Skip to main content

MAKALA: VIMBUNGA PACHA KUPIGA AFRIKA MASHARIKI TR. 5 NA 6


Mvua Afrika Mashariki: Vimbunga pacha kupiga Alhamisi, Ijumaa

Kimbunga
Vimbunga viwili vinatarajiwa kutua katika pwani ya Afrika Mashariki usiku wa leo Alhamisi na kesho Ijuamaa, mamlaka za hali ya hewa zinaripoti.
Eneo la Puntland nchini Somalia ndilo linalotarajiwa kuathirika zaidi na tufani hiyo.
Kwa mujibu wa wataalamu wa hali ya hewa, mgandamizo wa hali ya hewa ambao ulikuwa ukitengeneza vimbunga hivyo pacha umesababisha mvua kubwa katika nchi tisa za ukanda wa Afrika Mashariki.
Zaidi ya watu 130 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko na maporomoko ya udongo nchini Kenya na Uganda.
Jinsi mvuvi huyu wa Kenya alivyookolewa na ndege katika mafuriko
Sehemu kubwa ya Somalia ni kame kwa muda mrefu, lakini toka mwezi Septemba, mvua kubwa ya zaidi ya mara mbili ya wastani wa kawaida zimekuwa zikinyesha sehemu kadhaa za nchi hiyo.
Kwa ujumla mvua zisizo za kawaida zinanyesha katika baadhi ya maeneo ya Kusini mwa Ethiopia, Tanzania, Djibouti, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini.
Athari za mvua kubwa Afrika Mashariki
Hata hivyo, mvua hizo zinatarajiwa kupungua kasi mara baada ya kutua kwa vimbunga hivyo.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari juu ya vimbunga hivyo.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, mgandamizo katika pwani ya Somalia unatarajiwa kuendelea kuwa mbali na pwani ya Tanzania na hautarajiwi kuwa na madhara kwa Tanzania.
Mafuriko
"...mgandamizo mdogo wa hewa uliopo kusini magharibi mwa bahari ya Hindi (karibu na kisiwa cha Madagascar) unatarajiwa kuimarika na kuelekea kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar, na hivyo unatarajiwa kusababisha ongezeko la mvua pamoja na vipindi vya mvua kubwa hususan katika baadhi ya maeneo ya Pwani ya Kaskazini ya nchi yetu kati ya terehe 5 na 6 Disemba 2019," inaeleza taarifa ya TMA.
"Mamlaka imeendelea kutoa tahadhari ya vipindi vifupi vya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es salaam na Pwani na angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma."

Mada zinazohusiana

Comments