa ufasiri wake. Basi, hutamaniwa kuwa
katika malezi ya viongozi wa kesho wa jumuiya na makusanyiko, na pia ya
wasaidizi wao, yazingatiwe madai ya Liturujia ya Neno iliyorekebishwa kweli.
Hivyo, kutokana na jitihada ya wote, Kanisa litaendeleza utume wake
liliokabidhiwa “wa kujilisha mkate wa uzima kutoka katika meza moja ya Neno la
Mungu na pia ya Mwili wa Kristo, na kuwapa waamini” (Dei Verbum, 21).
Lectio divina ni somo, la binafsi au la kijumuiya, la sehemu
ndefu au si ndefu ya Maandiko, yanayopokelewa kama Neno la Mungu, na lenye
kukua chini ya mwongozo wa Roho Mtakatifu, katika tafakari, sala na taamuli.
Juhudi ya kusoma kwa utaratibu Maandiko, hata
kila siku, ni mazoea ya kale ya Kanisa. Kama mazoea ya pamoja, hushuhudiwa
katika karne ya tatu, enzi za Orijene; huyu alikuwa akitoa homilia akianzia na
matini ya Maandiko, kwa kuisoma mfululizo katika siku za juma. Wakati ule
kulikuwepo makusanyiko ya kila siku kwa ajili ya masomo na maelezo ya Maandiko.
Desturi hiyo haikupata daima mafanikio makubwa
kati ya Wakristo, na baadaye ikaachwa (Taz. Orijene, Hom. Gen., X,
1).
Lectio divina kama mazoea hasa ya binafsi, inajulikana katika
mazingira ya wamonaki wa mwanzoni. Katika enzi zetu, hati fundisho ya Tume ya
Biblia iliyokubaliwa na Papa Pius XII iliipendekeza na kuhimiza kwa mafrateri
wote, wa kijimbo na wa kitawa (De Scriptura Sacra, 1950; EB 592).
Sisitizo juu ya lectio divina katika tabia zake mbili, ya
kijumuiya na ya binafsi, hivyo imekuwa tena ya kawaida. Lengo linalokusudiwa ni
kuunda na kulisha “upendo wa kweli na wa kudumu” kwa Maandiko Matakatifu,
chemchemi ya uhai wa ndani na wa uzaaji wa kitume (De Scriptura Sacra; na Divino
afflante Spiritu; EB 591 na 567), na pia kukuza ufahamu bora wa liturujia,
na kuihakikishia Biblia nafasi muhimu katika masomo ya theolojia na katika
sala.
Hati ya Mtaguso Dei Verbum (n. 25)
husisitiza vilevile somo la makini la Maandiko kwa upande wa Mapadre na Watawa.
Aidha – na hili ndilo jambo jipya – huwaalika wote “waamini wa Kristo”
kujifunza “uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu” (Flp 3:8). Hupendekezwa
njia kadha wa kadha. Karibu na somo la binafsi, hushauriwa somo katika kikundi.
Hati ya Mtaguso hukazia kuwa somo la Maandiko lazima lisindikizwe na sala, kwa
sababu sala ndiyo jibu kwa Neno la Mungu linalopatikana katika Maandiko chini
ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Katika taifa la Mungu zimeanzishwa mbinu nyingi
kwa ajili ya somo la kijumuiya, na hakuna budi kuhimiza shauku hiyo ya kumjua
zaidi Mungu na mpango wake wa wokovu katika Yesu Kristo kwa njia ya Maandiko.
Matumizi ya mara kwa mara ya Biblia katika
huduma ya kiuchungaji hushauriwa na Dei Verbum (n. 24), nayo
huchukua mbinu tofauti kadiri ya aina ya hemenetiki wanayotumia wachungaji na
ambayo waamini wanaweza kuielewa. Inawezekana kuona maeneo yake muhimu matatu:
katekesi, mahubiri na utume wa kibiblia. Tena, yanaingia mambo mengi, kadiri ya
kiwango cha jumla cha maisha ya kikristo.
Maelezo ya Neno la Mungu katika katekesi (Sacrosanctun Concilium,
35; Mwongozo wa jumla wa katekesi, 1971,16), chemchemi yake ya
kwanza ni Maandiko Matakatifu, ambayo, yakielezwa katika muktadha wa Mapokeo,
huwa ni chanzo, msingi na kanuni ya mafundisho ya katekisimu. Ingefaa sana
kwamba moja la malengo ya katekesi liwe ni kuingiza kwenye ufahamu sahihi ya
Biblia, na usomaji wake uletao matunda, unaowezesha kufumbua ukweli wa kimungu
uliomo, na kuamsha jibu, la ukarimu mkuu uwezekanavyo, kwa ujumbe ambao Mungu
anawafikishia wanadamu kwa njia ya Neno lake.
Katekesi lazima ianze na muktadha wa kihistoria
wa ufunuo wa kimungu ili kuonyesha watu na matukio ya Agano la Kale na ya Agano
Jipya kwenye mwanga wa mpango wa Mungu.
Halafu, ili kupita kutoka kwa matini ya Biblia
hadi maana yake ya wokovu kwa wakati wa sasa, hutumika taratibu za kihemenetiki
mbalimbali, zinazotokeza maelezo ya aina tofauti. Mafanikio ya katekesi
hutegemea ubora wa hemenetiki inayotumika. Kuna hatari ya kubaki kwenye maelezo
ya juujuu, yanayotazama matukio na watu wahusika wa Biblia, kuendana na
mfululizo wa nyakati tu.
Ni wazi kuwa katekesi haiwezi kutumia Biblia yote,
isipokuwa sehemu ndogo tu ya matini zake. Kwa kawaida, hutumia hasa masimulizi,
katika Agano Jipya na katika Agano la Kale. Husisitiza hasa Amri kumi za Mungu.
Lazima iangalie kutumia sawia maaguzi ya manabii, mafundisho ya vitabu vya
hekima, na hotuba kuu za Injili, kama Hotuba ya mlimani.
Mafundisho kuhusu Injili lazima yapeleke
kukutana na Kristo, ambaye huleta ufunguo wa ufunuo wote ya kibiblia, na
kuwasilisha mwito wa Mungu, ambao kila mmoja anapaswa kuitika. Neno la manabii
na lile la “wahudumu wa neno” (Lk 1:2) halina budi kuonekana kana kwamba
limetolewa sasa kwa Wakristo.
Maonyo sawia yanafaa kwa huduma ya mahubiri,
inayopaswa kutokeza katika matini za kale lishe ya kiroho inayofaa kwa mahitaji
ya sasa ya jumuiya ya kikristo.
Sasa, huduma hiyo hutekelezwa hasa mwishoni mwa
sehemu ya kwanza ya adhimisho la Ekaristi, kwa njia ya homilia inayofuata
tangazo la Neno la Mungu.
Maelezo yanayotolewa katika homilia juu ya
matini za Biblia hayawezi kuingia katika vipengele vingi. Kwa hiyo inafaa
kutilia maanani michango muhimu ya matini hizo, ile ambayo huangazia imani na
huwa na mvuto kwa maendeleo ya maisha ya kikristo, yawe ya kijumuiya au ya
kibinafsi. Kwa kuonyesha michango hiyo, lazima kushughulikia uhusisho na
utamadunisho, kadiri tulivyosema hapo juu. Kwa lengo hilo, inafaa kufuata kanuni
sahihi za kihemenetiki. Kukosa matayarisho katika fani hiyo, matokeo yake ni
kishawishi cha kukataa kuchambua kwa kina katika masomo ya Biblia na kubaki tu
kuhubiri maadili au kuongea kuhusu masuala ya kisasa, bila kuyaangaza na Neno
la Mungu.
Katika nchi mbalimbali yalitolewa machapisho (publications),
kwa msaada wa wafafanuzi, ili kusaidia wanaohusika na uchungaji kufasiri
kisahihi masomo ya Biblia ya liturujia na kuyahusisha kwa namna ya kufaa. Ni
matumaini kuwa juhudi hizo zienee hata zaidi.
Wahubiri lazima waepukane na msisitizo wa upande
mmoja tu kuhusu wajibu zinazowapasa waamini. Ujumbe wa Biblia sharti udumishiwe
tabia yake maalum ya kuwa habari njema ya wokovu uliyotolewa na Mungu. Mahubiri
yatakuwa na manufaa na yatalingana zaidi na Biblia yakisaidia kabla ya yote
waamini “kujua karama ya Mungu” (Yn 4:10), ilivyofunuliwa katika Maandiko, na
kufahamu kwa namna iliyo bora masharti yatokanayo.
Utume wa kibiblia una shabaha ya kujulisha Biblia kama Neno la
Mungu na chemchemi ya uhai. Kwanza, huhimiza kazi ya kutafsiri Biblia katika
lugha mbalimbali, na kusambaza tafsiri hizo. Huamsha na kutegemeza shughuli
nyingi: uundaji wa vikundi vya Biblia, mihadhara kuhusu Biblia, “majuma ya
Biblia”, uchapishaji wa magazeti na vitabu, n.k.
Mchango maalum hutolewa na vyama na harakati za
kikanisa zinazoweka katika nafasi ya kwanza somo la Biblia kwa mtazamo wa imani
na wa uwajibikaji wa kikristo. “Jumuiya ndogondogo” nyingi zinatia Biblia kama
kiini cha mikutano yao na kudhamiria lengo la aina tatu: kujua Biblia, kujenga
jumuiya na kuwahudumia watu. Na hapo pia msaada wa wafafanuzi unafaa ili kuepa
uhusisho usio na misingi. Lakini, ni sababu ya furaha kuona Biblia mikononi mwa
watu wanyonge na maskini, wanaoweza kutilia nuru ya ndani kwa ufasiri na
uhusisho wake kisasa, kwa upande wa mtazamo wa kiroho na wa kimaisha, kuliko
wale wenye sayansi inayojitegemea yenyewe (taz. Mt 11:25).
Umuhimu unaozidi kukua daima wa vyombo vya
upashanaji habari (“mass-media”) – vitabu na magazeti, redio, televisheni –
hudai kuwa tangazo la Neno la Mungu na ujuzi wa Biblia vienezwe kwa bidii kwa
njia ya vyombo hivyo. Dhima maalum sana za vyombo hivyo, na tena, nguvu ya juu
ya kuwaathiri watazamaji wengi hudai matayarisho ya pekee kwa ajili ya utumiaji
wake ili kuepa ufaraguzi usiopendeza, na pia matokeo ya kushangaza chapwa.
Iwe ni katekesi, iwe ni mahubiri au utume wa
kibiblia, matini ya Biblia lazima ionyeshwe daima kwa heshima istahilivyo.
Ijapo ekumeni kama harakati maalum na
iliyoratibishwa si ya siku nyingi sana, wazo la umoja wa taifa la Mungu
unaokusudiwa kurudishwa kwa njia ya harakati hiyo lina misingi ya kina katika
Maandiko. Lengo hilo lilikuwa juhudi ya daima ya Bwana (Yn 10:16; 17:11.20-33).
Inatazamia umoja wa Wakristo katika imani, matumaini na upendo (Efe 4:2-5),
katika kuheshimiana (Flp 2:1-5) na katika mshikamano (1Kor 12:14-27; Rum
12:4-5), lakini pia, na hasa, umoja hai na Kristo, kama matawi katika mzabibu
(Yn 15:4-5), au viungo vya mwili na kichwa (Efe 1:22-23; 4:12-16). Umoja huo
sharti uwe mkamilifu, kwa mfano wa ule wa Baba na Mwana (Yn 17:11-22). Maandiko
hueleza msingi wake kitheolojia (Efe 4:4-6; Gal 3:27-28). Jumuiya ya kwanza ya
kitume ni mfano wake thabiti na hai (Mdo 2:44; 4:32).
Wingi wa masuala ambayo dialogia ya kiekumeni
hukabiliana nao una uhusiano na ufasiri wa matini za Biblia. Baadhi ya masuala
hayo ni ya kitheolojia: elimu ya mambo ya mwisho, muundo wa Kanisa, mamlaka kuu
ya Papa na mamlaka ya pamoja ya Maaskofu, ndoa na talaka, kuwapa daraja la
upadre kwa wanawake, n. k. Mengine ni ya taratibu ya kikanuni na kisheria;
yanahusu uendeshaji wa Kanisa lote zima na wa makanisa mahalia. Hatimaye,
mengine ni ya taratibu hasa ya kibiblia: orodha ya vitabu vya kanoni, masuala
kadhaa ya kihemenetiki, n. k.
Ufafanuzi wa Biblia, ijapo hauwezi kudai kutatua
masuala yote hayo peke yake, hutakiwa kuipa ekumeni mchango muhimu. Maendeleo
yenye maana yamekwisha onekana. Kwa sababu ya kutumia mbinu zilezile na malengo
ya kiekumeni yanayofanana, wafafanuzi wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo
walifikia kuelekeana kwa vikubwa katika ufasiri wa Maandiko, zinavyoonyesha
matini na tanbihi za tafsiri nyingi za Biblia za kiekumeni, na tena vitabu na
makala nyingine pia.
Inafaa, tena, kutambua kuwa, kuhusu mambo kadhaa
ya pekee, tofauti katika ufasiri wa Maandiko mara nyingi zinatia changamoto na
zinaweza kudhihirika kuwa za kutimizana na za kuleta manufaa. Ndivyo ilivyo
zinapoonyesha tunu za mapokeo maalum ya jumuiya za Kikristo mbalimbali na hivyo
kufafanua sura mbalimbali za fumbo la Kristo.
Kwa vile Biblia ilivyo msingi jamii wa kanuni ya
imani, sharti la kiekumeni hudai, kwa Wakristo wote, mwito wa ari wa kusoma
upya Maandiko yaliyovuviwa, katika utiifu kwa Roho Mtakatifu, katika upendo,
katika unyofu na katika unyenyekevu, kuyatafakari na kuyaishi, ili kufikia kwenye
toba ya moyoni na utakatifu wa maisha, ambavyo, pamoja na sala kwa kuomba umoja
wa Wakristo, ni roho ya harakati yote ya kiekumeni (taz. Unitatis
Redintegratio, 8). Ingetakiwa, basi, kufanya kuwe rahisi kwa Wakristo walio
wengi iwezekanavyo kujipatia Biblia, pia kuhimiza uandaaji wa tafsiri za
kiekumeni – kwani matini moja ileile jamii husaidia usomaji na uelewa wa pamoja
–, pia kuchochea vikundi vya sala vya kiekumeni ili kusaidia, kwa njia ya
ushuhuda halisi na hai, kutengeneza umoja katika utofauti (taz. Rum 12:4-5).
HITIMISHO
Kutokana na yaliyosemwa katika hati hii kwa
kirefu – ijapo bado kwa ufupi mno katika pointi nyingi – hitimisho la kwanza
litokanalo ni kwamba ufafanuzi wa kibiblia hutekeleza, katika Kanisa na katika
ulimwengu, jukumu la lazima kabisa. Kutaka kuepukana nao wakati wa kuifasiri
Biblia kungekuwa ndoto ya mchana, na kungeonyesha kukosa heshima kwa Maandiko
yaliyovuviwa.
Wafundamentalisti, kwa kutaka kuwafanya
wafafanuzi kana kwamba wangekuwa watafsiri tu (hivyo wakisahau kuwa kutafsiri
Biblia ni tayari kazi ya ufafanuzi) na wakikataa kuwafuata mbele zaidi katika
uchunguzi wao, hawaelewi kuwa, kwa ajili ya kero, inayostahili sifa, ya kuwa
waaminifu kamili kwa Neno la Mungu, wanashika njia, ambazo kwa kweli,
zinawapeleka mbali na maana halisi ya matini za Biblia, na pia mbali na kupokea
kikamilifu matokeo ya Umwilisho. Neno la milele lilichukua mwili katika wakati
maalum wa historia, katika mazingira ya kijamii na kiutamaduni yanayoeleweka
wazi. Anayetaka kulisikiliza, sharti alitafute kwa unyenyekevu pale
linapopatikana, akikubali msaada wa lazima wa ujuzi wa kibinadamu. Ili kuongea
na wanaume na wanawake, tangu zamani za Agano la Kale, Mungu alitumia kila
kifaa cha lugha ya binadamu, lakini, wakati huohuo, alipaswa kuliweka Neno lake
chini ya masharti ya lugha hiyo. Heshima ya kweli kwa Maandiko yaliyovuviwa
hudai kuwa zitendeke juhudi zote zinazotakiwa ili kuweza kudaka vizuri maana
yake. Kweli, haiwezekani kuwa kila Mkristo afanye mwenyewe binafsi kila aina ya
utafiti, mpaka awezeshwe kuelewa vizuri zaidi matini za Biblia. Kazi hiyo
wanakabidhiwa wafafanuzi, walio wahusika, katika sekta hii, kwa manufaa ya
wote.
Hitimisho la pili ni kwamba tabia yenyewe ya
matini za Biblia hudai kuwa, kwa ajili ya kuzifasiri, uendelee kutumika mbinu
ya kihistoria-kiuhakiki, walau katika hatua zake kuu. Kwa maana, Biblia
haijionyeshi kama ufunuo wa moja kwa moja wa kweli zisizohusiana na wakati,
bali kama ushuhuda wa kimaandishi wa mfululizo wa matukio ambayo kwayo Mungu
hujifunua katika historia ya wanadamu. Mbali na mafundisho matakatifu mengi ya
dini nyinginezo, ujumbe wa Biblia umesimikwa imara katika historia. Hutokana na
hilo kwamba maandishi ya Biblia hayawezi kueleweka barabara bila utafiti wa
taathira zake za kihistoria. Utafiti wa “kidiakronia” hudumu kuwa wa lazima
katika ufafanuzi. Njia za “kisinkronia”, kwa vyovyote, haziwezi kuchukua nafasi
yake. Ili kuweza kufanya kazi kwa mafanikio, lazima kwanza ziyakubali matokeo
ya [utafiti wa kidiakonia], walau kwa ujumla.
Lakini, kisha kutimiza sharti hilo, njia za
“kisinkronia” (ya kibalagha, ya kisimulizi, ya kisemiotiki, na nyingine)
zinaweza kusaidia kufanya upya ufafanuzi, na kutoa mchango wa kufaa sana. Mbinu
ya kihistoria-kiuhakiki, kweli, haiwezi kudai ukiritimba, bali inatakiwa
kutambua mapungufu yake, na pia hatari zilizomo mbele yake. Ustawi wa siku hizi
wa hemenetiki za kifalsafa na, kwa upande mwingine, maoni tuliyotoa kuhusu
ufasiri katika mapokeo ya kibiblia na mapokeo ya Kanisa, vilitilia nuru
mandhari kadhaa za suala la ufasiri, ambazo mbinu ya kihistoria-kiuhakiki
ilitaka kusahau. Kwani, kwa kutaka kukaza vema maana ya matini kwa kuziweka
katika muktadha wao wa kihistoria wa asili, mbinu hiyo huonekana mara nyingine
kukosa kuzingatia umkikimkiki wa maana ya matini na uwezekano wa kukua kwake.
Isipofikia kuchunguza uhariri wa matini, bali hutazama tu masuala ya machimbuko
na utabakishaji (stratification) wa matini, hautimizi kikamilifu jukumu
lake la kiufafanuzi.
Kwa kuwa aminifu kwa Mapokeo makuu, ambayo
Biblia huyashuhudia, ufafanuzi wa kikatoliki lazima uepe – kadiri
inavyowezekana – aina hii ya uharibifu kitaaluma na kudumisha tabia yake ya
kuwa somo la kitheolojia, ambalo lengo lake muhimu ni kwenda kina katika imani.
Hilo halimaanishi bidii pungufu katika utafiti wa kisayansi kamili, wala
uharibifu wa mbinu kwa sababu ya juhudi ya utetezi. Kila sekta ya utafiti
(uhakiki wa matini, mitaala ya lugha, uchanganuzi wa kifasihi, n.k.) ina sheria
zake, zinazopasika kufuatwa kwa uhuru. Lakini hata moja ya sekta hizo maalum ni
lengo linalojitosheleza. Katika utaratibu wa jumla wa jukumu la ufafanuzi,
mwelekeo kwenye lengo kuu lazima ukubaliwe ili kuepesha nguvu kumwagwa bure.
Ufafanuzi wa kikatoliki hauna haki ya kufanana na mkondo wa maji unaopotea
katika mchanga wa uchanganuzi wa uhakiki pindukia. Unatekeleza, katika Kanisa
na katika ulimwengu, dhima iletayo uhai: yaani, kutoa mchango wake kwa
urithishaji halisi zaidi wa maudhui ya Maandiko yaliyovuviwa.
Kwa lengo hilo hasa zinaelekea juhudi za
ufafanuzi wa kikatoliki, kwa kuungana sana na upyaisho wa fani nyingine za
kitheolojia, pia na kazi ya kiuchungaji ya uhusisho na utamadunisho wa neno la
Mungu. Kwa kuchunguza masuala ya leo na kudokeza maoni fulani kuhusu masuala
hayo, inatumainiwa kuwa hati hii imerahisisha, kwa ajili ya wote, ufahamu
dhahiri zaidi wa wajibu wa wafafanuzi Wakatoliki.
Roma, 15 Aprili 1993.
[1] Tunaposema
“mbinu” (method) ya kiufafanuzi tunamaanisha jumla ya taratibu za
kisayansi zinazotumika ili kufasiri matini mbalimbali. Tunaposema “njia” (approach),
maana yake ni utafiti unaoongozwa kadiri ya mtazamo wa pekee.
[2] Matini
ya ibara hii ya mwisho ilipitishwa kwa wingi wa kura 11 juu ya 19; wanne
walipinga na wanne hawakupiga kura (abstension). Waliopinga waliomba
matokeo ya kura yachapishwe pamoja na matini yenyewe. Tume imekubali.
[3] Hemenetiki
ya neno iliyoendelezwa na Gerhard Ebeling na Ernst Fuchs ina chanzo chake
katika njia nyingine [ya ufasiri] na unatokana na uwanja mwingine wa fikra.
Unahusu zaidi theolojia ya kihemenetiki kuliko falsafa ya kihemenetiki. Hata
hivyo, Ebeling akubaliana na waandishi kama Bultmann na Ricoeur katika kusema
kwamba Neno la Mungu linapata maana yake kamilifu likiunganika tu na wale
linaowaelekea.
Comments
Post a Comment